In Summary

Muziki ni biashara ya nyota, kuna wakati hung’aa, pia hufifia. Muziki ni bahari, kuna kupwa na kujaa. Ukiwa na vyanzo vingine vya mapato, inakuwa rahisi kupiga hatua kubwa kimaisha, lakini pia ni ulinzi wako.

RAIS wa 44 wa Marekani, Barack Obama, alipohutubia Chuo Kikuu cha Howard, Washington DC, Mei 7, 2016, alisema, hivi sasa Michael Jordan kama mchezaji bora wa kikapu wa muda wote, anamiliki timu ya mpira wa kikapu. Jordan ‘MJ’ ni mmiliki wa klabu kongwe ya NBA, Charlotte Hornets.

Obama alisema: “Nilipokuwa namaliza chuo, mtu mweusi aliyekuwa anang’ara kwenye TV alikuwa Mr T (mcheza myeleka), utamaduni wa mtu mweusi ulikuwa Hip Hop, watu walirap mitaani kama chipukizi, lakini sasa Shonda Rhymes anang’ara na shoo ya Thursday Night, Beyonce anatikisa dunia.

“Siku hizi mtu mweusi haishii kuwa mburudishaji, kumiliki studio za muziki, CEO wa kampuni ndogo, meya au mwakilishi, sasa mtu mweusi ni Rais wa Marekani.” kipindi Obama anatoa hotuba hiyo alikuwa bado Rais.

Hapa kuwataja wachache; MwanaFA, AY, Prof Jay, Diamond Platnumz, Sugu na Ali Kiba, wamepanda vyeo, kutoka kutegemea muziki kuishi, kungojea simu za mapromota kwa ajili ya shoo, stresi za mauzo na nyingine bila kusahau msamiati wa ‘kubaniwa, hivi sasa ni wafanyabiashara. Yes, ni businessmen!

Ni fahari kubwa kuwa na wanamuziki kwenye wenye kuwaza nje ya MIC. Wanaoyaona maisha upande ambao, haushirikishi booth (chumba cha kuingizia sauti). Wenye akili kuwa maisha hayajengwi kwa midundo na lyrics peke yake, bali maisha yana zawadi nyingi kwa kila mitikasi halali.

TUANZIE KWA JK

Desemba 19, mwaka jana, Rais wa Nne JMT, Jakaya Kikwete alitwiti: “Kuna siku nilimsihi MwanaFA na wanamuziki wengine kufanya shughuli nyingine zaidi ya muziki pekee. Nimefarijika leo kunitembelea na kutambulisha bidhaa yake mpya ya body spray. Hii ni hatua kubwa na nzuri kwa vijana wetu. Tuwaungishe!”

Katika twiti hiyo ya JK, aliambatanisha na picha akiwa na FA, wameshikilia body spray za FYN by Falsafa. Hiyo product ya body spray kutoka kwa FA tutajaji kunako mwisho wa reli. Kwa sasa twende hivi;

Machi mwaka jana, mhariri mwandamizi wa jarida la Forbes, Zack Greenburg, alichapisha kitabu chenye jina “3 Kings: Diddy, Dr Dre, Jay-Z and Hip Hop’s Multibillion-Dollar Rise”. Yaani Wafalme Watatu: Diddy, Dre, Jay-Z na Kukua kwa Mabilioni ya Dola kwenye Hip Hop.

Ndani ya kitabu hicho, Greenburg anawaelezea Diddy, Dre na Jay-Z kuwa sio kwamba ni matajiri zaidi kwenye Hip Hop, bali utajiri wao ni mkubwa kuliko mwanamuziki wa aina yoyote.

Hiyo inamaanisha nini? Ni kwamba angalau Jay-Z hufuruka kwenye mauzo, lakini Diddy na Dre hawapo kwenye orodha ya wanamuziki ambao wameshafanya mauzo makubwa kupitia muziki wao, lakini ndiyo matajiri wakubwa.

Kama utajiri ungekuwa ni mauzo peke yake, Dre, Jay-Z na Diddy wasingefika popote mbele ya Eminem, ambaye rekodi zinaonesha ndiye rapa aliyeuza zaidi, akifikisha nakala 220 milioni. Hata hivyo, utajiri wake unakisiwa kuwa dola 210 milioni, yaani Sh483 bilioni.

Rihanna, Madonna na Elton John ni wanamuziki walio hai wenye kufuru ya mauzo. Madonna ameshauza nakala 300 milioni, utajiri wake ni dola 590 milioni, sawa na Sh1.4 trilioni. Elton John nakala 300 milioni, utajiri wake ni dola 500 milioni, ambazo ni Sh1.1 trilioni. Rihanna mauzo ni nakala 250 milioni, utajiri ni dola 245 milioni, kwa madafu ni Sh564 bilioni.

Katika chati za mauzo ya muziki, Kanye West anatajwa kuwa juu ya Jay-Z. Akitajwa kuuza nakala 132 milioni, lakini utajiri wake ni dola 160 milioni, sawa na Sh368 bilioni. Jay-Z mauzo yake ni nakala 100 milioni. Ukigusa utajiri wa Jay-Z unatisha! Ni dola 930 bilioni, sawa na Sh2.1 trilioni.

Mmarekani Dan Western, anayemiliki mtandao wa Wealthy Gorilla, ametoa takwimu za Januari 2019 kuwa Diddy ana utajiri wa dola 855 milioni, sawa na Sh2 trilioni, wakati Dre ukibopa wake umesimama kwenye dola 820 milioni, ambazo ni Sh1.9 trilioni.

Ukitazama orodha ya wanamuziki walio hai ambao wameshafanya mauzo makubwa, wamo pia Celine Dione, Mariah Carey, Tylor Swift, Garth Brooks, Billy Joel, Phil Collins, Frank Sinatra na wengine, lakini kwa mkwanja bado hawatii maguu kwa hao wafalme watatu.

SABABU NI NINI?

Jibu ni neno la JK, wanamuziki wafanye kazi zaidi ya muziki. Tajiri namba 3 duniani, Warren Buffett husema: “Usiweke mayai yote kwenye kapu moja.”

Ukitegemea muziki peke yake, kipato chako kitategemea muziki tu. Na soko likiwa bovu, unajikuta hohehahe! Rapa MC Hammer, alikuwa tajiri sana miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990. Soko la muziki lilipomkunjia ndita, Hammer alifilisika. Aliuza jumba lake la kifahari, magari, helikopta, na wapambe walimkimbia.

Muziki ni biashara ya nyota, kuna wakati hung’aa, pia hufifia. Muziki ni bahari, kuna kupwa na kujaa. Ukiwa na vyanzo vingine vya mapato, inakuwa rahisi kupiga hatua kubwa kimaisha, lakini pia ni ulinzi wako.

Wafalme watatu waliamua kuwa businessmen kuliko kubaki wanamuziki. Waliwekeza kwenye biashara tofauti na matokeo yake wanapaa kimaisha, vilevile maisha yao ya kifedha ni salama. Akianguka sehemu moja, biashara nyingine zipo kumlinda.

Mwaka 2006, Dre hakuwa mmoja wa marapa watano matajiri. Akaunganisha nguvu na prodyuza mwenzake, Jimmy Iovine, wakaanzisha kampuni ya Beats Electronics LLC ‘Beats by Dre’, ya uzalishaji wa vifaa vya sauti kama spika, earphones, headphones.

Wazo lilitokana na kuona wanaibiwa muziki wao na wezi waliharibu muziki. Dre alilalamika kuwa wanamuibia muziki na wanamharibia na muziki ambao ameufanyia kazi. Beats by Dre zikaanzishwa ili kulinda ubora wa muziki.

Baada ya hapo, Beats by Dre zikageuka biashara kubwa. Kampuni ya simu ya HTC iliingiza fedha kabla ya kuuza hisa zake. Mwaka 2014, kampuni ya Apple, iliinunua Beats by Dre kwa dola 3 bilioni, sawa na Sh6.9 trilioni. Utaona kuwa utajiri wa haraka wa Dre umesababishwa na Beats by Dre.

Diddy tangu kitambo ana mitikasi mingi. Anamiliki wa mtandao wa kebo televisheni wa Revolt. Kampuni yake ya mavazi ya Sean John inamlipa vizuri.

Ana hisa zake kwenye kamapuni ya Diageo’s Ciroc, inayozalisha pombe kali ya Ciroc, pia ni mwanahisa wa kampuni ya pombe ya DeLeon tequila. Zaidi anamiliki kampuni ya maji ya AQUAhydrate.

Jay-Z anamiliki klabu za usiku. Wabongo wanaotumia Uber, basi wajue Jay-Z ana mpunga wake ndani. Kampuni ya JetSmarter Inc, huitwa Uber ya ndege, yaani ukitaka private jet, fasta unapata. Jay-Z kawekeza mzigo hapo.

Kampuni ya vipodozi ya Julep, ndani yake kuna hisa za Jay-Z. Ongezea kampuni za muziki kama Tidal ambayo ni ya kustrim muziki mtandaoni. Hapo hatujagusa Roc-A-Fella records na Roc Nation.

NYOTA NI NJEMA

Ali Kiba ni mwanahisa wa kinywaji cha MoFaya energy. AY anamiliki kampuni ya uandaaji wa vipindi vya redio na televisheni. Kipindi chake maarufu ni Mkasi kilichokuwa kikitangazwa na mtangazaji Salama Jabir. Hivi karibuni alitangaza kuja na kampuni ya usafirishaji.

FA tayari ametambulisha body spray za FYN by Falsafa. Diamond ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Wasafi Media yenye Wasafi TV na Wasafi Radio FM. Vilevile ana hisa kwenye Diamond Karanga na kadhalika.

Forefathers wa Bongo Fleva, Sugu na Prof Jay, wao ni wabunge, lakini pia wamejitanua kibiashara. Sugu anamiliki hoteli ya nyota tatu Mbeya, inayoita Desderia.

Profesa Jay yeye anayo shule yake ya LJay Busy Bee pale Mbezi Beach, Dar es Salaam. Sasa, usiwaite wanamuziki, waite businessmen.

ADVERTISEMENT