In Summary

Ingawa walikuwa wametengana, John na Helen walikuwa wanaishi kama ‘Paka’ na ‘Panya’, kwa kila mmoja akimwogopa mwenzake

Utangulizi

Mwanamke mrembo anauawa ndani ya bafu, nyumbani kwake, eneo la Tabata, Jijini Dar es Salaam. Kwanza kabisa, muuaji huyo katili alimtumia ujumbe wa vitisho muda mfupi tu kabla ya kutekeleza mauaji hayo. Pia, muuaji huyo alimbaka mrembo huyo kabla ya kumuua. Upelelezi wa Jeshi la Polisi, unafanyika mara moja.

 Msako mkali dhidi ya muuaji huyo unafanyika, na inagundulika siri nzito iliyojificha nyuma ya mapazia kuhusiana na kifo hicho chenye utata. Kama kawaida, mtunzi wako mahiri,  PATRICK J. MASSAWE anatiririka na hadithi hii ya kusisimua.      Fuatilia mpaka mwisho wake…

 

MCHANA  wa saa sita hivi, John Bosho  alikuwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Harrier  la rangi ya fedha, lililokuwa na kiyoyozi kilichompatia hewa nzuri ya ubaridi kiasi cha kulifukuza joto lililokuwa linafukuta huko nje.  Muda huo alikuwa anatafuta eneo la kupaki gari hilo, kwenye maegesho, nje ya Hoteli ya The Kibo II Anex, mtaa wa Kipata, eneo la Gerezani.

Hii ni hoteli iliyopo ndani ya jumba la ghorofa tano, linalopakana kabisa na jengo la ghorofa, linalomilikiwa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika, katika Barabara ya Lumumba, umbali wa mita tano hivi, na pia siyo mbali sana na Viwanja vya Mnazi Mmoja. Baada ya kulipaki gari hilo, John Bosho alishuka na hatimaye kuingia ndani ya hoteli hiyo maarufu yenye hadhi, ambayo alizoea kwenda mara kwa mara kujipatia chakula cha mchana.

Kama kawaida, John Bosho alipoingia, alichagua meza moja ya pembeni na kukaa ili aweze kupatiwa huduma ya chakula. Kabla ya kuagiza chakula, aliangaza macho yake katika pembe zote za humo ndani, ambapo palikuwa na wateja kadhaa waliokuwa wanakula. Akiwa ni mwenyeji pale, aliweza kuhudumiwa chakula alichokipenda, aina ya wali kwa nyama ya ng’ombe.  Aliendelea kula taratibu huku akiangalia jinsi wateja wengine walivyokuwa wanaingia.

Wakati John Bosho akiendelea kula chakula chake taratibu, mara akaingia mwanadada mmoja, kimwana na mrembo wa haja, aliyekuwa anatembea kwa mwendo wa kunata. Moja kwa moja akaenda kukaa kwenye meza iliyokuwa pembeni, jirani yake tu. Mara baada ya kukaa, kimwana huyo aliangaza macho pande zote kuangalia alipo mhudumu, na mhudumu alipomwendea, alimwangiza chakula, wali kwa nyama ya kuku, pamoja na soda moja aina ya Mirinda.

Kimwana huyo alipohudumiwa chakula kile alichokuwa ameagiza, alinyanyuka na kunawa mikono yake katika sinki maalum lilokuwa umbali mfupi kutoka ilipokuwa meza yake. Alipomaliza kunawa, akarudi tena na kendelea kula taratibu, tena kwa mapozi ya hali ya juu, kwani hakuwa na haraka. Wakati wote huo alikuwa akiangalia chakula chake na wala hakuwa na muda wa kuangalia pembeni.

John Bosho aliendelea kumwangalia kimwana huyo kwa muda wote, ikiwa siyo mara yake ya kwanza kumwona akiingia hotelini pale. Ni mara nyingi walikuwa wanakutana, yaani ni kama bahati vile, kwani kila mmojawapo anapoingia, basi hujikuta wote wameingia, tena kwa wakati mmoja kana kwamba walikuwa wameahidiana.

Kwa kiasi fulani, mwanadada huyo mrembo wa nguvu, alikuwa amemwingia akilini John Bosho, kiasi cha kumfanya atamani kummiliki na awe wake. Hivyo akawa anageuza shingo yake mara kwa mara kumwangalia, na halikadhalika kimwana huyo alikuwa akimwangalia yeye, bila shaka akishangaa kwa kukutana kwao. Yeye John Bosho aliendelea kumkazia macho huku  akijaribu kumuundia tabasamu la nguvu, ambalo hata yeye aliliona na kulipokea kwa hisia kali.

Hata hivyo, mara baada ya kulipokea tabasamu hilo, kimwana huyo aliendelea kula chakula hicho, alichokuwa anakula kama vile hataki. Hakika Mwenyezi Mungu alikuwa amemjaalia kimwana huyo sura nzuri ya mviringo, iliyobandikwa macho mazuri, makubwa kiasi, malegevu, ambayo kama ukiyaangalia tu, hujikuta mtu akitoa salamu kwake, hususan mwanaume.

Kifua cha kimwana huyo mantashau, kilikuwa chembamba kilichobeba matiti madogo yaliyosimama wima, miguu yake ilikuwa minene kiasi iliyojaa nyama, na yenye matege ya kupendeza. Na miguu hiyo ikabeba makalio yaliyotuna kwa nyuma na kutikisika kila alipokuwa anatembea bila yeye mwenyewe kujua. Ni mtikisiko uliowaacha wanaume wengi wakiwa hoi kwa kudondosha udenda kwa kumtamani kimapenzi!

Akiwa ni kijana mtanashati, mwenye nguvu za kiuchumi, John Bosho aliamua jambo moja tu. Ni kwenda kumwingia kimwana huyo, ili aweze kumwaga sera zake. Yeye akiwa ni mwanaume wa shoka, asiyeogopa watoto wa kike wa aina ile, akaamua kunyanyuka kutoka katika meza yake. Baada ya kunyanyuka, akaelekea katika meza ile aliyokaa mwanadada huyo, kama vile walikuwa wanafahamiana kwa muda mrefu.

“Hali yako dada…” John Bosho alimsalimia huku akivuta kiti kimoja kilichokuwa upande wa mbele na kukaa huku wakitazamana.

“Nzuri tu,” kimwana huyo alisema huku akimwangalia John Bosho alivyokuwa amekaa kwenye kile kiti kilichokuwa kinatazamana na yeye.

“Samahani dada’ngu, nakaa kidogo bila idhini…” John Bosho akaendelea kumwambia huku akimtolea tabasamu jepesi.

“Kuwa huru, wala usijali…” kimwana huyo akamwambia kwa sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni!

John Bosho akakaa na kubaki akimwangalia!

“Mimi nimekuja hapa kwa lengo moja tu,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Ni kufahamiana na wewe. Tukiwa sote kama  Watanzania tunaoishi katika nchi ya amani, ni muhimu kufahamiana…”

“Unasema kufahamiana?” Kimwana huyo akamuuliza huku akiendelea kumwangalia kwa mshangao!

“Ndiyo. Ni kufahamiana tu, na si vinginevyo…” John Bosho akajibu kwa sauti ya upole huku akiirekebisha tai yake.

“Kwa hivyo umeona ufahamiane na mimi tu? Mbona humu hotelini wanaingia watu wengi tu?” Kimwana huyo akaendelea kumuuliza.

“Nina maana yangu…” John akamwambia.

“Maana ipi?”                           

“Ni historia ndefu…”

“Historia ndefu kivipi?”

“Unajua ni mara nyingi huwa naingia humu hotelini kula chakula mida kama hii,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Lakini kila ninapoingia ni lazima nikuone na wewe unaingia. Nafikiri hata wewe umetambua hilo.”

“Eeh,” kimwana huyo akacheka kidogo na kusema. “Kwa hivyo ni hilo tu?”

“Ndiyo hilo tu. Naona kama nyota zetu zimelingana.”

“Sijui kama zimelingana. Lakini poa, kufahamiana siyo vibaya…” kimwana huyo akasema huku akiendelea kukata nyama ya kuku kwa kisu, kwa mtindo ule wa kujifanya kama alikuwa ameshiba. Na hiyo ilikuwa ni kwa akina dada wengi wanaojiona wazuri!

“Kwa jina naitwa John Bosho. Mimi ni Mtanzania, pia ni mfanyabiashara maarufu hapa Jijini Dar es Salaam, ninayeishi eneo la Ukonga. Bado sijaoa, niko ‘singo.’ Kadi yangu ya kibiashara hii hapa…” John Bosho akamwambia huku akifungua pochi yake iliyokuwa imetuna. Akatoa kadi moja ya kibiashara na kumpa. Ni kadi iliyokuwa na jina la kampuni, anuani, na namba za simu.

“Ahsante sana,” kimwana huyo akasema. Halafu akaipokea ile kadi ya kibiashara na kuitia ndani ya pochi yake iliyokuwa pale juu ya meza upande wa kushoto. Kisha akamwangalia John Bosho kwa nukta kadhaa katika kumsoma. Ni kweli alikuwa ni kijana mtanashati!

 

        ********

JOHN Bosho alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka ipatayo thelathini na sita mpaka arobaini hivi, akiwa ni kijana mwenye elimu ya kidato cha sita, aliyoipata katika Shule ya Sekondari ya Mirambo, Mkoani Tabora. Hata hivyo baada ya kuhitimu na kufaulu vizuri, alitakiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuendelea na masomo zaidi.

Lakini kwa sababu alizozijua mwenyewe, John Bosho hakuendelea na masomo, kwa kile alichokiona kama alikuwa anapoteza muda wa kuanza kuchakarika na maisha. Baadaye alijiunga na vijana wenzake na kujiingiza katika biashara za madini ya aina mbalimbali, dawa za kulevya, na nyinginezo haramu, zisizokubalika na jamii.

Akiwa ni mtu aliyejipanga kisawasawa katika kufanya shughuli zake za haramu bila kujulikana, aliamua kushirikiana na vijana wake maalum anaofanya nao kazi, ambao pia walikuwa wakifuata amri yake bila kupinga.

Vijana hao machachari na wasiokuwa na woga wa aina yoyote,  John Bosho aliwapata katika kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam baada ya kuhangaika sana, kwani kupata watu wa kukubaliana na amri utakayowapa  ni kazi sana. Na katika kujiimarisha katika shughuli zake za haramu, John Bosho aliamua kuwapa mafunzo maalum vijana wake, na kuweza kutumia silaha za moto, kama bunduki na bastola.

Baada ya kuhitimu vizuri katika matumizi ya silaha,  John Bosho aliamua kuwatuma sehemu mbalimbali nchini na kufanya vitendo vya uhalifu, ikiwa ni uporaji kwa wafanyabiashara wakubwa wenye fedha, hasa wanaojihusisha na biashara za madini, huko Mererani, mkaon Manyara, utekeji nyara na nyingine. Baada ya kufanikiwa katika ukamilishaji wa kazi hiyo haramu, vijana hao humkabidhi mali yote yeye, anayepanga utaratibu wa mgawo.

Kazi hiyo John Bosho alifanikiwa kuifanya kwa muda mrefu bila kushtukiwa, akionekana kama mfanyabiashara anayejihusisha na biashara maduka ya vifaa vya ujenzi. Alifanikiwa kufungua duka kubwa la vifaa vya ujenzi, katika mtaa wa Swahili, eneo la Kariakoo.

Ni duka ambalo lilikuwa linauza vifaa vya ujenzi kwa ujumla likiwa limejaa bidhaa za aina mbalimbali zinzohusika na shughuli za ujenzi kwa ujumla, kama vile, saruji, mabati ya aina mbalimbali, nondo na vinginevyo. Yote ile ilikuwa ni kivuli tu, ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi. Duka hilo lilijulikana kwa jina la  J. B. Enteprises Ltd.

Mbali na duka kumiliki duka lile, pia, John Bosho alikuwa anamiliki bohari kubwa la kuhifadhia bidhaa zake, lililoko eneo la Ubungo Machimbo ya Mawe. Ni bohari ambalo alikuwa amelikodi kutoka kwenye kampuni moja ya ujenzi, kwa ajili ya kuhifadhi mizigo yake anayoiagiza kutoka nchi za nje. Ndani ya bohari hilo, palikuwa na ofisi ya kuratibu mipango yake haramu, anapokutana na vijana wake.

Hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuwashtukia, John Bosho na wenzake, kwani walifahamika kama wafanyakazi wake waliokuwa katika mishughuliko ya kikazi. Alijitahidi sana kuratibu mipango yake bila kufahamika na kwa kiasi fulani alifanikiwa sana na kuendelea kujilimbikizia fedha na kufanya anachotaka, hata kujipatia wasichana warembo anaowataka!

 

      ********

JEURI yake ya fedha na kupenda wanawake, John Bosho alifanikiwa kumnasa mwanadada mmoja mrembo, aliyejulikana kwa jina la Helen Fataki, siku za nyuma. Huyo alikuwa ni mwanamke wa shoka na mfanyabisahara maarufu aliyekuwa katika umri  wa ujana, miaka ishirini na minane hivi.

Baada ya kumnasa na kuendelea naye kimapenzi kwa muda, walikuja kushindana baada ya Helen kugundua kuwa yeye alikuwa ni mtu anayejihusisha na kazi za uhalifu. Hivyo basi, John Bosho akaamua kujiweka kando na kuendelea na shughuli zake za kibiashara ndani ya jiji la Dar es Salaam na hata nje ya nchi.

Ingawa walikuwa wametengana, John na Helen walikuwa wanaishi kama ‘Paka’ na ‘Panya’, kwa kila mmoja akimwogopa mwenzake. John alimwogopa Helen asije akamchoma na kutoa siri zake kwa Jeshi la Polisi, juu ya kazi yake ya uhalifu aliyokuwa anaifanya, Helen Fataki naye alimwogopa John Bosho asije akamlipua na kumwondoa uhai ili asiweze kutoa siri zake nje, ambazo akiwa kama mpenzi wake, alikuwa anazifahamu!

Ni mara nyingi John Bosho alikuwa akimtishia maisha kwa kumwonya kutoitoa siri ile kamwe! Hivyo Helen Fataki akawa ameshikwa pabaya, akautia mdomo wake kufuli kwa kutoitoa siri ile kwa mtu yeyote. Basi ukawa mchezo wa kuwindana, hadi John Bosho alipokutana na mwanadada yule, Anita, ndani ya Hoteli ya The Kibo II Anex muda na wakawa wanafahamiana kwa undani zaidi!

Baada ya John Bosho kumkabidhi kadi yake ya kibiashara, mwanadada huyo akatabasamu kidogo, halafu akasema:

“Nashukuru sana kwa kunipatia kadi yako ya kibiashara….”

“Na mimi nashukuru pia, kwa kuipokea…” John Bosho akamwambia huku akiunda tabasamu pana.

“Kwa jina naitwa Anita Anthony. Ninafanya kazi katika shirika moja lisilo la kiserikali. Bado sijaolewa…”  akajitambulisha mwanadada huyo, aliyejulikana kwa jina la Anita.

Pia yeye akampatia kadi yake ya kibiashara kutoka katika pochi yake ndogo, aliyoitoa ndani ya mkoba wake uliokuwa pale juu ya meza.

“Nashukuru sana kwa kunipatia kadi yako. Utanisamehe sana, lakini huu ndiyo mwanzo wa kufahamiana…” John Bosho akamwambia Anita.

“Na mimi nashukuru pia…” Anita naye akamwambia huku akimwangalia kwa chati. Halafu akaendelea kumalizia chakula chake taratibu.

Mwadada huyo mrembo, Anita Anthony, alikuwa amezaliwa na kukulia kwenye familia iliyojimudu kimaisha. Alikuwa ni mtoto wa pekee wa kike kwa wazazi wake, jambo ambalo lilimfanya alelewe kwa kudekezwa kidogo. Alizaliwa na kukulia eneo la Kiwalani, Jijini Dar es Salaam, akiwa na wazazi wake, Mzee Anthony Mkonyi na mama yake mzazi, Bi. Matilda Msechu, wakiwa na asili ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Pia, Anita alikuwa na kaka zake wawili waliomtangulia, waliojulikana kwa majina ya Peter na Joseph. Alipata Elimu yake ya Msingi, katika  Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, jijini Dar, ambapo baada ya kumaliza, alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tambaza. Alisoma pale hadi alipohitimu kidato cha sita, ndoto ambayo alikuwa nayo muda mrefu hasa ukizingatia aliithamini elimu.

Baadaye alijiunga na Chuo cha Uhasibu Chang’ombe na kufanikiwa kupata Shahada yake ya Uhasibu. Hakika Anita alifurahi sana na hatimaye akaajiriwa na Shirika moja lisilo la Kiserikali, akiwa katika kitengo cha fedha, kama  mtunza fedha. Ofisi ya shirika hilo, iko ndani ya Jengo la Shirikisho la Vyama vya Ushirika, lililoko mtaa wa Lumumba, eneo la Mnazi Mmoja.

Anita aliipenda kazi hiyo na kuifanya kwa moyo mkunjufu, akiwa bado msichana mwenye umri wa miaka 26 hivi, mbichi kabisa. Tuseme alikuwa ni mtu mwenye kiu ya maendeleo, aliyependa kujiondoa katika tatizo la kuwa tegemezi. Hivyo basi, baada ya kukutana na John Bosho siku hiyo, naye alijikuta akimpenda kijana huyo mtanashati, ukizingatia naye alikuwa akimwona kila mara na kuridhishwa na ule utanashati wake.

Baada ya John Bosho na Anita kufahamiana, walikaa pale hotelini kwa muda huku wakishushia chakula kwa vinywaji baridi, wakiongea hili na lile kama vile watu waliokuwa wamefahamiana muda mrefu. Walipomaliza wakaagana na kuahidiana kukutana siku nyingine, na hata kuwasiliana kwa mawasiliano ya simu zao za kiganjani.

Anita alipotoka pale hotelini, alielekea ofisini, anakofanyia kazi, ndani ya Jengo la Shirikisho la Vyama vya Ushirika. Kwa vile hapakuwa mbali, alitembea kwa miguu tu huku wakiongozana na John Bosho. Walipofika nje, John Bosho akaliendea gari lake lililokuwa eneo la maegesho, akapanda na kuondoka kuelekea katika mishughuliko yake mingine ya siku ile.

 Anita alipoingia ofisini kwake, alikaa kitini na kufungua pochi yake aliyoitoa ndani ya mkoba. Akaitoa ile kadi ya kibiashara aliyopewa muda ule walipokutana na John Bosho, halafu akaiangalia kwa makini, na aliporidhika, akairudisha ndani ya pochi na kuendelea na kazi zilizokuwa zinamkabili.

Ukweli ni kwamba, ingawa Anita alikuwa ameshampenda John Bosho Lakini hakuwa akimjua undani wake sana, kwa vile ilikuwa ndiyo mara ya kwanza wamekutana.

ADVERTISEMENT