In Summary

Tajiri mkubwa (bilionea) wa Abu Dhabi wa ukoo wa watawala wa UAE, Sheikh Khaled bin Zayed Al Nahayan, alisema majuzi kuwa amekubaliana na mmiliki wa klabu ya Newcastle United ya England, Mike Ashley, kununua klabu hiyo iliyoko katika daraja kuu katika soka la England kwa gharama ya Paundi za Uingereza milioni 350.

London, England. Mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi katika Ghuba kati ya taifa dogo la Qatar na majirani zake, wakiongozwa na Saudi Arabia na Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), unaweza kabisa kuanza kujitokeza waziwazi sasa kwenye viwanja vya soka katika England.

Habari nyingi za karibuni zinaelezea kuwa wapinzani kwenye eneo hilo la Ghuba huba wanajiandaa kuzinunua klabu kubwa za soka katika Uingereza.

Tajiri mkubwa (bilionea) wa Abu Dhabi wa ukoo wa watawala wa UAE, Sheikh Khaled bin Zayed Al Nahayan, alisema majuzi kuwa amekubaliana na mmiliki wa klabu ya Newcastle United ya England, Mike Ashley, kununua klabu hiyo iliyoko katika daraja kuu katika soka la England kwa gharama ya Paundi za Uingereza milioni 350.

Wakati habari hizo zinatangazwa, imeelezwa pia kuwa Qatar nayo iko mbioni, na inaendelea na mazungumzo ya kuinunua klabu ya Leeds United wakati habari nyingine zinasema kuwa Saudi Arabia inainyemelea Klabu ya Manchester United.

Maslahi hayo ya nchi za Ghuba yanaweza kuhamisha uhasama kutoka kwenye ngazi ya Bara la Ulaya, ambako kwa zaidi ya miaka 10 sasa UAE imekuwa inaimiliki Klabu ya Manchester City ya England na Qatar inaimiliki Klabu ya Paris Saint- Germain (PSG) ya Ufaransa, na kuufanya ushindani wao wa kiuchumi kuingia  ndani ya viwanja vya England.

Wakati ni dhahiri kuwa umiliki wa Manchester City na PSG umeongeza nguvu zisizokuwa za kijeshi (soft power) za UAE na Qatar, umiliki wa kampuni ya City Football Group wa Klabu ya Manchester City, umetengeneza aina ya umiliki wa kipekee wa kibiashara wa soka ambako kampuni kubwa za Ghuba sasa zimenunua na kumiliki klabu za soka duniani katika nchi za Marekani, Australia, Bara la Asia na Marekani Kusini ikiwemo nchini Uruguay.

Mzunguko wa sasa wa mashindano ya kampuni za Ghuba kununua klabu za England, kwa namna fulani ni sehemu ya mvurugano uliolipuka katika Ghuba, miaka miwili iliyopita wakati kundi la nchi la nchi za eneo hilo zikiongozwa na UAE na Saudia Arabia, zilipoiwekea vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia nchi ndogo lakini tajiri sana ya Qatar.

Hata hivyo, pamoja na vikwazo hiyo, Qatar imeendelea kutamba na mwaka huu katika hali isiyotarajiwa ilishinda mashindano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Bara la Asia yaliyofanyika si kwingine, isipokuwa Abu Dhabi kwenyewe ambako ni sehemu muhimu ya UAE.

Aidha, nchi hiyo ndogo majuzi tu ilifanikiwa kuzima mbinu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), zilizoongozwa na UAE na Saudi Arabia za kulazimisha kupanuliwa kwa wigo wa idadi ya nchi zitakazoshiriki  Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 kutoka 32 hadi 48.

Kama mbinu hizo zingefanikiwa, zingevuruga mno maandalizi ya Qatar ya fainali hizo ambayo tayari yamepamba moto na wachunguzi wa mambo wanadai kuwa hiyo ndiyo ilikuwa shabaha hasa ya Saudi Arabia na UAE kutumia mgongo wa FIFA.

Ushindi huo wa Qatar umekuja kufuatia mlolongo wa jitihada ambazo nyingi zimekwama na nyingine zimepata mafanikio kidogo tu, zikiongozwa na Saudi Arabia na UAE, kuongeza ushawishi na nguvu za nchi hizo katika vyombo vya uendeshaji soka duniani, jitihada ambazo zingeziwezesha nchi hizo mbili kuongeza shinikizo dhidi ya Qatar.

Kasi ya nchi za Ghuba kuongeza nguvu zake duniani kwa njia zisizokuwa za kijeshi inalenga pia kuziwezesha nchi hizo kujionyesha katika sura nyingine tofauti na sura za utawala wa nchi hizo wa kidikteta na kiimla, na uvunjaji mkubwa wa haki za kibinadamu, ukiwemo mfumo wa ajira wa wageni unaolalamikiwa wa kutowathamini ipasavyo.

Kwa nchi hizo, kasi hiyo mpya ina faida kubwa mno kulinganisha na athari za mazingira ya sasa ya utawala wa nchi hizo zenye mitazamo ya kizamani.

Ukweli huo umethibitishwa na jinsi mashabiki wa Klabu ya Manchester City walivyowapokea na kuwakumbatia wamiliki wa Emirati wa klabu hiyo, na kuonyesha utayari wa mashabiki hao kusahau rekodi za kutisha za viongozi wa nchi hizo dhidi ya haki za binadamu katika UAE.

Wakati wa michezo ya ligi kuu ya klabu hiyo, kwa mfano, mashabiki wamekuwa wakiimba wimbo uliotungwa na mwanamuziki wa Marekani mwenye asili ya Afrika katika miaka ya 1920, wa Kum Ba Ya (Come by Here), kwa maneno:  “Sheikh Mansour m’lord, Sheikh Mansour, oh lord, Sheikh Mansour,” wakiwa na maana ya kumsifia Sheikh Mansour bin Zayed, mmiliki wa Manchester City ambaye pia ni Waziri wa Ofisi ya Rais katika UAE, na kaka yake wa mama tofauti, Rais wa UAE, Khalifa bin Zayed Al Nahyan.

   Kama alivyo Sheikh Mansour, mnunuzi wa Newcastle, Sheikh Khaled ambaye himaya yake ya kibiashara imejikita zaidi Dubai kuliko Abu Dhabi, dhahiri naye atataka kuonyesha kuwa umiliki wa klabu hiyo ni wa kwake binafsi - hata kama mtawala mkuu wa Emirati, Prince Sheikh Mohammed bin Zayed, hudhibiti kwa karibu kabisa masuala yote ya kiserikali na ya kibiashara katika Dubai.

Hata hivyo, nchi hizo za Ghuba zimekuwa na kazi ngumu ya kujibu shutuma dhidi ya uendeshaji wa nchi hizo kwa kutumia namna na njia zisizokuwa za kijeshi. Tofauti na UAE na Saudi Arabia, ambazo mara kwa mara hujibu moja kwa moja tuhuma dhidi yao, Qatar imekuwa inajibu tuhuma dhidi yake, hasa tokea kushinda haki ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia la 2022, kwa kuzungumza na wapinzani wake kuliko kukabiliana nao kibabe.

Matokeo yake ni kwamba Qatar, kwa mfano, imefanya mabadiliko hata kama ni kidogo - hata kama yamechelewa mno katika mfumo wake wa kafala ama wa udhamini, ambao huwaweka waajiriwa kwenye huruma ya moja kwa moja ya waajiri wao. Kwa hakika, hata UAE nayo, imefanya mabadiliko kidogo zaidi hata hatua za nchi zimekuwa ni matokeo ya shinikizo la makundi ya watetezi wa haki za binadamu na wale wa ajira ya haki duniani.

Hata hivyo, UAE na Qatar zinaweza kujikuta katika hali ya jitihada zao kurudishwa nyuma na matokeo ya kesi zilizofunguliwa dhidi ya umiliki wao katika soka, hasa kama walifungua kesi hizo watahsinda mahakamani.

Klabu ya Manchester City, kwa mfano, imechukizwa mno na uchunguzi wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kuhusu madai ya klabu hiyo kuvunja na kuvuruga sheria na taratibu za haki za matumizi ya fedha katika uendeshaji wa vilabu.

Adhabu ya kosa hilo inaweza kuzuiwa kushiriki katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa msimu mmoja. Mwenyekiti na mchunguzi mkuu wa chombo cha UEFA kinachofanya uchunguzi katika masuala hayo, Yves Leterme, amewasilisha matokeo ya uchunguzi wa kesi hiyo na mapendekezo yake kwa chombo cha juu zaidi cha maamuzi cha masuala hayo kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Hivyo hivyo, Rais wa PSG ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya UEFA na Mwenyekiti wa Kampuni ya Televisheni ya kutangaza michezo ya beIN Sports katika Qatar, Nasser Al-Khelaifi, wiki iliyopita alifunguliwa mashtaka ya rushwa nchini Ufaransa kuhusiana na mchakato wa kuwania nafasi ya kuandaa mashindano ya mwaka huu ya riadha duniani kwa Qatar.

Katika hoja ambayo inaweza kusambaa na kuingia hata Uingereza, Javier Tebas, Rais wa La Liga - Ligi Kuu ya soka ya Hispania, anazishutumu klabu za Manchester City na Paris Saint-Germain kuwa “klabu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Serikali, moja ikiendeshwa na mapato ya Serikali ya mafuta na nyingine na mapato ya sSerikali ya gesi asili” ambazo zinastahili kufukuzwa kutoka kwenye mashindano ya Ulaya kwa sababu ni tishio kwa mchezo wa soka.

Akiunga hoja ya mashabiki wa Klabu ya Manchester City kukataa shutuma dhidi ya UAE kama “ya kibaguzi”, mwenyekiti wa PSG, Khaldoon al Mubarak amezitupilia mbali shutuma za Tebas akizitaja kuwa ni “matusi ya kibaguzi”.

Hoja hiyo ya ubaguzi inaweza tu kuendelea kukubalika kwa kadri mashabiki wa timu hizo, kama alivyo Howard Hockin, wakiendelea kuamini kuwa ni kweli mashabiki wa klabu hizo wanaweza kuwa ni “wanafiki” ambao hawajali au hawana habari na “uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi za Mashariki ya Kati.”

Mtangazaji huyo wa habari za Klabu ya Manchester City, Hockin, anaongezakuwa,  “Abu Dhabi ni nchi inayoendelea na inayokuja juu na ilitaka kujenga jina na heshima yake kupitia soka. Ni hatua ya kujitangaza na kujijenga sura yake, na sisi hatuna tatizo na jambo hilo.”

“Najua jambo hili linatakiwa kunisumbua lakini halinisumbui. Najua kuwa natakiwa kujali aina ya viatu ninavyovaa vinatengenezwa wapi, kwa mfano kama vinatengenezwa na jasho la watumwa – lakini sijali kabisa. Siuchukulii wala kuungalia mchezo wa soka kama kigezo cha maadili yangu. Siamini kama ninauza utu wangu kwa kuiunga mkono Klabu ya Manchester City.”

Swali kubwa kwa sasa ni kama Hockin ataendelea na msimamo wake endapo tabia za uendeshaji biashara za mmiliki wa klabu hiyo au siasa za UAE yenyewe zitaanza kuwa mzigo kuliko kuwa faida kama ilivyo sasa?

Kesi na masuala ya kisheria yanayomkabili Al-Khelaifi vinaweza katika muda mfupi ujao vikawakabili hata mashabiki wenyewe wa Klabu ya Paris Saint-Germain.

Makala hii imeandikwa na Dk James M Dorsey, mtaalam wa soka na mtunzi wa vitabu kuhusu mchezo huo katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

ADVERTISEMENT