In Summary

Monaco aliibukia kwenye timu B mwaka 2015, lakini kwa haraka sana ilipofika Desemba akapandishwa kwenye kikosi cha kwanza wakati alipotokea benchi kwenye mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Caen, ambapo alicheza sambamba na wakali Bernardo Silva na Fabinho.

PARIS, UFARANSA . KYLIAN Mbappe ni Desemba tu hapo aliondoka kwenye miaka ya utoto, lakini akiwa amecheza mechi 180 huku akiwa tayari ameshatupia wavuni mabao 100 katika maisha yake.

Straika huyo Mfaransa alifunga bao lake la 100 Jumanne iliyopita, akiwa na umri wa miaka 20 na siku 173, wakati alipofunga bao la kwanza kwenye ushindi wa 4-0 iliyopata Ufaransa dhidi ya Andorra kwenye kufuzu Euro 2020.

Mbappe amefikisha mabao hayo 100 kwa haraka sana ikiwa ni miaka mitatu na nusu tu tangu alipoingia kwenye soka, huku akiwagalagaza Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kwenye kutupia.

Mbappe, 20, alianzia kung’ara akiwa AS Bondy na licha ya kuzivutia klabu kibao kama Chelsea, Liverpool na Real Madrid aliamua kwenda zake AS Monaco kukuza kipaji chake.

Monaco aliibukia kwenye timu B mwaka 2015, lakini kwa haraka sana ilipofika Desemba akapandishwa kwenye kikosi cha kwanza wakati alipotokea benchi kwenye mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Caen, ambapo alicheza sambamba na wakali Bernardo Silva na Fabinho.

Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 16 tu. Mbappe alifunga bao lake la kwanza kwenye soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 17 na siku 62, Februari 20 - ambayo ilikuwa mechi yake ya saba kwenye soka la kulipwa. Alitokea benchi na kufunga katika dakika za majeruhi, akifunga kwa mguu wa kushoto kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Troyes. Tangu hapo, Mbappe hakurudi nyuma.

Msimu wa 2016/17, Mbappe alionyesha ubora wake, ambapo alifunga mabao 26 na kuwasaidia Monaco kushinda ubingwa wa Ligue 1 na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbappe alipiga hat-trick yake ya kwanza Desemba 2016 kwenye ushindi wa 7-0, wakati AS Monaco ilipoichapa Stade Rennais na kupiga tatu nyingine kwenye ligi miezi mitatu baadaye. Etihad siku zote utakuwa na kumbukumbu tamu kwa Mbappe, kwamba ndiko alikofunga bao lake la kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati alipoweka kambani kwenye kichapo cha 5-3 kutoka kwa Manchester City. Mbappe alifunga tena kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Man City, kisha akapiga tatu kwenye robo fainali dhidi ya Borussia Dortmund na moja kwenye nusu fainali dhidi ya Juventus, ambao ndio ulikuwa mwisho wa Monaco kwenye michuano hiyo msimu huo.

Kisha akahamia kwa mkopo Paris Saint-Germain, ambao baadaye ilimbeba jumla kwa ada ya Pauni 162 milioni mwaka uliofuatia, lakini ni baada ya kuwafurahisha sana, akifunga mabao 21 na kufanikiwa kubeba ubingwa wake wa pili wa Ligue 1 akiwa na umri wa miaka 19 tu.

Ilimchukua mechi saba kufunga bao lake la kwanza huko kwenye kikosi cha Monaco, lakini Mbappe alihitaji mechi tano tu kufunga bao la kwanza kwenye Timu ya Taifa ya Ufaransa, hiyo ilikuwa wakati ilipoichapa Uholanzi 4-0. Hiyo ilikuwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2018.

Mabao yake manne, yakiwamo mawili dhidi ya Argentina na moja kwenye fainali, yalitosha kuifanya Ufaransa kubeba ubingwa wa dunia katika fainali hizo zilizofanyika Russia.

Haikushangaza kuchaguliwa kuwa kinda bora kwenye fainali hizo na alichaguliwa katika kikosi cha kwanza cha michuano hiyo, World Cup Dream Team.

Wakidhani kwamba Mbappe atakuwa amechoshwa na Kombe la Dunia, Mbappe alianza kwa kasi akifunga mabao 15 katika mechi 15 za mwanzo, kabla ya kumaliza msimu akiwa na mabao 39, huku 33 akiwa amefunga katika mechi 29 alizocheza kwenye Ligue 1 na ndio maana kwa sasa anasakwa na wababe kama Real Madrid.

Kuhusu mabao 100, Aguero alifikisha idadi hiyo akiwa na umri wa miaka 21 na siku 285, akiwa amemzidi Mbappe kwa siku 477. Wayne Rooney alifikisha akiwa na umri wa miaka 22 na siku 87, wakati Messi alihitaji siku kumi zaidi kutoka kwenye umri huo wa Rooney kufikisha idadi hiyo. Messi alifunga bao lake la 100, Septemba 2009 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dynamo Kiev.

Ronaldo alipokuwa na umri wa miaka 20 na siku 173, kipindi hicho alikuwa akijiandaa na msimu wake wa tatu Manchester United, huku akiwa amefunga mabao 20 kwenye soka la klabu na tisa kwa Timu ya Taifa ya Ureno.

Ronaldo alifikisha mabao 100 akiwa na umri wa miaka 23 na hiyo ilikuwa kwenye Kombe la FA dhidi ya Tottenham, Januari 27, wakati alipofunga mbili uwanjani Old Trafford na timu kutinga raundi ya tano.

ADVERTISEMENT