In Summary

Siku hiyo mapambano matano yatapigwa kwenye ukumbi huo, huku mawili kati yake yakiwa hayana wapinzani, jingine ni la Nicholas Mwangi, ingawa awali Mwakinyo alikuwa acheze na Ocampo.

BONDIA Hassan Mwakinyo amebakiza siku tisa tu kupanda ulingoni kuonyesha uwezo wake , pambano ambalo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa ngumi kuhusu mpinzani wake.

Wapo wanaodhani kufanywa siri kwa mpinzani wake ni dalili mbaya kwa Mwakinyo na atapoteza pambano hilo, pia wapo wanaoamini hakuna ulazima wa kumjua mpinzani wake.

Pambano la Mwakinyo limewekwa kwenye mtandao wa ngumi za kulipwa wa Dunia (Boxrec) ambao, unaonyesha bondia huyo Mtanzania atazichapa pambano la raundi nane Machi 23, mwaka huu, kwenye Ukumbi wa Kenyatta International Conference Centre, jijini Nairobi, Kenya.

Hata hivyo, mpinzani wake hajawekwa wazi, japo Mwakinyo atazichapa pambano la utangulizi kumsindikiza Fatuma Zarika atakayekuwa akitetea ubingwa wake wa dunia wa WBC dhidi ya Catherine Phiri.

Siku hiyo mapambano matano yatapigwa kwenye ukumbi huo, huku mawili kati yake yakiwa hayana wapinzani, jingine ni la Nicholas Mwangi, ingawa awali Mwakinyo alikuwa acheze na Ocampo.

“Sio lazima mpinzani wa bondia kuwekwa kwenye boxrec, kama amesaini mkataba wa pambano basi bondia mwenyewe atakuwa akimfahamu mpinzani wake, hao wengine wanaohoji atacheza na nani watulie,” alisema wakala wa ngumi nchini, Emmanuel Mlundwa.

Msikie Mwakinyo sasa

Bondia huyo ambaye yuko Uingereza kwa zaidi ya mwezi mmoja chini ya udhamini wa SportPesa Tanzania amewaambia wanaohoji kuhusu mpinzani wake wamuulize matokeo na si kutaka kujua anacheza na nani.

“Najua wapo wenye hofu kuwa huenda nitapigwa ndiyo sababu mpinzani wangu amefishwa, mimi sio bondia wa hivyo, najiandaa nikijua nacheza na nani, hivyo mashabiki wangu wajiandae kuuliza matokeo sio mpinzani wangu,” alisema Mwakinyo.

SportPesa yamtaja mpinzani wake

Mwanaspoti halikuishia hapo, limemfichua mpinzani wa Mwakinyo na sasa si kitendawili tena kwa wadau wa ngumi, japo kwenye Boxrec amefichwa.

Sasa bondia huyo atazichapa na Sergio Eduardo Gonzalez wa Argentina pambano la uzani wa super welter.

“Tulikuwa tunasubiri taarifa kutoka Liverpool kuhusu mpinzani wa Mwakinyo na sasa atacheza na Gonzalez na si Ocampo,” alisema Sabrina Msuya wa SportPesa.

Alisema Mwakinyo atarejea Machi 20 ambako atakwenda moja kwa moja nchini Kenya tayari kwa pambano hilo.

Rekodi ya mpinzani wake

Gonzalez atashusha uzani kutoka ule wa kati na kumfuata Mwakinyo kwenye super welter.

Bondia huyo anayejiita kwa jina la utani El Zurdo El Tigre anatumia mkono wa kushoto (southpaw) ana uzoefu wa kutosha kwenye ngumi akiwa na rekodi ya kupigana mapambano 58.

Ameshinda mara 31 (15 KO) amepigwa mara 23 (11 KO) na ametoka sare mara nne tangu mwaka 2000 alipoingia kwenye ngumi ana miaka 40.

ADVERTISEMENT