In Summary

  • Akiongea wakati wa mazoezi ya timu yake uwanjani Mbaraki Sports Club jana asubuhi, Mwalala alisema hakuna tatizo lolote timuni na kwamba wangali na matumaini ya kufikia lengo lao la kufanya vizuri na hata kuchukua ubingwa.

MOMBASA. KOCHA Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala jana aliwataka mashabiki wao waondowe wasiwasi kutokana na kushindwa na Kakamega Homeboys na badala yake, wafike kwa wingi kuishangilia timu inapocheza na Nakumatt FC hapo kesho.

Wakati huo huo, Mwalala amesema huenda hapo kesho akampa muda wa kucheza beki Fred Nkata ambaye amekuwa majeruhi kwa kipindi kirefu. “Nkata ameanza mazoezi magumu na wenzake na hivyo, naweza kumpa muda wa kucheza Jumatano,” akasema.

Akiongea wakati wa mazoezi ya timu yake uwanjani Mbaraki Sports Club jana asubuhi, Mwalala alisema hakuna tatizo lolote timuni na kwamba wangali na matumaini ya kufikia lengo lao la kufanya vizuri na hata kuchukua ubingwa.

“Yataka ifahamike kuwa tungali na nafasi ya kupanda tena juu kwani timu zilizo juu yetu zikiteleza na kupoteza mechi, tutarudi tulipokuwako. Hii ndio hali ya mchezo, naomba  tushirikiane kuhakikisha tumefanikiwa kufikia lengo letu katika mechi zetu zijazo,” akasema.

Alisema kwa wakati huu, wana majeruhi watatu- Wycliffe Ochomo, Wilberforce Lugogo na David King’atua lakini akawa na matumaini ya baadhi ya hao kupona na kucheza mechi kabla ya ligi kumalizika.

Alisema wana ushirikiano mzuri sana na maofisa wa timu na mashabiki na akaomba ushirikiano huo udumishwe ili kupatikane mafanikio. “Kupoteza pointi kadhaa kusitufanye kuvunjika nguvu bali tuzidi kushirikiana tuweze kutimiza lile tunalolitaka,” akasema Mwalala.

Timu hiyo ya Bandari inatarajia kupambana na Kariobangi Sharks siku ya Jumapili katika mechi nyingine ya ligi kuu na kuwakaribisha Gor Mahia kwenye mechi ya SportPesa Shield siku ya Jumatano ya wiki ijayo, zote zikiwa uwanja wa nyumbani.

ADVERTISEMENT