In Summary

Timu Nne za Young Warriors, Ambassador FC,Utumishi Meatu na Bariadi United zinashiriki Hatua hiyo ambayo ndio itakayompata Bingwa wa mkoa huo msimu huu.

LIGI Daraja la Tatu mkoa wa Simiyu Hatua ya Nne Bora imeanza juzi kwa mabingwa watetezi wa mashindano hayo Ambassador FC kulazimishwa Suluhu na Bariadi United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi.

Timu Nne za Young Warriors, Ambassador FC,Utumishi Meatu na Bariadi United zinashiriki hatua hiyo ambayo ndio itakayompata bingwa wa mkoa huo msimu huu.

Hatua hiyo ya nne bora inachezwa kwa mtindo wa ligi ambapo timu yenye pointi nyingi kuliko wenzake ndio atakuwa bingwa wa mkoa huo.

Mchezo huo ulikuwa na mgumu kutokana na timu hizo mbili kila wanapokutana lazima pachimbike kutokana na upinzani wa timu hizo mbili mkoani hapa.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Simiyu (SIFA), Kulwa Mtebe alivitaka vilabu vinavyoshiriki Ligi hiyo kuhakikisha vinafuata kanuni za mashindano hayo ili kumaliza salama hatua hiyo.

Alisema wao  kama viongozi wanataka kuona wanampata bingwa wa kweli ambaye atawakilisha vyema mkoa huo kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa.

“Hii hatua ni ngumu sana hivyo tunataka kila timu izingatie Kanuni za Ligi ambazo ndio zinazotuongoza tukizifuata hizi hakuna malalamiko yatakayoweza kujitokeza,” alisema Mtebe.

 

ADVERTISEMENT