In Summary

Kimsingi, ungeweza kusema kwamba mechi hiyo imeishia hapohapo Etihad, lakini Guardiola amewaambia wachezaji wake kuchukulia siriazi mchezo wa marudiano. Kinachoonekana Burton watakuwa wahanga wa kupigwa nyingi kweli wakati watakapocheza mechi zao mbili zote na mabingwa hao wa England.

MANCHESTER, ENGLAND

PEP Guardiola amewaambia wachezaji wake ni kufungulia mbwa tu mwanzo mwisho kwenye mchezo wao wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya timu ya daraja la chini, Burton Albion. Kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Uwanjani Etihad juzi Jumatano, Manchester City ilishinda mabao 9-0.

Kimsingi, ungeweza kusema kwamba mechi hiyo imeishia hapohapo Etihad, lakini Guardiola amewaambia wachezaji wake kuchukulia siriazi mchezo wa marudiano. Kinachoonekana Burton watakuwa wahanga wa kupigwa nyingi kweli wakati watakapocheza mechi zao mbili zote na mabingwa hao wa England.

Katika mechi hiyo, Gabriel Jesus alipiga nne peke yake, wakati mabao mengine yalifungwa na Kevin de Bruyne, Oleksandr Zinchenko, Phil Foden, Kyle Walker na Riyad Mahrez.

Mechi ya marudiano itapigwa Jumatano, Januari 23. Hiyo ni mara ya kwanza kwa Man City kufunga mabao tisa kwenye mechi moja baada ya miaka 31 iliyopita, ambapo waliichapa Huddersfield Town 10-1 kwenye michuano hiyo, wakati ikiwa imepita miaka 32 tangu kushuhudiwa kwa mabao mengi kwenye mechi moja katika mikikimikiki ya kombe hilo, wakati Liverpool walipojipigia Fulham 10-0, Septemba 1986. Hata hivyo, hiyo si mara ya kwanza kwa soka la Uingereza kushuhudia timu moja ikichapwa mabao kwenye mechi moja.

Southampton 8-0

Sunderland (2014-15)

Kwenye mechi hii, straika Graziano Pelle alifunga mara mbili, kabla ya mastaa wa Sunderland, Santiago Vergini na Liam Bridcutt kujifunga na kisha mabao mengine kutoka kwa Jack Cork, Dusan Tadic, Victor Wanyama na Sadio Mane yakitiririka kwenye nyavu zao na kuifanya Southampton kushinda mechi hiyo kwa mabao 8-0.

Hilo limebaki kwenye kumbukumbu ya kudumu ya kocha Gus Poyet, aliyekuwa akiinoa Sunderland wakati huo.

Man United 9-0 Ipswich (1994-95)

Straika, Andy Cole aliweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mechi moja, wakati alipoweka kambani mabao matano peke yake kuisaidia Manchester United kuichapa Ipswich 9-0.

Kitu kilichoshangaza ni kwamba kwa msimu huo, Man United ilishindwa kubeba ubingwa, lakini mambo mabaya zaidi yalikuwa kwa Ipswich Town kwa sababu walishuka daraja. Hiyo mechi ni moja ya mechi nyingi zilizoshuhudia mabao mengi kwenye soka la Uingereza.

Newcastle 8-0 Sheffield Wednesday (1999-00)

Kwenye mchezo huo, Alan Shearer alimjibu Andy Cole kwa kupiga mabao matano katika mechi moja, wakati alipoisaidia Newcastle United kuangusha kipigo kizito kwa Sheffield Wednesday cha mabao 8-0.

Mechi hiyo ilionyesha mwanzo mzuri kwa kocha, Bobby Robson wakati alipokuwa akianza kazi yake ya ukocha kwenye kikosi cha Newcastle na hivyo kuandikisha ushindi wa kishindo uliobaki kuwa kumbukumbu hadi sasa.

Chelsea 8-0 Aston Villa (2012-13)

Kipindi hicho, Chelsea ilikuwa chini ya kocha Mhispaniola, Rafa Benitez. Wakiwa kwenye ubora wao, Chelsea walicheza kwa kiwango bora kabisa walipowasambaratisha Aston Villa 8-0.

Katika mechi hiyo, straika Fernando Torres alicheza kwa kiwango matata kabisa na kuwafanya watu waamini kwamba Mhispaniola huyo anarudi kwenye ubora wake baada ya uhamisho wake wa pesa nyingi kutoka Liverpool kwa Pauni 50 milioni.

Tottenham 9-1 Wigan (2009-10)

Wigan Athletic ilicheza kwa kiwango cha hovyo kwelikweli kwenye mechi hiyo dhidi ya Tottenham Hotspur na kuwaomba radhi mashabiki wao.

Kwenye mechi hiyo, Wigan ilikubali kichapo cha mabao 9-1 na hivyo kuifanya Spurs kuwa timu ya pili kwenye Ligi Kuu England kufunga mabao tisa kwenye mechi moja baada ya ile ya Man United na Ipswich Town kwenye msimu wa 1994-95. Mechi hiyo inaingia kwenye rekodi za kushuhudia mechi zilizoshuhudia mabao mengi.

Man United 1-6 Man City (2011-12)

Kwenye mechi hii, straika Mario Balotelli alipata umaarufu zaidi wakati alipofunga bao kisha kufunua jezi yake na kuonyesha fulana ya ndani iliyokuwa na maandishi ‘Why Always Me’.

Baada ya hapo, kila kona ishu ilikuwa Balotelli kutokana na kitendo alichokifanya mtukutu huyo, huku Manchester United wakikumbana na udhalilishaji mkubwa wa kufungwa mabao mengi kutoka kwa mahasimu wao Manchester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Mbaya zaidi, Manchester United ilikumbana na kipigo hicho ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford uliofurika mashabiki.

Man United 8-2

Arsenal (2011-12)

Manchester United, ilikuwa na viungo waliopatana zaidi kwa wakati huo, Tom Cleverley na Anderson, waliishushia kipigo kizito Arsenal cha mabao 8-2. Straika, Wayne Rooney alifunga hat-trick, huku kocha Arsene Wenger, aliyekuwa akiinoa Arsenal wakati huo akikiri kwamba kipigo hicho kimemuumiza sana hasa ukizingatia kwamba msimu ndio kwanza ulikuwa unaanza na kichapo hicho kimetoka kwa wapinzani wao wakubwa kwenye Ligi Kuu England.

Everton 7-1

Sunderland (2007-08)

Hakika hiki ni kipindi kibaya zaidi kwa Roy Keane kwenye kazi yake ya ukocha, wakati alipokuwa akiinoa Sunderland iliyokumbana na kipigo cha mabao 7-1 kutoka kwa Everton. Paul McShane alifanya hivyo kumruhusu Yakubu kuifungia Everton bao la kuongoza na baada ya hapo kilichofuatia ni kwamba kipa wake Keane alikuwa bize tu kuokota mipira kwenye wavu wake na hadi mwisho wa mchezo, Sunderland ilichapwa saba, huku mtaani utasikia vijana wanasema Sunderland imepigwa wiki.

Nottingham Forest 1-8

Man United (1998-99)

Kocha wa sasa wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjær wakati huo akiwa mchezaji, alifunga mabao manne peke yake kwenye mechi hiyo, kuisaidia timu yake kuangusha kipigo kizito cha mabao 8-1 kwa Nottingham Forest. Kikosi cha Man United wakati huo kikiwa chini ya kocha Alex Ferguson hakika kilikuwa kwenye ubora wake na ndio msimu huo kilibeba mataji matatu makubwa, huku wakiichapa Bayern Munich kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huko uwanjani Nou Camp.

Chelsea 8-0 Wigan (2009-10)

Huu ni msimu ambao Chelsea ikiwa chini ya kocha, Carlo Ancelotti iliweka rekodi kwenye Ligi Kuu England kwa kufunga mabao mengi, wakati ilimaliza msimu kwa mabao 103. Kabla ya mechi yao ya kuwachapa Wigan 8-0, Chelsea ilikuwa kwenye msimu huo imeshapiga mabao saba timu za Sunderland, Aston Villa na Stoke City, kabla ya kuongeza moja kwa Wigan na kwenda kubeba ubingwa huo wa ligi katika staili ya kipekee kabisa.

Middlesbrough 8-1

Man City (2007-08)

Mechi yake ya mwisho Sven-Goran Eriksson kwenye kikosi cha Manchester City ilimalizika kwa udhalilishaji mkubwa wakati alipokwenda kukutana na kipigo kizito kutoka kwa Middlesbrough huko Uwanjani Riverside. Kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu England, staa wa Boro, Afonso Alves alipiga hat-trick kuhakikisha kwamba Man City wanakufa mabao 8-1 katika mechi tamu kabisa ambayo ndio ilikuwa hitimisho la kocha raia wa Sweden, Erikkson kuwa kocha kwenye kikosi hicho cha Etihad.

ADVERTISEMENT