In Summary
  • Mshambuliaji nguli wa Liverpool Ian Rush amemshauri kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp, kutopoteza nguvu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya badala yake aelekeze nguvu zaidi katika Ligi Kuu England ili aweze kutwaa taji hilo walilokosa kwa kipindi kirefu.

Liverpool, England. Nguli wa Liverpool, Ian Rush amemshauri kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp kutoelekeza nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya badala yake akomae na Ligi Kuu England ili kutwaa ubingwa.

Rush amesema mashabiki wa Liverpool wana kiu cha kutwaa taji la Ligi Kuu kuliko lile la Ulaya hivyo akashauri wasikubali kuiachia mwanya Manchester City.

Alisema kwa mtazamo wake Man City inayonolewa na Pep Guardiola, itapunguza nguvu kwenye Ligi Kuu England na kujikita zaidi katika Ligi ya Mabingwa.

Rush, mwenye miaka 57, anayeshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool, akiwa na mabao 199 katika mechi 427 alizoitumikia alionya kuwa litakuwa kosa iwapo Klopp atataka kukomaliza mataji yote kwa mpigo.

“Nadhani kosa moja kubwa lililofanyika msimu uliopita ni Liverpool kutokuwa na kipaumbele katika taji lolote ndiyo maana tulikosa yote, ninashauri msimu huu tuelekeze nguvu katika Ligi Kuu England,” alisema.

Mara ya mwisho kwa Liverpool kutwaa taji la England ni mwaka 1990 wakati lile la Ulaya mara ya mwiho kulitwaa ilikuwa mwaka 2005.

Aliitaka Liverpool kuhakikisha inaelekeza nguvu katika ligi hiyo na kupania kushinda kila mchezo bila kuangalia Man City inafanya nini wala timu nyingine zinazochuana kuwania ubingwa huo.

Msimu uliopita Liverpool ilimaliza ligi katika nafasi ya tatu na ikafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufungwa na Real Madrid mabao 3-1, katika mchezo wa fainali ambayo shujaa wao, Mohamed Salah aliumizwa bega na Sergio Ramos.

Kwa msimu huu hadi mzunguko wa kwanza unamalizika Liver inaongoza kundi C ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Napoli pointi tano na PSG ina pointi nne, zote zina nafasi ya kutinga hatua ya mtoano kama itashinda mechi zote za mzunguko wa pili.

 

ADVERTISEMENT