In Summary

Kiungo huyo aliachwa na ndege hiyo kutokana na kutakiwa kwenda kufanya vipimo vya mkojo kujua kama ametumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni

Turin, Italia. Kiungo Paul Pogba ameikosa ndege ya kurudi Manchester na wachezaji wenzake baada ya kutakiwa kufanyiwa vipimo vya kuona kama ametumia dawa kufuatia ushindi mzuri wa Man United mabao 2-1 dhidi ya Juventus.

Kiungo huyo Mfaransa alitua kwenye Uwanja wa ndege wa Manchester Airport saa moja baada ya wachezaji wenzake kuwasili wakitokea Turin.

UEFA ina utaratibu wa kuchagua wachezaji yeyote kutoka timu zinazocheza kwa lengo la kupima mkojo kubaini matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku mchezoni kila baada ya mechi. 

Jambo zuri ni Jose Mourinho na vijana wake kurejea mapema wakiwa na furaha kubwa ya ushindi asubuhi ya leo Alhamisi baada ya mafanikio katika mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa.

Kocha huyo alipokewa na Makamu mwenyekiti Ed Woodward baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Manchester.

Mabao ya Juan Mata kwa mpira wa adhabu pamoja na lile la kujifunga kwa Alex Sandro katika dakika tano za mwisho kwenye Uwanja wa Allianz yalitosha kuiweka Man United katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya mtoano.

Ushindi huo ni ishara njema kwao kabla ya mchezo wao wa Jumapili dhidi ya watani wao wa Jadi vinara wa Ligi Kuu Manchester City huku Mourinho akitaka kubadilisha mwanzo mbaya wa Man United.

 

Man United ilikubali bao la mapema lililofungwa na Cristiano Ronaldo, lililoamsha shangwe kwa wenyeji wa jiji la Turin, lakini walifanikiwa kurudi mchezo na kuondoka na ushindi huo.

Man United bado wapo nafasi ya pili nyuma ya Juventus katika Kundi H, wakihitaji pointi mbili ili kujihakikishia kufuzu kwa 16 bora, kama watashinda mechi yao dhidi ya Young Boys kwenye Uwanja Old Trafford huku wakiomba Juventus iifunge Valencia.

ADVERTISEMENT