In Summary
  • Akizungumza na Mwanaspoti, Makakala alisema wanawakaribisha wageni kwa wingi kuja kushiriki na kushangilia kwa kuwa michezo ni afya, hujenga urafiki na kuimarisha uhusiano na kwamba watapata fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini.


KAMISHNA Jenerali wa Idara ya Uhamiaji nchini (CGI) Anna Makakala amewataka wageni wanaotarajia kuingia nchini kwaajili ya kushuhudia mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (Afcon U17) kufuata taratibu huku akisisitiza wale wanaotarajia kupitia njia za panya kuingia nchini imekula kwao.

Makakala ameweka wazi kuwa wamejipanga kudhibiti njia zote za mipaka ya nchi ambazo hutumiwa na wageni kuingia hasa wale wanaoingia bila kufuata taratibu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Makakala alisema wanawakaribisha wageni kwa wingi kuja kushiriki na kushangilia kwa kuwa michezo ni afya, hujenga urafiki na kuimarisha uhusiano na kwamba watapata fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

“Wageni wafuate taratibu za kuingia na wale wanaofikiri kupitia mashindano haya kutakuwa na upenyo wa kupita sehemu zisizostahili hasa wahamiaji haramu, hawana nafasi kabisa, tumejipanga kila idara kuthibiti hilo.

“Tanzania imepata nafasi ya kuandaa mashindano makubwa sana na ina vivutio vingi kama mbuga za wanyama na Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine, hivyo mbali na mashindano watakuwa na fursa nyingine ya kushuhudia vivutio hivyo,” alisema

Alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia Serengeti Boys kwenye michuano hiyo itakayoanza Jumapili hii.

Alisema jukumu lao ni kuwakaribisha wageni.

ADVERTISEMENT