In Summary
  • Kwa kifupi ni kwamba Tanzania imevuna kile ilichopanda, lakini ukweli wa mambo mfumo wa soka letu hasa kwa vijana ndio uliotuangusha.

MASHABIKI wa soka bado wanaendelea kusononeka kushindwa kufanya vizuri kwa Serengeti Boys katika Fainali za Afcon U17 wakiwa kama wenyeji.

Tanzania imeondolewa mapema tena kwa aibu katika michuano hiyo, kitu ambacho hakuna mdau wa soka aliyekuwa akitarajia hasa ikizingatiwa kuwa, wadau walikuwa na matumaini makubwa na vijana hao.

Yapo mambo mengi yamekuwa yakitajwa kuiangusha timu hiyo kwenye fainali hizo, hata juzi bungeni Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe naye alieleza yake juu ya kuchemsha kwa Serengeti akidai ahadi za mawakala wa kimataifa zilichangia.

Huko mitaani nako wadau wanaamini ahadi ya magari na Sh 20 milioni walizoahidiwa watoto hao kabla ya kuanza kwa fainali hizo ni sababu iliyowachanganya mapema na kujikuta wakifungwa mechi zote tatu.

Kwa kifupi ni kwamba Tanzania imevuna kile ilichopanda, lakini ukweli wa mambo mfumo wa soka letu hasa kwa vijana ndio uliotuangusha.

Tanzania na sifa zote za kuwa na ligi ya kiwango cha juu na nchi inayokimbiliwa na nyota mbalimbali wa kigeni kutoka nje ya nchi, tunaangushwa na kushindwa kuwekeza kwenye soka la vijana ndio maana tumekuwa hatuna timu imara za taifa kuanzia zile za vijana.

Hata kama kumekuwa na michuano kadhaa ya vijana, lakini mfumo wa kuwatunza wachezaji wanaoibuliwa kwenye michuano hiyo ni tatizo linalokwamisha kama nchi kusonga mbele.

Ukifuatilia nchi zilizokuja kushiriki fainali hizo wakiwamo majirani zetu wa Uganda tu, asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hizo za U17 wametokea kwenye akademi ama klabu za Ligi Kuu kwa upande wa timu za vijana tofauti Tanzania.

Kama klabu hazina mfumo wa kuwa na timu za vijana, tutapataje timu imara za taifa? Kama klabu zingekuwa na mfumo waliokuwa wakiutumia zamani wa kuwa na timu za watoto, vijana na zile za wakubwa sio taifa tu lingenufaika, bali hata klabu zenyewe zingeepukana na kubeba mzigo wa gharama kila kipindi cha usajili.

Kwa wanaokumbuka miaka ya 1970, Simba, Yanga na hata klabu nyingine zilikuwa na mfumo wa kuwa na timu za aina hiyo, Yanga Kids, Simba Kids, Yanga na Simba B kisha zile kubwa ambapo vipaji mbalimbali viliibuliwa na kuja kuwa tegemeo.

Tangu klabu zilipoachana na mfumo huo, soka la Tanzania limekuwa likiyumba, likikosa muelekeo na ndio matokeo ya timu zetu za vijana kuchemsha, ikiwamo Serengeti Boys mbele ya washindani wao wa Afcon U17-2019.

Ukiangalia kikosi cha Nigeria, Angola, Cameroon, Morocco, Guinea, Segenal na hata Uganda wote walionekana kuwa wamekamilika kuliko Serengeti, hata kama timu hii ya vijana imetwaa taji la Cecafa U17 na katika michuano ya nchi za Kusini mwa Afrika. Michuano hiyo haikuwa kipimo kizuri cha kuitathmini Serengeti. Kwa sababu kwenye Afcon U17 Cecafa Zone, haikufurukuta mbele ya Ethiopia na Uganda zilizoingia fainali na Uganda kubebea taji kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Hii ilikuwa inatoa picha kwamba, licha ya kuwa wenyeji, bado timu yetu haikuwa na maandalizi mazuri na wala sio ishu za wachezaji kuvurugwa na ofa za akina El Hadji Diouf na wenzake juu ya kuwapeleka nyota wa Serengeti Ulaya. Tatizo ni kwamba hatuna mfumo sahihi wa kuwajenga wachezaji wetu tangu ngazi za chini na kuwaandaa vyema kwa michuano mikubwa kama hiyo ya Afcon U17.

Mwaka juzi Tanzania ilionekana kuwa imara zaidi katika michuano ya Afcon U17-2017 kule Gabon kwa sababu TFF ya Jamal Malinzi ilishikia bango timu hiyo na kufanya maandalizi kamambe ikiwamo timu kupelekwa kambini nje ya nchi sambamba na kushiriki michuano mikubwa iliyowajenga wachezaji, ambao wengi wao walikuwa wakitoka kwenye timu za vijana za klabu za Ligi Kuu.

Kwa sasa ni klabu chache zenye utamaduni wa kutengeneza vijana kuanzia chini, ukiondoa Mtibwa Sugar ambao kwa miaka yote tangu ipande Ligi Kuu katikati ya 1990, Azam na kidogo Simba, JKT Tanzania, klabu nyingine zimekuwa zikimiliki timu za vijana za kuungaunga.

Ni vyema kutumia matokeo ya Serengeti Boys kama darasa kwa klabu na wasimamizi wa soka la Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji mkubwa katika soka la vijana ili tuje kunufaika na vipaji vilivyopo, lakini pia kusaidia kuwa na timu imara za kutuwakilisha.

ADVERTISEMENT