In Summary
  • Mbali na wanariadha hao wa kike, pia Mtaka alilipa deni la mabati kwa wanariadha washindi katika mbio za Dodoma Marathon zilizofanyika mwaka 2016 ambazo zilitolewa na mdhamini kwa shirikisho kwa ajili ya kuzikabidhi kwa wanariadha lakini zilipotelea mikononi viongozi wa RT.

ARUSHA.Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka amefanikiwa kuzima mgomo baridi waliotaka kuuweka wanariadha nyota wa Tanzania kuelekea mashindano ya wazi ya Taifa kwa ajili ya kuchagua timu itakayoingia kambini kujiandaa na mbio za dunia za nyika ‘World Cross Coutry’ mapema mwezi march katika Mji wa Ahrus nchini Denmark.

Mtaka amefanikiwa kuzima mgomo huo wa kichini chini baada ya kuwalipa wanariadha madeni yao yote waliyokuwa wanadai Shirikisho hilo ikiwemo zawadi za wanariadha wa kike walifanya vizuri mwaka 2017 kwenye mbio za dunia za nyika nchini Uganda kiasi cha shilingi milioni 4.8 zilizotolewa na Shirikisho la Riadha la Dunia (ITF) kupitia mfuko wa RT na kila mmoja alipata mgawo wa Sh800,000.

Wanariadha sita wa kike waliopata mgawo wa fedha hizo ni Failuna Abdi Matanga, Anjelina Daniel Tsere, Magdalena Shauri, Sara Ramadhani, Mayselina Mbua, Siaka Kalinga ambao walikuwa washindi wa sita kwa upande wa timu na kuzawadiwa kiasi cha Dola 6000 ambazo fedha hizo ITF iliziingiza kwenye Akaunti ya RT lakini hadi mwaka huu walikuwa bado hawajapewa.

Akitoa sababu za wanariadha kucheleweshewa fedha hizo na RT wakati zilikwisha tolewa na ITF tangu mwaka 2017, Mtaka alisema kuwa fedha hizo ziliingizwa na shirikisho la riadha Duniani (ITF) kwenye akaunti isiyo sahihi ya RT, hivyo walilazimika kutoa taarifa wazirudishe kwao na watume tena kwenye akaunt sahihi ya shirikisho hali iliyochukua mda mrefu.

Akipokea fedha hizo mmoja wanariadha hao Anjelina Tsere alimshukuru Mtaka kwa kutimiza ahadi hiyo ambayo walishaikatia tamaa ya kuipata tena ambapo amesema hali hiyo imerudisha Imani yao kwa shirikisho na kuahidi kufanya vema zaidi mwaka huu.

Mbali na wanariadha hao wa kike, pia Mtaka alilipa deni la mabati kwa wanariadha washindi katika mbio za Dodoma Marathon zilizofanyika mwaka 2016 ambazo zilitolewa na mdhamini kwa shirikisho kwa ajili ya kuzikabidhi kwa wanariadha lakini zilipotelea mikononi viongozi wa RT.

Wanariadha Gabriel Geay (kwa upande wa wanaume) na Fadhila Salum (wanawake) waliokuwa washindi wa pili katika mbio zile alitakiwa kulipwa bati 100 kila mmoja ambapo walifidiwa kiasi cha shilingi milioni moja kila mmoja (1,000,000) huku Catherine Lange aliyeshika namba tatu alikuwa anadai bati 40 alipatiwa Sh400,000.

ADVERTISEMENT