In Summary

 

  • Marsh Queens itakuwa ugenini kuwakabili Yanga Princess katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake utakaopigwa kwenye uwanja wa Karume Dar es Salaam

MWANZA. KOCHA wa Marsh Queens,Godfrey Chapa amesema kuwa mapungufu yaliyoonekana kwenye mechi iliyopita na kusababisha kukosa pointi tatu, ameyafanyia kazi hivyo leo Alhamisi Yanga princess wasitegemee mteremko.

Marsh Queens ambao walianza mzunguko wa pili kwa sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Baobab Queens wanawakabili Yanga Princess iliyotoka kupata ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Sisterz FC.

Kocha Chapa alisema kuwa mchezo uliopita mabeki wake ndio walikosa umakini,lakini kwa sasa benchi la ufundi limekaa na kuyafanyia kazi mapungufu hayo,hivyo leo pointi tatu ni muhimu dhidi ya wapinzani hao.

Alisema kuwa vijana wake wana ari na morari nzuri na wameahidi kusahihisha makosa yao ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao kuhakikisha wanavuna ushindi.

“Hatukufurahia matokeo ya mechi iliyopita,lakini tulibaini mapungufu na tumeweza kuyafanyia kazi kwahiyo kesho (leo) tunaamini ushindi utakuwepo,vijana wameahidi kufanya kweli,” alisema Chapa.

Kocha huyo aliongeza kuwa anaamini wapinzani wao wamejiandaa kuonyesha ushindani na kuendeleza ushindi kwenye uwanja wao,lakini ameandaa mbinu ambazo zitawamaliza mapema.

Aliweka wazi kuwa mchezo wa leo ni wa kusaka ushindi,hivyo watacheza kwa mashambulizi kuhakikisha wanafikia malengo yao na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake.

“Tunajua tunaenda kupambana na timu nzuri iliyotoka kupata ushindi,lakini na sisi tuna mbinu zetu tutakazotumia kupata tunachotaka,tutashambulia mwanzo mwisho,”alisema Kocha huyo.

 

ADVERTISEMENT