In Summary

Shida ni Manchester United kama wanaweka ngumu hivi, wakidai kiungo wao huyo anauzwa kwa Pauni 150 milioni.

Madrid, Hispania. ASIKWAMBIE mtu, Real Madrid wanateswa sana na huduma ya kiungo Mfaransa, Paul Pogba. Mchana usiku wanahitaji atue kwenye kikosi chao.

Lakini, shida ni Manchester United kama wanaweka ngumu hivi, wakidai kiungo wao huyo anauzwa kwa Pauni 150 milioni.

Basi katika kutafuta kuwalainisha Man United, Real Madrid wamepanga kumtumia staa mmoja baina ya Gareth Bale au Isco katika kubadilishana na Pogba ili akakipige kwenye kikosi chao.

Los Blancos dhamira yao ipo wazi ya kutaka kumsajili Pogba kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huku mwenyewe akisema kwamba umefika wakati wa kwenda kukamilisha na changamoto mpya.

Huko Madrid, mastaa Bale na Isco wote wameshafunguliwa mlango wa kutokea, lakini kwa sababu itakuwa ngumu kupatikana mnunuzi wa moja kwa moja, Real Madrid wanataka kuwatumia mastaa hao kama chambo ya kumpata staa wanayemtaka, Pogba.

Jambo zuri ni kwamba Bale na Isco wote kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kutua huko Old Trafford, hivyo linaweza kufanya jambo hilo kuwa jepesi. Man United wanamtaka Isco hasa ikizingatiwa kwamba bado hawajafahamu hatima ya kiungo wao wa Kihispaniola, Juan Mata.

Real Madrid wao wameshafanya matumizi ya Pauni 268.6 milioni kuwanasa wachezaji kama Eder Militao, Rodrygo Goes, Luka Jovic, Fernald Mendy na Eden Hazard kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi hivyo wanataka kufungua milango kwa baadhi ya mastaa waliopo hapo waondoke.

Jambo hilo wanataka kumtumia ama Bale au Isco pamoja na pesa ili kumchukua Pogba, kutokana na Man United kumthaminisha kiungo wao kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni.

ADVERTISEMENT