In Summary
  • Klopp ni mmoja wa makocha wanaotajwa kwamba wanafaa kwenye kuinoa Real Madrid ambayo kwa sasa mambo yake si mazuri wakiwa hawana kocha baada ya kufuta kazi Julen Lopetegui na sasa wakinolewa na kocha wa mpito, Santiago Solari.

MADRID, HISPANIA.UNAAMBIWA hivi, kuna kazi nyingine hazikimbiliwi. Moja ya kazi hizo ni kwenda kuwa kocha wa Real Madrid, mabosi wake watakuhesabia kwa jambo moja tu, kushinda kinyume cha hapo, kibarua chako kimeota mbawa.

Hivi karibuni tu, Real Madrid ilimfuta kazi kocha Julen Lopetegui, ikiwa ni miezi michache tu tangu alipopewa kibarua hicho kwenye majira ya kiangazi mwaka huu baada ya Zinedine Zidane kuachana na wababe hao wa Bernabeu.

Ukitaka kujua kwamba kazi ya kuinoa Real Madrid haikimbiliwi, hawa makocha mahiri kabisa, lakini walikataa ofa ya kwenda kuwa makocha kwa wababe hao wa Bernabeu.

5.Antonio Conte

Mtaliano, Antonio Conte amefutwa kazi huko Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita. Lakini, bado hajamalizana na wababe hao wa Stamford Bridge juu ya kulipwa fidia yake, hivyo kwa hivi sasa bado yupo chini ya Chelsea. Kutokana na hilo, Conte ni ngumu kukubali ajira ya moja kwa moja kabla ya kumalizana na Chelsea kwa sababu atakuwa amejiharibia kupata mafao yake. Ripoti zinadai kwamba Real Madrid walimtaka Conte muda mfupi tu baada ya Zinedine Zidane kuondoka Bernabeu. Baada ya kushindwa kumpata Conte wakaamua kumchukua, Julen Lopetegui, ambaye kwa sasa wamemfuta kazi. Baada ya kutokea hilo, imedaiwa kwamba Los Blancos wamerudi mezani kwa Conte kumpelekea ofa nyingine ya kumtaka awe kocha wake. Chochote kitakachotokea acha kitokee, lakini ukweli ni kwamba kwenye majira ya kiangazi ya mwaka huu, Conte aliwakatalia Real Madrid walipomtaka akawe kocha wao.

4.Jurgen Klopp

Kocha wa Kijerumani, Jurgen Klopp yupo kwenye mipango yake matata ya kuijenga Liverpool ili kuwa bora kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mipango yake ni kushinda mataji akiwa na miamba hiyo ya Anfield kabla ya kuachana na timu hiyo. Kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund aliwahi kufuatwa na Real Madrid wakimtaka akawe kocha wao, lakini Mjerumani huyo wala hakutaka maelezo mengi, alichofanya ni kuwagomea tu.

Klopp ni mmoja wa makocha wanaotajwa kwamba wanafaa kwenye kuinoa Real Madrid ambayo kwa sasa mambo yake si mazuri wakiwa hawana kocha baada ya kufuta kazi Julen Lopetegui na sasa wakinolewa na kocha wa mpito, Santiago Solari.

3.Mauricio Pochettino

Kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino amekuwa akihusishwa na kibarua cha Real Madrid kwa muda mrefu sana tangu dirisha la majira ya kiangazi huko Ulaya. Lakini, kutokana na Spurs kuwa na mipango thabiti kwa kujenga uwanja mpya kabisa jambo hilo lilimfanya Pochettino aamue kubaki kwenye timu hiyo.

Hata hivyo, Real Madrid mpango wao upo palepale katika kuhakikisha wanapata huduma yake, lakini kwa sasa itawabili wapambane maana Manchester United nao wanamhitaji. Man United nao wanamtolea macho Muargentina huyo huku wakimtazama, Jose Mourinho mwenendo wake kuona kama kuna kitu anaweza kukifanya cha maana huko Old Trafford.

2.Massimiliano Allegri

“Niliwakatalia Real Madrid. Nilifanya hivyo nilipozungumza kwa simu na Florentino Perez kwa sababu mtu ambaye nazungumza naye ana kwa ana ni rais Agnelli. Namshukuru Florentino kwa ofa, lakini nisingeweza kuibukali kutokana na heshima yangu ninayowapa Juventus,” alisema.

Hata hivyo, ripoti zinadai kwamba kocha Allegri muda wake unaweza kufika tamati mwishoni mwa msimu huko Juventus kama timu hiyo inashindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Juventus imekuwa ikimpa kocha huyo kila anachokihitaji ikiwamo kumsajilia supastaa, Cristiano Ronaldo kwenye dirisha lililopita.

1.Arsene Wenger

Imeelezwa kwamba Madrid walimsaka sana kocha huyo wa zamani wa Arsenal na hilo liliweka bayana kocha huyo.

Wenger alisema wakati Arsenal inajenga uwanja wake wa Emirates, alisaini mkataba wa miaka mitano na katikati ya mkataba huo, Real Madrid walimpelekea ofa ya kutaka kumsajili, lakini hakuondoka akidai asingeweza kuisaliti timu yake. Akiwa hana klabu kwa sasa, Wenger anaweza kubebwa na Real Madrid kutimiza ndoto zao za kunolewa na kocha huyo raia wa Ufaransa. Kocha Wenger siku za karibuni alidai kwamba atarudi kazini kuanzia Januari na haijulikani ni wapi hasa gwiji huyo wa Arsenal atakwenda kufanya kazi.

ADVERTISEMENT