In Summary

Kuhusu idadi ya wanasoka walio chini yao, Okoth anasema kuwa, mbali na
wachezaji wa ligi kuu ya Kenya (KPL) na wale wanaocheza katika ligi
mbalimbali za ndani, ROSMA tayari wameshapata maombi kutoka Burkina
Faso, Tanzania, Uganda na Zanzibar.

MAISHA ya soka ni mafupi sana. yanaanzia umri wa miaka 18-30. Kung’ara
kwenye ulimwengu wa soka ukiwa chini ya miaka 18 ni bahati. Kutesa
baada ya umri wa miaka 30, ni bahati pia. Wengi hawavuki hapa, na hata
wakivuka, huvuka wakiwa wachovu kweli kweli.


Kutokana na hili, ndio maana ni vizuri kwa mwanasoka kujipanga.
Kujipanga kwa maana ya kwamba wakati bado ana nguvu na kipaji chake
kinauzika, ni lazima ahakikishe, miguu yake ifanye kazi ya kumpatia
mafanikio yanayomtosha kusukuma maisha baada soka.

Ukiachana na suala la umri, katika maisha haya mafupi ya soka kuna
changamoto kibao tu. Majeraha ya kila mara. Vita ya kupigania namba.
Kutapeliwa na mawakala feki. Kutumikishwa vibaya na vilabu.
Kucheleweshewa malipo na kadhalika.

Kutokana na hilo, Straika wa zamani wa Gor Mahia na Mathare United,
Ronald Okoth (30), aliamua kujitoa muhanga, kwa ajili ya manufaa ya
baadae ya wanasoka wenzake na maendeleo ya Soka la Kenya. Kiu yake
ilikuwa ni kufuta dhuluma dhidi ya wanasoka.

Katika umri wa miaka 29, akiwa bado ana nguvu za kuendelea kusakata
kabumbu, Okoth alitundika daluga na kuamua kufuata njia waliyofuata
Mino Raiola na Jorge Mendez. Aliamua kujikita katika kazi ya uwakala
na usimamizi wa michezo.

Mapema mwaka huu, Mwanasoka huyo aliyewahi kukipiga katika klabu ya
Jericho All Stars, Congo United, Mahakama FC, Nairobi Stima FC,
Western Stima FC na KCB, aliamua kuanzisha Kampuni ya RO Sports
Management (ROSMA).

Hivi karibuni, Mwanaspoti ilipata kuchonga na mhitimu huyo wa Shahada
ya Sayansi ya Mawasiliano, kutoka Chuo Kikuu cha Kenya Methodist,
ambaye anaeleza maana ya ROSMA, majukumu yake na kilichopelekea
kuanzishwa kwa ROSMA.

“RO Sports Management, ni kampuni ya michezo inayojihusisha na
usimamizi na utafutaji wa soko kwa ajili ya wachezaji ambao ndio
wateja wetu. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha tunatambua vipaji vya soka
na kuviuza katika klabu za ndani na nje ya nchi,” anasema Okoth.

Kwa mujibu wa Okoth, moja ya mambo yaliyompelekea kuamua kuchana na
soka na kujikita katika kazi hiyo, ni changamoto walizopitia katika
kutafuta vilabu vya kuchezea, ambapo kwake yeye, anasema ilibidi
ajitume sana, kabla ya Jericho All Stars, kuamua kumsajili.

“Unapoangalia ‘hustle’ ambayo maplayer wanapitia kusaka timu,
unagundua kuwa kuna haja ya kuwa na mawakala waliosajili. Huko mitaani
kumejaa matapeli, wanasoka wengi hujikuta wakipoteza muda wao, kucheza
soka bila malipo, sio kwamba klabu hailipi, lakini kiasi kikubwa cha
malipo huishia kwenye mifuko ya mawakala hawa feki”

Kuhusu idadi ya wanasoka walio chini yao, Okoth anasema kuwa, mbali na
wachezaji wa ligi kuu ya Kenya (KPL) na wale wanaocheza katika ligi
mbalimbali za ndani, ROSMA tayari wameshapata maombi kutoka Burkina
Faso, Tanzania, Uganda na Zanzibar.

“Muitikio ni mzuri sana, tofauti na tulivyotarajia. Mpaka sasa tuna
zaidi ya wachezaji 16 walioomba kufanya kazi nasi, kutoka ndani na nje
ya Kenya. Tumeingia mkataba na wanne, kwa sababu unajua kumanage watu
wengi pia si rahisi,” anasema Okoth, ambaye pia ni Mchambuzi wa Soka
kwenye Runinga na Redio.

Licha ya kuingia mkataba na wachezaji wanne tu, ambao ni Roy Okal na
Chris Ochieng wa Mathare United FC, Harun Pamba wa Nairobi Stima FC na
Moses Mburu wa AFC Leopards, ROSMA pia inaendelea kutoa huduma kwa
wengine 12 waliosalia, pale panapohitajika, wakiwa na matumaini ya
kuingia nao mkataba katika siku za usoni.

Kwa kuwa maisha ya uchezaji Soka, haidumu zaidi ya miaka 20, kuna haja
ya mchezaji kujipanga namna ya kuishi maisha baada ya Soka, na kwa
kutambua hilo, Okoth anasema kuwa, mbali na kuwasaini wachezaji hao na
kuwatafutia vilabu, ROSMA pia imejipanga kuhakikisha wateja wake
wanakuwa na maisha mazuri baada ya kutundika daluga.

Anasema kuwa, kazi ya kwanza ni kuwaelekeza namna bora ya kusimamia
fedha, kwani historia inaonesha kuwa wachezaji wengi hawana desturi ya
kuweka akiba na mara nyingi hujiingiza katika anasa, akitolea mfano
masaibu yaliyomkuta nyota wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa maisha ya wachezaji hayategemei soka,
Okoth ambaye pia ni Mfanyabiashara na mbunifu wa mavazi, anasema
ROSMA, pia inalenga kuwaendeleza wateja wao kielimu, kuwasaidia
kuingia katika biashara na ujasiriamali na kutawatafutia dili la
matangazo.

“Soka la Kenya linakuwa kwa kasi kubwa sana, lakini niamini kuwa sio
wachezaji wote wanaonufaika na kasi hii ya ukuaji. Hii inatokana na
changamoto nyingi wanazopitia, changamoto hizi, huwakatisha tamaa,

Lengo letu ni kuondoa changamoto hizi. Tunataka wachezaji wasiwaze
kitu kingine zaidi ya kucheza soka kwa ufanisi, hilo linawezekana
wakiwa na maisha ya uhakika. Unapompa mchezaji uhakika wa kupata
chakula, makazi na pesa ya kuendesha maisha, lazima atakupa
unachokitaka uwanjani,

Unajua katika, maisha huwezi tegemea kazi moja. Tunataka kwanza
kuwaendeleza kielimu wachezaji hawa, baada ya hapo tutawasaidia kukuza
vipato vyao, kwa kuwaingiza kwenye biashara na kuwatafutia dili la
matangazo kwenye makampuni.” Anasema Okoth.

Majukumu mengine ya ROSMA, ni kuhakikisha video na wasifu wa wachezaji
waliochini ya menejimenti yake, zinapatikana kwa urahisi na haraka
kwani, mara nyingi wachezaji wengi wamekuwa wakifeli majaribio huko
nje, kutokana na kukosa wasifu inayoeleweka.

Mbali na hilo, Okoth ameanza mpango wa kushirikiana na mawakala
wengine wakubwa wa soka duniani kama Jorge Mendez, Mino Raiola na
wengine kibao, kutangaza vipaji vya soka vilivyoko nchini na Barani
Afrika.

Yote tisa, kumi ni kwamba, Okoth anasema amejipanga kutoa msaada wa
kisheria na ushauri wa namna ya kukabiliana na maisha baada ya soka.
Tayari ROSMA, imeonesha nia, kikubwa ni wadau kuwaunga mkono. Kila la
heri ROSMA!

ADVERTISEMENT