In Summary

Kocha Ndayiragije baada ya kutambulishwa uongozi wa Azam ulimuonyeshea baadhi ya majina ya wachezaji aliopendekezwa kwa ajili ya kusajili.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Kombe la FA, Azam imeanza kujiimarisha kikosi chake kwa kuwaongezea mikataba wachezaji wao na kusajili wapya kwa msimu ujao.

Mabosi hao wa Chamazi walikuwa wameshaanza mazungumzo na wachezaji mbalimbali, lakini walisimama kutokana na kocha Ettiene Ndayiragije aliwaomba kusubili mpaka yeye afike.

Kocha huyo baada ya kutambulishwa uongozi wa Azam ulimuonyeshea baadhi ya majina ya wachezaji ambao walipendekezwa na yeye akaanza kupitisha mchujo.

Leo asubuhi kulikuwa na kikao cha vigogo wa klabu hiyo ambapo walijadiliana kuhusu mustakabali wa msimu ujao ndipo kocha huyo akalipitisha jina la Iddi Selemani 'Idd Nado' kutoka Mbeya City.

Chanzo kimoja kutoka ndani ya timu hiyo kililiambia Mwanaspoti mchezaji huyo anasaini mkataba muda wowote kwani maongezi ya pande mbili yameshakamilika.

"Anasaini miaka miwili muda wowote mwalimu tayari yeye pia amelizika naye, ni mchezaji mzuri tunaamini kabisa ataisaidia timu yetu," alisema.

Chanzo hiko kiliongeza wachezaji wengine ambao watasaini muda wowote ni Braison Raphael (miaka miwili) ambaye alikuwa kwa mkopo KMC na kipa Benedict Haule (miaka miwili).

Azam msimu ujao watashiriki kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuchukua Kombe la FA, kwa kuifunga Lipuli bao 1-0 lililofungwa na Obrey Chirwa.

ADVERTISEMENT