In Summary
  • Meneja wa Mkomola, Alfred Amede anayeishi Zanzibar, amefunguka mchongo mzima ulivyokuwa mpaka kijana huyo akatua Ukraine.

USAJILI wa mshambuliaji Yohana Mkomola katika klabu ya Arsenal Kiev ya Ukraine, uliwashtua wengi kwa vile si jambo jepesi kwa mchezaji kupata dili la moja kwa moja kutoka Bongo hadi Ulaya tena katika timu ya Ligi Kuu.

Bahati mbaya kwake ni kwamba mwisho wa msimu huu, timu hiyo imeshuka daraja baada ya kushika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ya Ukraine inayohusisha timu 12, huku Shakhtar Donetsk wakitwaa ubingwa wakifuatwa na Dynamo Kyiv katika nafasi ya pili.

Hata hivyo, hiyo bado haifuti ukubwa wa jambo lililofanywa na kinda huyo aliyeng’aa katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa chini umri wa miaka 17 akiitumikia Serengeti Boys ya Tanzania katika fainali zilizofanyika Gabon 2017.

Wakati Mbwana Samatta anayetamba Ulaya akiwa na klabu yake ya KRC Genk alipita njia ndefu kabla ya kufika Ulaya baada ya kuanzia Simba ya Tanzania, TP Mazembe ya DR Congo na kisha ndiyo kutua Ubelgiji, Mkomola ameenda moja kwa moja kwenye Ligi Kuu Ulaya akitokea Ligi Kuu ya Biongo aliyocheza msimu mmoja tu.

Meneja wa Mkomola, Alfred Amede anayeishi Zanzibar, amefunguka mchongo mzima ulivyokuwa mpaka kijana huyo akatua Ukraine.

KAKA AMPA ULAJI

Kweli damu ni nzito kuliko maji, hiyo ni baada ya Samuel Mkomola ambaye ni kaka wa Yohana kuamua kumkutanisha na Alfred ili aweze kupata dili la nje.

Amede anasema Samuel alimueleza kwamba mdogo wake umefika muda wa kwenda nje ya nchi na haikumchukua muda mrefu kabla ya kukamilisha dili hilo.

“Mimi mwenyewe ujue nimecheza mpira na kaka zake, lakini baadaye niliamua kuachana nao na kusoma nje na ndipo nikaanza kutengeneza njia za soka na baadhi ya watu.”

Anaongeza: “Kwa Mkomola ilikuwa jambo la kawaida kwenda kwasababu nilianza kutuma video zake mapema mno kabla hajasaini Yanga lakini timu za Ulaya zilikuwa hazina imani naye mwanzoni.”

YANGA ILIMCHELEWESHA

Kumbe mchongo wa Mkomola kwenda nje ulianza mapema tu baada ya kutua Yanga lakini timu za Ulaya zilikuwa zinaogopa kuvunja mkataba kwasababu ulikuwa mpya.

Amede anasema mchezaji huyo kilichokuwa kinambeba ni uwezo wake wa kupambana na mabeki ambao aliouonyesha kupitia Afcon U-17 ya Gabon lakini pia kucheza Mashindano ya Caf akiwa na Yanga.

“Timu zillizoonyesha nia zilikuwa ni nyingi, lakini ilikuwa ngumu kwasababu alikuwa na mkataba mpya,” anasema wakala huyo.

Anaiongeza hata katika dirisha dogo la usajili alipata timu ya kwenda kufanya majaribio lakini bado ilikuwa ngumu kutokana na Yanga kuendelea kuwa naye kabla ya kumtoa kwa mkopo African Lyon.

STRESS ZAMPA AKILI

Baadaya kutolewa kwa mkopo kwenda African Lyon, Mkomola akili yake ilikuwa haijatulia katika timu hiyo na mara kwa mara alikuwa akikacha mazoezi na hata mechi na hivyo kufanya mazoezi yake peke yake.

Meneja wake anafichua kwamba baada ya kugundua hilo ilibidi amchukue na kumpeleka Zanzibar kwaajili ya kumuweka sawa kwa upande wa akili.

“Unajua huyu ni kijana mdogo sana, kwahiyo anapokuwa na mawazo inabidi ujue namna ya kumuweka sawa. Nilimchukua na kumleta Zanzibar nikawa namsimamia mwenyewe mazoezi muda wote, nakumbuka ilikuwa Februari,” anasema.

Anaongeza alipokuwa Zanzibar ndipo akamdokeza kwamba amepata timu mbili za kwenda kufanya majaribio nchini Ukraine hivyo ni muda sahihi kwake kujifua kwa nguvu zote kabla hajasafiri.

VISA NUSURA IHARIBU

Amede anafichua kwamba kuna wakati Mkomola alipotea ghafla katika kikosi cha Lyon lakini kumbe mchezaji huyo aliondoka kimya kimya na kwenda nchini Kenya kutafuta Visa ya Ukraine.

“Haikuwa safari nyepesi kwa Mkomola kwasababu tulienda kama mara tatu Kenya. Nakumbuka ya kwanza tulienda pamoja kwa ndege wakati tukiwa na mualiko wa timu ya kwanza (jina kapuni) lakini tulirudi nchini bila mafanikio.”

“Mara ya pili akaenda yeye peke yake, lakini kulikuwa na usumbufu kidogo kwasababu ikawa ni timu ya pili imemtumia mualiko nayo kwahiyo walimsumbua na hakufanikiwa kupata visa, kitu hicho kilimchanganya sana.”

Aliongeza mara ya tatu ilibidi waondoke wote wawili lakini ukata ukawa umewatembelea hivyo walitumia usafiri wa gari kuelekea nchini Kenya na haikuwa rahisi kufika.

“Mara zote alikuwa anaenda na ndege lakini safari ya tatu kidogo pochi haikuwa vizuri kwahiyo ilibidi tutumie usafiri wa gari, tulienda wote ili kuelewesha kidogo jinsi ambavyo ilikuwa mpaka mchezaji kupokea mialiko mitatu, kikubwa nashukuru Mungu tulifanikiwa kupata Visa,” anasema.

AFAULU KIULAIINI

Baada ya kufanikiwa kupata Visa na kutimkia nchini Ukraine kimya kimya, Amede anafichua kwamba mchezaji wake alifaulu kabla ya muda wa majaribio aliopangiwa kumalizika.

“Mkomola alipewa wiki tatu za kufanya majaribio na Arsenal Kiev, lakini kikubwa cha kumshukuru Mungu ni kwamba majaribio yake hayakuwa marefu kwani alionyesha uwezo na wakaridhika naye,” alisema.

Aliongeza kwamba licha ya kwamba ligi ya huko ilikuwa inaendelea, uongozi wa Arsenal Kiev uliamua kumbakisha mchezaji huyo ili kuwa katika mikono salama.

“Unajua wenzetu wapo makini kwa kile ambacho wanakifanya, waliona bora aendelee kubaki kule kuliko kurejea nchini kwahiyo kijana yupo na anafanya mazoezi pamoja na timu yao ya pili, lakini amesajiliwa kwa upande wa wakubwa,”.

NDOA NA YANGA

Wengi wamekuwa wakijiuliza Mkomola amewezaje kusaini mkataba na Arsenal Kiev huku akiwa na mkataba na Yanga, lakini meneja wake Amede akishirikiana na mwenzake Johnson Pallangyo waliweza kuzungumza na viongozi wa Yanga na kukubaliana pande hizo kuvunjiana mkataba.

“Kiukweli Yanga haikuwa na faida na Mkomola kwasababu alikuwa hachezi, kwahiyo tuliomba wamuachie na wao kwa wema wakaona hawana kazi naye basi wakamuachia, hivyo mkataba ukavunjwa kwa makubaliano ya pande mbili,” anasema.

MKWANJA VIPI UTURUKI

Licha ya kusaini timu kubwa nchini Uturuki, mashabiki na wadau wengi wa soka nchini walikuwa wakisubiri kuona mchezaji huyo kasajiliwa kwa bei gani kwani kuingia katika timu ya Ligi Kuu Ulaya lazima mpunga wa maana utoke.

Hata hivyo, amesema mchezaji huyo alijiunga na Arsenal Kiev kama mchezaji huru kwahiyo masula ya kimaslahi anawaachia familia yake kwa ujumla.

“Makubaliano ya kimaslahi namuachia yeye na familia yake, lakini watu wanabidi wakumbuke kwamba Yohana anahitaji kuendelezwa kidogo na mpira wetu na kule ni tofauti sana,’’.

Anaongeza anabidi aachwe akomae hata kwa msimu mmoja na baada ya hapo ndiyo waanze kuangalia kuhusu masuala ya pesa kutokana na umri wake bado kuwa mdogo.

WACHEZAJI WENGINE

Amede ameliambia Mwanaspoti kwamba Mkomola ni mmoja tu wa wachezaji walio chini ya menejimenti yake.

“Mimi na Pallangyo tulisoma Russia kwahiyo tulitengeneza mawasiliano mazuri na watu wa Ulaya. Kuna mchezaji Simba alitumiwa mpaka tiketi lakini cha ajabu jamaa hakwenda, vitu hivi havipendezi” anasema wakala huyo kuhusu wachezaji wengine anaowapa dili.

ADVERTISEMENT