In Summary

Nakimbia sana eeh! Ni hivi, baada ya Tupac kutajwa kuwa amechaguliwa kutunukiwa Rock & Roll Hall of Fame Class of 2017, wapondaji walianzisha michongo yao. Walisema Tupac hakustahili, kwani LL alikuwa supastaa wa Rap kabla yake.

MACHI 29, mwaka huu, kiwanja ni Barclays Center, Brooklyn, New York, ndipo itafanyika shughuli ya tuzo za Rock & Roll Hall of Fame 2019. Bila shaka nasi wa dunia ya tatu tutaona kwa televisheni, maana lebo kama chaneli za HBO na SiriusXM, zimepewa haki ya matangazo kwa kulipia, yaani Pay Per View (PPV).
Usijidanganye aisee, lengo langu si kulipigia debe tukio hilo. Twende sawa, utaelewa ukionesha ustaarabu. Tuanze hivi; Desemba 13, mwaka jana, siyo mbali sana, ni mwezi uliopita tu.
Ndipo majina ya watakaotunukiwa Rock & Roll Hall of Fame mwaka huu yalitangazwa.
Bi mkubwa Janet Jackson baada ya kupendekezwa mara nyingi na kura kutotosha, safari hii amechaguliwa. Ataenziwa kwa tuzo ya Rock & Roll Hall of Fame mwaka huu. Bendi za Rock, Def Leppard, Roxy Music, The Cure, The Zombie na Radiohead, vilevile mamkubwa wa Rock, Stevie Nicks, kwa pamoja watatunukiwa Rock & Roll Hall of Fame 2019.
Hapa sasa tumefika kwenye jawabu. Linatokana na wapendekezwa ambao kura zao hazikutosha, kwa hiyo hawatatunukiwa Rock & Roll Hall of Fame mwaka huu.
Waliokosa ni bendi za Rock, Rage Against the Machine, Devo na MC5, bendi ya Pop ya Ujerumani, Kraftwerk, bendi ya Funk, Rufus & Chaka Khan, mbabe wa instruments, Todd Rundgren, babu John Prine na rapa LL Cool J.
Ooh, jibu ni LL Cool J. Unajua kwa nini jibu ni LL? Jawabu ni Tupac Shakur. Vipi nakuchanganya eeh? Unaona nyotanyota siyo? Usikonde, majibu yote utapata, unachotakiwa ni kuonesha ustaarabu.
Ngoja nisikuchoshe; Desemba 2016, majibu ya watunukiwa wa Rock & Roll Hall of Fame 2017 yalitoka. Fundi wa Folk Rock, Joan Baez, bendi za Rock, Electric Light Orchestra, Journey, Yes na Pearl Jam, vilevile rapa Tupac Shakur walishinda.
Unadhani hivyo tu ndiyo jibu limetosha? Bado! Aprili 9, 2017, ilikuwa ni kilele cha tuzo za Rock & Roll Hall of Fame 2017. Tupac hayupo duniani tangu Septemba 13, 1996. Hivyo, swali lilikuwa ni akina nani wangepanda jukwaani kumuenzi Tupac?
NAJIFANYA USAIN BOLT?
Nakimbia sana eeh! Ni hivi, baada ya Tupac kutajwa kuwa amechaguliwa kutunukiwa Rock & Roll Hall of Fame Class of 2017, wapondaji walianzisha michongo yao. Walisema Tupac hakustahili, kwani LL alikuwa supastaa wa Rap kabla yake.
Sifa za kustahili kutunukiwa Rock & Roll Hall of Fame zipo katika makundi mawili. Mosi, ni umri. Kwamba msanii ili awanie tuzo, inabidi wimbo wake wa kwanza uwe umefikisha au kuzidi umri wa miaka 25 katika mwaka anaopendekezwa. Pili, ni nguvu ya muziki wake, upekee wa kazi zake na ushawishi wa kijamii anaokuwa nao mwanamuziki husika.
Kuhusu umri ni kweli, LL ni supastaa tangu mwaka 1985. Albamu yake ya kwanza, Radio, ilitoka mwaka huo ikiwa na ngoma kali kama I Can't Live Without My Radio, Rock the Bells na kadhalika, iligonga platinum, yaani iliuza nakala zaidi ya milioni moja. Wakati huo LL alikuwa bwa'mdogo wa umri wa miaka 17 tu.
Novemba 1991, Tupac 'Makaveli' aliachia albamu yake ya kwanza, 2Pacalypse Now, ikiwa na dude la kwanza, Trapped kisha Brenda's Got a Baby. Kabla ya balaa lake kama solo, alichana ndani ya ngoma, Same Song ya Digital Underground ambayo ni kruu ya zamani ya Pac. Mpaka hapo unakubali kuwa LL kamtangulia sana Tupac.
Ukipiga hesabu ya kigezo cha umri, ni kwamba singo ya kwanza ya LL ilifikisha umri wa miaka 25 mwaka 2010, kwa hiyo tangu mwaka 2011, LL alikuwa na sifa za kuteuliwa kuwania tuzo ya Rock & Roll Hall of Fame ambayo iliasisiwa mwaka 1983 na Ahmet Ertegun, ambaye alikuwa bosi wa lebo ya Atlantic Records.
Kikokotoo cha 2Pacalypse Now kinaleta majibu kuwa wimbo wa kwanza wa Tupac, ulifikisha umri wa miaka 25 mwaka 2016. Mwaka huohuo aliteuliwa kuwania Rock & Roll Hall of Fame 2017. Desemba 2016, alitangazwa kuwa mmoja wa washindi na Aprili 2017 alitunukiwa.
Kwa nyongeza ni kwamba Agosti 2016, wakati orodha ya wawania Rock & Roll Hall of Fame 2017 inatangazwa, wimbo wa kwanza wa Tupac ulikuwa haujafikisha umri wa miaka 25.
Sema watu walijua kwa vile tuzo zingetoka 2017, basi kigezo cha umri kingekuwa kimeshatimizwa. Na kweli, Desemba 2017 wakati majina ya washindi yalipotangazwa, umri ulikuwa umeshatimia.
Ndipo hapo wana walianza kuteseka, kwamba LL alipaswa kutangulia. Tuzo za mwaka 2018 na 2019, zote LL kura hazijatosha. Wakati Tupac mara moja tu, akapigiwa kura za kishindo na kuchukua tuzo. Ni kwamba ukimchukia Tupac anapoitwa King wa Hip Hop utateseka bure, maana jamaa ana kila kitu, tungo kali, mashairi konzi, floo yenye mamlaka, mbabe wa mauzo sokoni na anapendwa na mamilioni ya watu duniani kote.
Ni hivi, kwa umri LL katangulia, lakini kigezo cha pili kuhusu ubora kazi na ushawishi kwa jamii, Tupac anampiga bonge la mweleka LL. Ongeza kuwa Tupac ndiye rapa wa kwanza kushinda Rock & Roll Hall of Fame kama solo. Kundi la N.W.A la akina Ice Cube, Dre, Eazy E na kadhalika lilishinda mwaka 2016, wakati marapa wa Grandmaster Flash and the Furious walitunukiwa mwaka 2007.
Kama ambavyo Tupac alivyokuwa mwana Hip Hop wa kwanza kushika namba moja kwenye chati za muziki Marekani na Ulaya, akawa wa kwanza kuuza platinum mara tano akiwa jela kupitia albamu ya Me Against the World, akawafunga tela kwa kufikisha mauzo ya nakala zaidi ya milioni 75, ndivyo na kwenye Rock & Roll Hall of Fame alivyowatangulia.
USIKU UKAWA MTAMU
Turudi kuleee; swali lilikuwa ni akina nani wangepanda jukwaani kumuenzi Tupac? Lilikuwa bonge la tukio.
Snoop Dogg alipanda jukwaani na kutoa hotuba baabkubwa iliyotoa watu machozi. Tupac alikuwa binadamu, aliyefanya Hip Hop kwa kiwango ambacho hakuna aliyefanya kabla yake. Hayo ni maneno ya Snoop.
Snoop ni gangster, lakini kuna wakati sauti ilikwama. Snoop na Tupac walikuwa washkaji sana. Stori ya 2Pac ilimchoma Snoop ingawa ni yeye aliisimulia. Alizungumza kwa upole, watu walilia. Kisha Snoop akapokea tuzo ya Rock & Roll Hall of Fame kwa niaba ya Tupac.
Alipoondoka Snoop, akaja Alicia Keys na piano yake, akaimba chorus za nyimbo za Pac kama Dear Mama, Ain't Mad at Cha, Changes, Ambitions as a Ridah na I Got Around, huku akielezea alivyompenda Tupac na kutamani kama angekutana naye. Alicia ni wa East Coast kwa akina Notorious BIG, Jay Z, P Diddy, LL na wengine, wakati Tupac alikuwa kinara wa West Coast. Tofauti hiyo haijamzuia Alicia kumpenda.
Ooh, baada ya Alicia walipanda wahuni wa West Coast, rapa YG na Snoop waliimba 2 of Amerikaz Most Wanted wa 2Pac aliomshirikisha Snoop. YG alichana vesi za 2Pac.
Akapanda Treach wa Naughty By Nature, akachana Hail Mary ya 2Pac, kisha T.I akawadatisha wadada na wamama kwa Keep Ya Head Up ya 2Pac. Ilikuwa siku ya Tupac the King. Snoop akasema 2Pac ni Greatest Rapper of all time. Usiteseke!

ADVERTISEMENT