In Summary

Picha hiyo inamwonyesha Hazard akiwa kibonge, huku wengine wakiamini kwamba picha imechezewa kabla ya kupostiwa kwenye ukurasa wa Twitter wa klabu hiyo, kwa sababu huo si mwonekano halisi wa supastaa huyo wa Kibelgiji

MADRID, HISPANIA. Mashabiki wa Real Madrid wamemshutumu staa wao mpya Eden Hazard kwa kuwa kibonge katika kipindi hiki cha mapumziko ya majira ya kiangazi.

Mashabiki hao wa Los Blancos waliamua kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuelezea mwonekano wa Hazard baada ya picha yake aliyopigwa akiwa na jezi za mazoezi za timu hiyo zilizotumwa kwenye mtandao wa klabu kuzua mjadala.

Picha hiyo inamwonyesha Hazard akiwa kibonge, huku wengine wakiamini kwamba picha imechezewa kabla ya kupostiwa kwenye ukurasa wa Twitter wa klabu hiyo, kwa sababu huo si mwonekano halisi wa supastaa huyo wa Kibelgiji. Kuna wanaoamini kwamba huenda picha imehaririwa kwa maana ya kuchukulia kichwa cha Hazard na kuwekwa kwenye mwili wa Karim Benzema maana si kwa mwonekano wa mchezaji huyo.

Shabiki mmoja wa Los Blancos aliandika: “Ni kweli tumelipa 1oo milioni kwa Hazard kibonge.”

Mwingine aliandika: “Hivi imekuwaje, Hazard akawa kibonge hivi ndani ya mwezi mmoja tu??? Duh hayo ni maajabu.”

Mwingine alisema: “Ni macho yangu au Madrid wamemsajili kibonge Hazard?”

Lakini, staa huyo alidaiwa kutaniwa na wenzake tangu alipokuwa Chelsea, wakimwambia anakitambi wakati alipovua jezi walipokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia kushangilia ubingwa wa Europa League.

Kuna shabiki mmoja alisema: “Hakika mimi inanishangaza sana hivi huyu kibonge Hazard anawezaje kubaki kuwa mmoja wa wachezaji watano bora duniani. Hivi angekuwa mwembamba kidogo na misuli shupavu angekuwaje.”

Picha za hivi karibuni zimekuwa zikimwonyesha Hazard kuwa kibonge, huku mastaa wenzake wa zamani huko Stamford Bridge, Gonzalo Higuain na David Luiz waliwahi kumwambia winga huyo kuwa ana kitambi baada ya mechi yao ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Arsenal katika fainali ya Europa League, Mei mwaka huu.

ADVERTISEMENT