In Summary
  • Michuano hii ndio inayotoa mwakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ndio maana msisimko wake umekuwa mkubwa kwa kila timu ambazo hazina nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambaye hutoa mwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hutumia nguvu kubwa kuhakikisha wanashinda taji hilo la FA ili kushiriki michezo ya kimataifa.

MICHUANO ya Kombe la FA maarufu kama Azam Sports Federation Cup, ipo msimu wa nne tangu iliporejeshwa tena na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya utawala wa Jamal Malinzi.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 2016 na kushuhudiwa Yanga wakibeba taji kabla ya Simba kunyakua msimu wa pili na mwaka jana Mtibwa Sugar walilitwaa kwa kuifunga Singida United kwenye fainali kali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Msimu huu wa nne unaoingia hatua ya 16 Bora umekuwa na msisimko mkubwa na mashabiki wa soka wanaendelea kupata uhondo waliokuwa wameukosa kwa muda mrefu.

Kwa wanaokumbuka michuano hii ilisimama awali tangu 2002 ilipochezwa mara ya mwisho ya JKT Tanzania (enzi za JKT Ruvu) kutwaa taji la mwisho, hivyo kurejeshwa upya kumeongesha msisimko kwa kuwapa fursa wachezaji wa klabu shiriki kucheza zaidi katika msimu mmoja.

Michuano hii ndio inayotoa mwakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ndio maana msisimko wake umekuwa mkubwa kwa kila timu ambazo hazina nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambaye hutoa mwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hutumia nguvu kubwa kuhakikisha wanashinda taji hilo la FA ili kushiriki michezo ya kimataifa.

Michuano hiyo ni miongoni mwa mashindano inayosaidia kuwapa fursa wachezaji na klabu zisizo za Ligi Kuu kuonyesha ujuzi wake na kupata uwakilishi wa nchi kwa wanaokumbuka wakati wa mfumo wa awali wa michuano hiyo, Tanzania Stars, iliyokuwa ikiundwa na wachezaji nyota wa zamani iliwahi kuiwakilisha nchi kwa miaka miwili mfululizo, mwaka 1997 na 1998.

Hivyo kurejeshwa kwa Kombe la FA ni faraja na furaha kubwa kwa wadau wa soka waliokuwa wakiililia michuano michuano hiyo ili kuzipa nafasi klabu nyingine fursa ya kuiwakilisha nchi mbali na timu za Ligi Kuu.

Mwanaspoti linafurahishwa na namna michuano ya FA inavyoboreshwa kila msimu na kuifanya iwe na msisimko mkubwa, huku ikiihimiza TFF kuhakikisha inaendeshwa kwa ufanisi na kusaidia kupata wadhamini zaidi.

Licha ya hivyo, lakini Mwanaspoti pia inaiomba TFF kuangalia haja ya kurejesha michuano ya Kombe la Taifa, michuano mingine iliyokuwa mitamu miaka kadhaa ya nyuma.

Michuano ya Kombe la Taifa iliyokuwa ikishirikisha timu za mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara inakumbukwa namna ilivyosaidia kuibua vipaji vya soka mbalimbali kwa miaka mingi kabla ya kuanza kupoteza mvuto wake kwa kuendeshwa kwa mtindo wa bora liende.

Tunaamini kuna umuhimu mkubwa wa kurejeshwa kwa michuano hiyo kama ilivyofanywa kwa Kombe la FA, ingawa miaka michache iliyopita chini ya utawala wa Leodger Tenga ndani ya TFF iliwahi kutangazwa ingerejeshwa, lakini ikakwamishwa kwa kukosekana kwa wadhamini.

Kwa kuwa ni miaka mingi tumekuwa tukilia kushindwa kupata vipaji vipya ambavyo vingekuwa msaada mkubwa kwa timu zetu za taifa, Mwanaspoti inaamini michuano ya Kombe la FA, Kombe la Taifa na mingine inayoweza kubuniwa na kuendeshwa itarejesha heshima ya soka letu hasa katika ukanda huu.

Mikoani kuna vipaji vingi vya soka, lakini havionekani kwa sababu hakuna michuano inayoweza kuwaibua na kuwafanya waonwe kama ilivyowatoa wenzao kupitia michuano ya Kombe la Taifa na hata hiyo ya FA.

Hivyo tunatoa wito kwa TFF na wasimamizi wengine wa michezo ikiwamo Wizara ya Michezo na Hata Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuangalia namna ya kurejesha michuano mingine iliyozimika kitambo na kuliingia soka letu katika kaburi la sintofahamu.

Kuwepo kwa michuano mingi zaidi kutafanya wachezaji wapate muda mrefu wa kucheza na pia kuwibua vipaji ambavyo havifahamiki kwani kwa wanaokumbuka michuano ya Taifa Cup iliwahi kumuibua Mohammed Chuma kutoka Mtwara aliyeichezea Taifa Stars kwa mafanikio kwa muda wa miaka 10 mfululizo.

Kama isingekuwapo kwa michuano hiyo, huenda Chuma asingefahamika wala kuja kulisaidia taifa, ndio maana tunakumbusha kwa viongozi wa sasa wa TFF kuangalia namna ya kuirejesha tena michuano hiyo kwa manufaa ya soka la Tanzania.

Hata mataifa mengi yaliyoendelea yamekuwa yakisistiza michuano mbalimbali kwa ajili ya kuibua vipaji na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa.

TFF haijachelewa na vipaji vingi vinazaliwa kila kukicha, ni wakati sasa kwa wao kuanza kuanzisha ligi mbalimbali za ndani kuanzia ngazi ya chini ikiwamo pia kurejesha michuano ya Kombe la Taifa kama tunataka soka letu likue.

Vijana wengi wamekuwa wakilalamika vipaji vyao vimekuwa vikipotea bure kutokana na kukosa ligi za kushiriki na hii ni kwa sababu hata wale wanaoziongoza timu zao huko mitaani wanashindwa pa kusipeleka, lakini kama kungekuwa kuna michuano imenzishwa zingeshiriki na kutoa vipaji.

Tunasisitiza tena, kwa nia njema ya kuinua soka letu na kuweza kukabiliana kisoka na mataifa yaliyoendelea ni muhimu kwa TFF kurudisha michuano ya kombe la Taifa na kuandaa michuano mingi zaidi kuweza kutoa vipaji vipya.

ADVERTISEMENT