In Summary
  • Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa itakayoanza Novemba 27-28 mwaka huu, hivyo inajipanga kwa kusajili nyota watakaoisaidia timu hiyo kufanya vizuri zaidi.

KITITA cha fedha ambacho kipo kwenye akaunti ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba kinasubiri tu dirisha dogo la usajili lifunguliwe ili kutumika kunasa mastaa wa maana wanaotikisa kwenye soka la Afrika. Mastaa wengi ni wale wanaocheza klabu zinazotamba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo fungu hilo limezidi kuwapa jeuri ya kuvuta nyota wa maana.

Wakati wengi wakiamini kuwa kikosi ambacho Simba inacho kinaifanya isiwe na haja ya kutumia fungu kubwa la fedha, timu hiyo kwa sasa imetumia zaidi ya Sh 375 katika usajili wake wa dirisha kubwa iliponasa wachezaji nane, na imebakiwa na zaidi ya Sh 320 milioni.

Simba ambayo kwa mujibu wa bajeti iliyosomwa kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo Jumapili iliyopita, imetenga Sh 750 milioni kwa ajili ya usajili, ilitumia kiasi cha Sh 375 tu kwenye dirisha kubwa kuwanasa Pascal Wawa, Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Meddie Kagere, Adam Salamba, Hassan Dilunga, Cletous Chama, Deogratias Munishi ‘Dida’.

Pamoja na kutumia mkwanja huo, bado Simba imebakiwa na pesa ndefu kufanya matanuzi mengine ambazo wanaweza kukitumia katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Ikiwa na fungu la Sh 375 milioni mkononi ambalo linaweza kutumika katika usajili wake, fedha hizo zinatosha kusajili mojawapo kati ya majina ya mastraika watano tishio wanaokidhi vigezo vilivyowekwa na kocha Patrick Aussems katika usajili aliopanga kuufanya kwenye dirisha dogo.

Hivi karibuni kocha huyo raia wa Ubelgiji aliliambia Mwanaspoti kuwa, amepanga kunasa mchezaji mmoja tu katika usajili wa dirisha dogo ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji.

Kutokana na kasi ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu nchini ambayo washambuliaji alionao wanayo, straika anayehitajika na Aussems kwenye dirisha dogo ni yule, ambaye ana ubora na uwezo wa hali ya juu ambao utaifanya Simba ifanye vizuri kimataifa.

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, imebaini nyota watano wenye ubora na uwezo wa hali ya juu katika safu ya ushambuliaji ambao kwa fungu ambalo Simba inalo katika akaunti yake, inaweza kumnasa mmojawapo na akaifanya vyema shughuli atakayopewa na Mbelgiji huyo.

Straika wa kwanza tishio, ambaye Simba ikimsajili katika dirisha dogo anaweza kuwapa jeuri ya kutamba kimataifa ni nyota wa AS Vita ya DR Congo, Jean-Marc Makusu Mundele.

Nyota huyo, ambaye ana thamani ya Pauni 150,000 (Sh 452 milioni) ameifungia AS Vita mabao 14 katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu huu.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambako AS Vita ilitolewa kwenye raundi ya kwanza, alifunga mabao manne na yumo kwenye chati ya vinara wa ufungaji licha ya timu yake kutolewa mapema, lakini balaa lake akalihamishia kwenye Kombe la Shirikisho alikofunga mabao 10 hadi sasa huku akiwa ameiongoza klabu hiyo ya DRC kufika hatua ya fainali.

Hata hivyo, Simba inapaswa kuongeza angalau kiasi cha Sh 77 milioni ili kumnasa mshambuliaji huyo, ambaye pia idadi kubwa ya klabu za soka nje na ndani ya Afrika zinamnyemelea.

Straika wa pili, ambaye kwa fungu la Sh 375 milioni anaweza kunaswa kirahisi na Simba ni Lazarous Kambole, raia wa Zambia anayechezea Zesco United.

Kambole (24), ameifungia Zesco United mabao saba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na thamani yake kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermkt.com ni Pauni 45,000 (Sh 134 milioni ).

Katika kikosi hicho cha Zesco United, mbali na Kambole, kuna straika raia wa Ghana, Zikiru Adams ambaye ameifungia timu hiyo ya Zambia mabao manne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo ya Zambia imeishia hatua ya makundi ikishika nafasi ya tatu.

Adams kama ilivyo kwa Kambole, naye ana miaka 24 na thamani yake ni pauni 30,000 ambazo ni sawa na Sh 90 milioni.

Rekodi na thamani ya mshambuliaji wa Cara Brazzaville ya Congo, Cabwey Kivutuka (20) kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu nayo vinaweza kuishawishi Simba kutumia noti kumnasa ili kuongeza mtu mwenye shughuli ya kibabe kwa mabeki wa timu pinzani.

Straika huyo mwenye thamani ya Dola 80,000 (Sh 183 milioni), amefunga mabao manne kwenye Kombe la Shirikisho tena dhidi ya timu ngumu na tishio za Enyimba, Williamsville na Raja Casablanca.

Nyota wa mwisho ambaye Simba inaweza kumnasa pasipo kutoka jasho kwa fungu lake ni ni Mnyarwanda Tuyisenge Jacquise anayechezea Gor Mahia ya Kenya, ambaye kwenye Kombe la Shirikisho amepachika mabao manne.

Mshambuliaji huyo alijenga safu tishio ya ushambuliaji ya Gor Mahia pindi alipokuwa akicheza sambamba na Meddie Kagere, ambaye kwa sasa yupo Simba hivyo usajili wake ikiwa utafanyika, utamfanya akutane tena na pacha wake.

Mbali na hilo, Tuyisenge ana rekodi nyingine tamu ya kuwaonea Yanga ambao ni watani wa jadi wa Simba, baada ya kuwafunga mara mbili mfululizo pindi timu hizo zilipokutana kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Thamani ya Tuyisenge kwa sasa inakadiriwa kuwa Dola 50,000 (Sh 114 milioni) ambazo ni sehemu tu ya fungu la usajili ambalo lipo mkononi mwa Simba hivi sasa.

MSIKIE MBELGIJI

Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema kilicho mbele yake katika dirisha dogo la usajili ni kuongeza straika mmoja, ambaye atakuwa na uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mabao kwa wenzake.

Aussems amesema usajili huo utalenga sana mashindano ya kimataifa ambayo msimu huu, Simba watacheza Klabu Bingwa Afrika.

Anasema akili yake ni kutafuta mastraika ambao wanafanya vizuri katika timu kubwa Afrika na hilo linawezekana kutokana na bajeti ya Sh 350 milioni iliyobaki katika usajili wa dirisha kubwa.

“Katika dirisha dogo ni ngumu kupata wachezaji wa maana kutokana wengi kuwa na mikataba na timu zao, lakini uwezo wa bejeti yetu inaruhusu kupata hata mshambuliaji mmoja mwenye uwezo huo.

“Nitakutana na Mohammed Dewji ‘MO’ ili kuzungumza na kuona tunafanya usajili wa namna gani ili kuwapata wachezajia ambao, tunashida nao katika timu haswa tukilenga mashindano ya kimataifa.

“Niwapongeze viongozi wa Simba wameonesha kuwa wana kiu ya kupata mafanikio kimataifa kutokana na pesa yao ambayo wameiweka ili kutumika katika usajili,” alisema Aussems ambaye alishaweka wazi kuwa ataandaa orodha ya wachezaji watano mpaka sita ili mmoja kusajiliwa.

“Macho yangu yanaangalia wachezaji ambao wanafanya vizuri kimataifa kwa sasa na tukapoanza kusajili nitawapa orodha ya wachezaji ambao, nawahitaji kamati ya usajili ili kufanya kazi yao na naimani watanifanikishia hilo,” aliongezea Aussems.

ADVERTISEMENT