In Summary

Asilimia kubwa viongozi ndiyo wanawasainisha wachezaji mikataba yao baada ya kujiridhisha na kuangalia mahitaji waliyoelekezwa na makocha wao ambao wengi wapo likizo.

Timu ya Taifa Stars, iliondolewa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika ‘Afcon’ huko Misri baada ya kufungwa mechi zote tatu za kundi lao.

Stars ilipangwa kundi moja na Algeria, Senegal na Kenya imeondolewa bila kuwa hata na pointi moja. Wanarudi nyumbani kuendelea na ratiba zao zingine ikiwemo kujiandaa na CHAN inayishirikisha wachezaji wanaocheza ligi ya ndani.

Sasa wakati Stars inarudi nyumbani kuendelea na ratiba nyingine, klabu nazo zinaendelea kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi kuu Bara.

Usajili unaendelea sasa kwa timu za Ligi Kuu pamoja na zile za madaraja ya chini, Ligi Daraja la Kwanza pamoja na daraja la pili.

Kila klabu inasisitiza inafanya usajili wake kulingana na ripoti ya makocha wao, hivyo hakuna kitakachoharibika.

Msimu ujao tutashuhudia klabu nyingi zikiwa na vikosi vyenye wachezaji wapya ambao wametoka timu nyingine, wakiwemo wageni na wazawa.

Asilimia kubwa viongozi ndiyo wanawasainisha wachezaji mikataba yao baada ya kujiridhisha na kuangalia mahitaji waliyoelekezwa na makocha wao ambao wengi wapo likizo.

Hii ikiwa na maana makocha watakaporejea watakuta viongozi wamemaliza kufanya usajili kama waliwavyoelekeza kwenye ripoti zao.

Sidhani kama kutakuwepo na kocha ambaye atalalamika kuwa amesajiliwa wachezaji asiowataka, hatutarajii kabisa hilo kulisikia.

Klabu kama Simba ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi kuu, Yanga, Azam, Namungo, KMC na nyinginezo zinafanya usajili kwa kasi ya ajabu kulingana na ratiba jinsi ilivyo kwani ligi inapaswa kuanza mwezi ujao hivyo hakuna muda wa kupoteza.

Klabu nne za ligi kuu zipo kwenye maandalizi ya michuano ya Caf na Simba na Yanga wanashiriki Ligi ys Mabigwa wakati Azam na KMC wao wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika hivyo kasi ya usajili lazima iwe kubwa kwani wanahitaji kuingia kambini mapema.

Azam na KMC ambao wanashiriki Kombe la Kagame wao walianza maandalizi yao huku wakiendelea na usajili kuimarisha kikosi chao na wameonekana kufanikiwa kwa hilo tofauti na Simba na Yanga ambao wanaonekana bado wanahitaji kuendelea kusajili.

Usajili wa klabu hizi kongwe unafikirisha kwa baadhi ya wachezaji wao lakini yote kwa yote ni kuanza kwa ligi ili kuona nani amefanya usajili kwa mujibu wa mahotaji ya makocha wao.

Wachezaji wapya wanapaswa kututhibitishia ubora wao kwenye ligi ya nyumbani ili kufuta dhana iliyoopo kichwani kwasasa hasa wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na hizi timu mbili Simba na Yanga.

Kilicho bora kitajidhihirisha chenyewe uwanjani hata kwa mechi moja tu, hakutakuwepo na sababu ya kuitoa kama watashindwa kufikia malengo, sababu za viwanja vibovu sio sababu ya msingi kwa mchezaji kushindwa kuonyesha kile alichonacho.

Kuna uwezekano mkubwa kabisa msimu utakapoanza na endepo waliosajiliwa wakashindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa basi viongozi hawa hawa ndio watawalalamikia wachezaji na makocha wao.

Vile vile kuna makocha hata kama hawatakuwa na ujasiri wa kutamka wazi lakini nao watawalalamikia viongozi wao kuwa waliosajiliwa si waliowahitaji.

Lakini kwa vile makocha ndio wenye kubeba lawama zote basi watapaswa kukubaliana na mazingira watakayokutana nayo huko mbele.

Usajili unaendelea, maandalizi yanaanza na michuano itaanza hivyo kuna watakaolia na watakocheka.

ADVERTISEMENT