In Summary
  • Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Samuel Lukumay, aliyechaguliwa na wanachama wa klabu hiyo alisema hawezi kuhudhuria usaili wa wagombea hao kwani hawakushirikishwa jambo lolote hatua ya awali.

USAILI wa wagombea 19 katika uchaguzi wa Yanga unaanza leo Alhamisi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF) zilizopo Karume lakini cha kushangaza, usaili huo huenda usiihusishe Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.

Ikumbukwe Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo nchini, Yusuph Singo alikaa kikao wiki iliyopita na Uongozi wa Yanga, TFF na BMT ili kuhakikisha wanakuwa pamoja katika mchakato wote wa uchaguzi huo lakini bado kuna sintofahamu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Samuel Lukumay, aliyechaguliwa na wanachama wa klabu hiyo alisema hawezi kuhudhuria usaili wa wagombea hao kwani hawakushirikishwa jambo lolote hatua ya awali.

“Ngumu kwenda kwasababu hatukushirikishwa jambo lolote, nimechaguliwa na wanachama kwa hiyo nafuata sheria za klabu yangu zinavyotaka, hatujashirikishwa mchakato wowote,” alisema.

Lukumay aliongeza kwamba TFF wanatambuaje kama hao wanaowafanyia usaili ni wanachama hai ikiwa uongozi wa Yanga haujashirikishwa.

“Yanga ndio inajua yupi ni mwanachama wake halali, sasa wanafanyaje usaili ikiwa hawajui kama ni wanachama hai au sio, Yanga ina taratibu zake,” alisema.

TFF tayari ilipitisha majina ya wagombea baada ya kuwafanyia mchujo wa awali na sasa wanaingia hatua ya usaili.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Ally Mchungahela aliliambia Mwanaspoti hatua zote huwashirikisha viongozi wa Yanga lakini hawafiki, hivyo kila hatua wataendelea nayo hata kama hawatakuwepo na leja ya wanachama wataitafuta.

Wagombea watakaofanyiwa usaili nafasi ya Mwenyekiti ni Mbaraka Igangula, Dr Jonas Tiboroha na Erick Ninga, Makamu Mwenyekiti ni Yono Kevela, Titus Osoro, Salum Chota na Pindu Luhoyo.

Wajumbe ni Hamad Islamu, Benjamin Mwakasonda, Silvester Haule, Salim Seif, Shifil Amri, Musa Katabaro, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Kingo, Ally Msigwa, Arafat Haji, Geofrey Mwita, Frank Kalokola, Ramadhan Said, Leonard Marango, Benard Mabula, Christopher Kashiririka, Athanas Kazige na Justin Bisangwa.

Uchaguzi huo unatarajia kufanyika Januari 13 mwakani.

ADVERTISEMENT