In Summary

Washambuliaji wa Senegal ni Sadio Mane (Liverpool), Mbaye Niang (Rennais), Mbaye Diagne na Pape Cisse (Olmpiacos), Moussa Konate (Amiens), Santy Ngom (Nancy), Ismaila Sarr (Rennais) na Keita Balde (Inter Milan).

Dar es Salaam. Rekodi ya upachikaji mabao katika mechi za kimataifa, zinaiweka kwenye hali nzuri kisaikolojia safu ya ushambuliaji ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) huko Misri hasa mchezo wa kwanza dhidi ya Senegal.

Licha ya kutamba katika klabu za Ulaya na kuwa na wachezaji wenye majina makubwa, washambuliaji wa Senegal wanapigwa bao na wale wa Taifa Stars kwa rekodi ya kufumania nyavu wanapokuwa kwenye timu yao ya Taifa inaposhiriki mashindano mbalimbali.

Senegal imewaita washambuliaji saba katika kikosi chao cha nyota 23 kitakachoshiriki AFCON ambacho kitacheza mchezo wa kwanza na Taifa Stars Jumapili Juni 23 kwenye Uwanja wa 30 June Air Defence, nchini Misri.

Mchezo huo ndiyo unatazamwa zaidi na timu zote mbili kwani utaanza kutoa taswira ya kila upande katika fainali hizo.

Washambuliaji hao ni Sadio Mane (Liverpool), Mbaye Niang (Rennais), Mbaye Diagne na Pape Cisse (Olmpiacos), Moussa Konate (Amiens), Santy Ngom (Nancy), Ismaila Sarr (Rennais) na Keita Balde (Inter Milan).

Wakati Taifa Stars ikihesabu siku kujiandaa kwa mchezo huo, rekodi zinaonyesha safu yake ushambuliaji ina mabao mengi kulinganisha na ile ya Senegal kwenye mechi zinazohusisha timu za Taifa.

Washambuliaji wanne tu wa Taifa Stars wamefunga mara 50 idadi ya mabao ambayo ni 11 zaidi ya mabao yaliyofungwa na washambuliaji saba walioitwa kwenye kikosi cha Senegal ambao kwa pamoja wamezifumania nyavu mara 39 katika mechi tofauti za timu ya Taifa.

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ndiye kinara wa mabao katika fowadi ya timu zote mbili akiwa na mabao 17 katika michezo 48 aliyocheza wakati kwa Senegal, Mane ndiye anaongoza akiwa amezifumania nyavu mara 16 katika michezo 60 tangu 2012.

Washambuliaji wengine wa Taifa Stars ni John Bocco ambaye amefunga mabao 16 katika mechi 69 alizocheza kwenye timu ya Taifa, Saimon Msuva mechi 53 mabao 10 na Thomas Ulimwengu mechi 45  mabao 7.

Upande wa Senegal, mbali na Mane anayeongoza kwa kuzifumania nyavu, Moussa Konate ndiye anafuatia akiwa amefunga mabao 12 katika mechi 32 alizocheza kwenye timu ya Taifa.

Wengine ni Keita Baldé ambaye ana mabao manne katika mechi 23, Ismaïla Sarr mechi 21 mabao 3, M’Baye Niang mechi 14 mabao 4 wakati Mbaye Diagne aliyecheza mechi nne na Santy Ngom aliyecheza mechi tatu wakiwa hawajapachika mabao.

Lakini wakati Stars wakitambia rekodi ya washambuliaji wake, upande wa Senegal wenyewe wanajivunia mlinda mlango wao Abdoulaye Diallo ambaye hajawahi kupoteza pambano katika mechi zake 17 alizoidakia timu hiyo tangu 2015, rekodi ambayo pia ameiweka kwenye timu ya vijana chini ya miaka 19 na 20 ya Ufaransa ambako amewahi kucheza na kudaka mara 10 katika kila timu.

Matokeo awali Stars vs Senegal

Taifa Stars na Senegal zilikutana mara mbili mwaka 2007 katika kusaka tiketi ya kufuzu kucheza Afcon ya 2008.

Machi 24, 2007 Taifa Stars ilikubali kipigo cha mabao 4-0 nchini Senegal kabla ya kutoka sare ya bao 1-1  katika mchezo wa marudiano Juni 2  Dar es Salaam, mfungaji wa Taifa Stars akiwa Nizar Khalfan chini ya Kocha Mbrazil, Marcio Maximo.

Rekodi

Katika michezo sita iliyopita ya timu hizo, rekodi zinaonyesha kila moja imeshinda mara tatu, lakini Senegal imefungwa mara mbili na kutoka sare moja, wakati Taifa Stars imefungwa mara moja na kutoka sare mbili.

Wadau waipa mbinu

Wakati rekodi ikiibeba Taifa Stars, wadau wa soka nchini wamesema kama Taifa Stars ikitulia na kucheza mechi hiyo kwa nidhamu ya hali ya juu inaweza kuiduwaza Senegal.

“Kikubwa katika mechi hiyo ni Stars kuwa makini, wawaheshimu Senegal kwa kuwa katika viwango wako juu hivyo watulie na kufanya mashambulizi ya kushitukiza,” alisema mchambuzi wa soka, Ally Mayay.

Alisema inawezekana Taifa Stars kuifunga Senegal na hiyo itakuwa ni zaidi ya mafanikio kwao ingawa hata sare katika mchezo huo itawajengea kujiamini katika mchezo wa pili.

Kipa wa zamani wa Taifa Stars, Idd Pazi alisema timu hiyo inapaswa kuwa na nidhamu ya kujilinda, kupambana kuhakikisha hawafungwi katika mchezo huo.

“Wakitaka kujifananisha na Senegal watafungwa mabao rahisi, waingie uwanjani kwa kuwaheshimu na ikiwezekana dakika 20 za mwanzo wajilinde huku wakiwasoma wapinzani wao kabla ya kuanza kushambulia kwa kushitukiza,” alisema.

Nyota wa zamani wa Taifa Stars, Hussein Ngulungu alisema Kocha Emmanuel Amunike ana mikakati madhubuti, lakini akasisitiza kwamba Watanzania wasiwe na matarajio makubwa ya kupata matokeo chanya.

“Sare kwetu itakuwa ni mafanikio, lakini ikitokea tumeshinda itawajenga vijana wetu,” alisema nyota huyo wa zamani.

ADVERTISEMENT