In Summary
  • Kwa sasa Stars inaendelea na kambi ya maandalizi kuelekea fainali hizo ambayo ipo jijini Cairo.

IDADI ya tiketi 30,000 imepangwa kuuzwa kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki baina ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Misri ikiwa ni maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini humo kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Mechi hiyo itachezwa keshokutwa Alhamisi Uwanja wa Borg El-Arab uliopo jijini Alexandria ukiwa ni wa kwanza kwa Stars iliyopo kambini nchini humo, kujipima nguvu huku wa pili ukiwa ni ule dhidi ya Zimbabwe, Juni 16.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chama cha Soka Misri (EFA), idadi ya mashabiki 30,000 tu ndio wanaruhusiwa kutazama mchezo huo na tiketi hizo zitauzwa katika vituo vitatu tofauti ambavyo ni Olympic Club, El-Teram SC na Uwanja wa ndege wa Borg El-Arab

Mchezo huo ambao utachezwa saa 3 usiku, utachezeshwa na marefa wote kutoka nchini humo na mwamuzi wa kati atakuwa ni Mohamed Adel atakayesaidiana na mwamuzi msaidizi namba moja, Samir Gamal na refa msaidizi namba mbili Youssef El-Bossaty.

Bei ya tiketi kwenye mchezo huo itakuwa ni Pauni za Misri 30 (Sh4,200) kwa mashabiki watakaokaa jukwaa la kawaida wakati wale watakaoketi jukwaa kuu watalipa Pauni 100 (Sh13,750).

Kwa sasa Stars inaendelea na kambi ya maandalizi kuelekea fainali hizo ambayo ipo jijini Cairo.

Kwenye fainali hizo, Stars imepangwa kundi C sambamba na timu za Algeria, Senegal na Kenya wakati wenyeji Misri wapo kundi A pamoja na timu za Uganda, Zimbabwe na DR Congo.

ADVERTISEMENT