In Summary

Unapoizungumzia nafasi ya kurugenzi ya ufundi, unautaja moyo wa mpira wa nchi nzima sehemu ambayo haitakiwi kuchezewa na kufanyiwa masihara kama tulichofanya wakati wa uteuzi.

KWENYE  maisha hakuna asiyekosea. Hii inamaanisha kila binadamu mwenye afya ya akili, lazima kuna wakati anakosea.
Ni hatua ambayo haikwepeki na kama kuna anayedhani hilo halipo, anguko lake litakuwa baya zaidi na ndipo atashtuka alikosea.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limetangaza rasmi limemfuta kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa     Ufundi, Ami Ninje aliyedumu katika nafasi hiyo kwa miezi tisa pekee.
Mbali na Ninje, TFF pia imelifuta benchi zima la ufundi la kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ya Serengeti Boys kilichoshiriki Fainali za Afcon za vijana zilizofanyika mwaka huu kwenye ardhi ya Tanzania.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Rais wa TFF, Wallace Karia na kudai ni kutokana na kufanya vibaya kwa au matokeo mabaya ya timu hiyo ya vijana.
Hii ni hatua ambayo ilipaswa kuchukuliwa na imefanyika kwa weledi mkubwa bila kuangalia urafiki bali kutanguliza masilahi ya nchi.
Bila kupepesa ni wazi, Ninje hakuwa na ubora wa kuwa mkurugenzi wa ufundi na alionekana wazi hakuwa mtu sahihi kuvaa viatu hivyo.
Unapoizungumzia nafasi ya kurugenzi ya ufundi, unautaja moyo wa mpira wa nchi nzima sehemu ambayo haitakiwi kuchezewa na kufanyiwa masihara kama tulichofanya wakati wa uteuzi.
Haikuwa inaingia akilini kuona mtu kama Sunday Kayuni akipuuzwa alafu Ninje ndiyo sahihi katika eneo hilo, hayo yalikuwa ni masihara makubwa kwa uhai wa soka letu.
Kwa sasa TFF inajifunza kutokana  na makosa ambayo waliyafanya kwa kukaa chini na kutafuta mtu mwafaka katika nafasi hiyo bila kuangalia kushibana kwa urafiki bali weledi unahitajika.
Mkurugenzi wa ufundi anatakiwa kuwa mtu mwafaka hasa ili kuhakikisha soka letu linatoka katika matope, unaweza kujiuliza unampa Ninje ukurugenzi wa ufundi, anawezaje kumhoji kwa akili ya soka kocha kama Emmanuel Amunike ambaye dunia inamtambua?
Achilia hilo, pia hata maamuzi ya kulifuta benchi la ufundi la Serengeti nayo ni hatua nzuri ya uwajibikaji ambayo TFF imechukua.
Hakika matokeo ya Serengeti waliyoyapata katika fainali ambazo Tanzania alikuwa mwejeji ziliwaumiza wengi na ulikuwa huhitaji kukutana na kiongozi yoyote wa TFF na hata makocha wa timu hiyo.
Serengeti Boys ilipoteza vibaya mechi zake tatu za hatua ya makundi tena wakicheza nyumbani,wakiruhusu mabao 12 wao wakifunga mabao sita mpaka wanatolewa.
Vijana walionekana kuzidiwa na kuacha simanzi kubwa ikiwa ni timu iliyofungwa mabao mengi hasa wakiwa kama timu wenyeji zaidi haikuwa na kitu chochote unahiweza kusema hii timu imetengenezwa au ina makocha wazuri.
Timu yetu ilikuwa na mapungufu mengi ambayo kama kweli makocha waliokuwepo wangekuwa na ubora ni wazi walipaswa kuyafanyia kazi kulingana na muda wa maandalizi makubwa waliyoyapata.
Serengeti haikuwa na mvuto bado ilionekana kanakwamba ni timu iliyokaa kambini kwa wiki mbili wakati ilidumu katika kambi kwa muda mrefu tena ikitumia gharama kubwa.
TFF sasa ni lazima ijifunze kupitia changamoto hizi mbili lakini pia viongozi wa juu wanapaswa kuacha kufanya kazi kwa urafiki na kujuana.
Hiki kinachotokea sasa ni madhara ya kufanya kazi kwa kuangalia sura na kushibana kwa urafiki kitu ambacho katika utawala wowote ni makosa makubwa.
Hakuna maana kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo hafai kabisa au Ami Ninje hapana lakini maana halisi hapa, bado hawakupewa nafasi katika maeneo ambayo ni mwafaka kwao.
Walipaswa kupewa majukumu ya chini kuonyesha kwanza ubora wao huku wakipandishwa taratibu kuliko kilichofanyika hapo kabla.
Ikumbukwe kabla ya Ninje TFF ilimpa nafasi Mirambo ya kuwa mkurugenzi wa ufundi na wadau kupaza sauti wakiona ni kama kituko katika uteuzi.
Imani yetu ni kwamba Rais Karia ambaye ndiyo mtu wa kwanza ambaye atakuwa lawamani mpira ukiharibika atakuwa amejifunza katika hili la kurugenzi ya ufundi na hata uteuzi wa makocha wetu.

ADVERTISEMENT