In Summary

Mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi, utacheza baadaye leo Jumamosi na Simba imetamba kwamba, iko kamili na lazima mtu apasuke.

SASA hawa Waarabu wanatokaje pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam? Ni saa chache tu zimebakia kabla ya Simba kushuka dimbani kusaka ushindi wa kwanza na muhimu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuvaana na JS Saoura ya Algeria.
Mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi, utacheza baadaye leo Jumamosi na Simba imetamba kwamba, iko kamili na lazima mtu apasuke.
Simba ambayo ina historia yake kwenye soka la Afrika, inataka kutimiza ndoto ya kuifanya kuwa timu ya kwanza kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tangu mfumo wake ulipobadilishwa mwaka 2017.
Ili Simba ijiweke mahali pazuri ni lazima itoke uwanjani na ushindi dhidi ya wapinzani wao hao kwenye kundi D.
Kwenye makaratasi ni mchezo unaoonekana kuwa mgumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania, lakini mikakati ya kiufundi iliyosukwa vyema na kocha Patrick Aussems na benchi lake la ufundi, ikiwa itatekelezwa vyema na kwa ufanisi wa hali ya juu ndani ya uwanja na wachezaji, Mwarabu ana nafasi finyu ya kuondoka na pointi pale Taifa.
Akifahamu fika kuwa mahitaji ya hatua za mwanzo na hii ambayo Simba ipo sasa ni tofauti, Aussems amefanya maboresho ya mbinu zake ili kuhakikisha timu yake inapata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Saoura na sio vinginevyo.
Kama ilivyo kawaida, Simba itaendelea kutumia soka lake la kufunguka na kushambulia kwa muda wote wa dakika 90 za mchezo, lakini Aussems ameongeza mbinu mpya endapo kutakuwa na kikwazo cha kupata mabao.
Mazoezi ya mwisho ya jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa, ambayo yalitoa taswira halisi ya kile ambacho Simba wanakwenda kukifanya kwenye mchezo huo dhidi ya Saoura ambao, utachezeshwa na mwamuzi Joshua Bondo kutoka Botswana.
Ni wazi Simba wataanza kwa kujaribu kupenya kupitia katikati kwa mbinu yao ya kupiga pasi fupi fupi kuelekea langoni mwa Saoura, lakini iwapo mbinu hizo zitashindwa huenda wakajenga mashambulizi kupitia pembezoni mwa uwanja wakiwatumia viungo/mawinga au mabeki wa pembeni.
Staili hiyo ya kushambulia inajengwa kwa pasi chini ya sita zinazoanzishwa eneo la katikati mwa uwanja ambako viungo wa Simba kisha kupiga ndefu pembeni kwa winga au beki wa kulia au kushoto, ambaye naye atapiga krosi kwa washambuliaji wa kati ambao watakuwa tayari wameingia langoni mwa wapinzani.
Iwapo mabeki wa Saoura wataonyesha umahiri wa kuondosha krosi za juu ambazo zitakuwa zinaelekezwa langoni mwao, Simba watalazimika kupiga krosi za chinichini kwa mtindo wa kuzitoa nje ya eneo la hatari ili ziwakute nyota walio nje ya boksi la adui ambao watakuwa na nafasi nzuri ya kupiga mashuti yanayoweza kuzaa bao kama alivyofanya Jonas Mkude alipofunga bao la kusawazisha dhidi ya Nkana Red Devils mwezi uliopita.
Simba wanaingia kwenye mechi ya leo wakitambia uimara wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imefunga bao katika mechi zote za Ligi ya Mabingwa ilizocheza msimu huu dhidi ya timu za Mbabane Swallows kwenye hatua ya awali na ule dhidi ya Nkana kwenye raundi ya kwanza.
Hapana shaka jicho na matumaini ya Simba vimeelekezwa kwa kiungo mshambuliaji Cletous Chama, ambaye amekuwa uti wa mgongo wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kutokana na uwezo wake wa kuendesha na kuchezesha timu, kutengeneza nafasi za mabao, kupiga pasi za mwisho na kufumania nyavu.
Katika kulidhihirisha hilo, Chama amehusika katika mabao sita kati ya 12 ambayo Simba imefunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ambapo mwenyewe amepachika mabao manne huku akipiga pasi mbili zilizozaa mabao.
Hofu kubwa kwa Simba ni kwenye safu yake ya ulinzi ambayo kwanza itamkosa beki mzoefu, Erasto Nyoni ambaye ni majeruhi, lakini bado imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakizinufaisha timu pinzani.
Safu hiyo ya ulinzi ya Simba inapaswa kucheza kwa umakini na nidhamu ya hali ya juu dhidi ya Saoura ambao, wamekuwa ni wajanja wa kutumia makosa ya timu pinzani kupata mabao yao.
Ukuta wa Simba utakaoundwa na Juuko Murshid, Aishi Manula, Mohammed Hussein, Paschal Wawa na Nicholas Gyan unapaswa kuwa makini na ujanja wa washambuliaji wa Saoura hasa Mohammed Hammia ambao, umekuwa ukitumika kumhadaa refa na kuisadia timu hiyo kupata penalti za mara kwa mara.
Katika mabao manne ambayo Saoura wameyafunga kwenye mechi nne za mwanzo za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, matatu yametokana na penati ambazo walipewa baada ya ujanja wa Hammia kumhadaa mwamuzi.
Ni mchezo ambao Simba watakutana na mshambuliaji wa Kitanzania, Thomas Ulimwengu ambaye anaweka rekodi ya kukutana na timu za Tanzania mara ya pili kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.
Mara ya kwanza, Ulimwengu alikutana na timu ya Tanzania mwaka 2016 wakati timu yake ya wakati huo, TP Mazembe ilipokutana na Yanga  kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems aliliambia Mwanaspoti kuwa kazi ya kuwamaliza Waarabu hao kwa upande wake inaelekea kumalizika na kilichobaki ni wachezaji wake kuikamilisha.
"Maandalizi yote kwa ajili ya mchezo yameenda vizuri na wachezaji wako tayari. Tutakuwa nyumbani hivyo mpango wetu ni uleue wa kushambulia na ndio maana hata ukiangalia kikosi changu ninachokiandaa kwa mchezo huo kina kundi kubwa la wachezaji ambao kiasili ni washambuliaji.
"Tunafahamu tunakutana na timu kutoka Uarabuni ambao wamekuwa na mbinu ya kujiangusha na kulalamika kwa refa hivyo, jambo la msingi ni sisi kutotazama nini ambacho watakuwa wakikifanya na badala yake kucheza kwa jinsi tulivyojipanga.
“Muhimu ni mashabiki kuja kwa wingi kuipa sapoti timu kama walivyofanya dhidi ya Nkana Red Devils na nawahakikishia kuwa tutacheza soka safi la kushambulia ambalo litawapa burudani tosha na tutahakikisha tunawapa furaha," alisema Aussems.

ADVERTISEMENT