In Summary
  • Liverpool juzi Jumnanne ilichapwa mabao 2-0 na vibonde wa kundi lao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Red Star Belgrade ya Serbia na kuifanya timu hiyo kukusanya pointi nne huku Liver ikibaki na sita sawa na Monaco iliyotoka sare ya bao 1-1 na PSG.
  • Msimu uliopita timu hiyo chini ya Kocha, Jurgen Klopp ilitinga hadi fainali na kuambulia kichapo cha maboa 3-1 dhidi ya Real Madrid.

BELGRAD,SERBIA.WAKUBWA wakisema tuwasikilize. Liverpool juzi Jumanne ilichapwa mabao 2-0 na vibonde wa kundi lao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Red Star Belgrade ya Serbia na sasa mastaa wawili wa zamani wa England wamesema ‘Liverpool ijiangalie’.

Mabao mawili ya Milan Pavkov katika dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza yalitosha kupeleka msiba Anfield ikiwa ni siku chache baada ya wababe hao wa Merseyside kukimbizwa na Arsenal katika pambano la Ligi Kuu England Jumamosi jioni ya wiki iliyopita.

Steve McManaman, staa wa zamani wa Liverpool pamoja na nyota mwingine wa zamani wa England, Tim Sherwood aliyetamba na Tottenham wameiweka Liverpool katika mstari mwekundu na kuipa tahadhari kubwa katika mechi mbili zinazofuata.

Liverpool wana pointi sita wakiwa wanashika nafasi ya pili lakini wana mechi mbili ngumu dhidi ya PSG ugenini na kisha dhidi ya Napoli nyumbani. Hata hivyo McManaman ametoa neno la tahadhari kwa wababe hao waliofika fainali msimu uliopita.

“Wanapata wakati mgumu wakicheza nyumbani kwa PSG kwa sasa, maana wapinzani hao wanacheza vizuri wakiwa nyumbani, kwa kuangalia matokeo ya leo (juzi) itakuwa ngumu kama Liverpool itakwenda katika pambano lake la mwisho dhidi ya Napoli namna hii ili ipate ushindi kwa sababu Waitaliano wanajua kujihami. Wamejiweka katika nafasi ngumu sana.” Alisema staa huyo ambaye aliwahi kuchukua ubingwa wa Ulaya na Madrid.

Kwa upande wa Sherwood alidai kwamba kichapo cha Liverpool ni angalizo kwa kikosi hicho kinachoongozwa na kocha Mjerumani, Jurgen Klopp ingawa bado wanaweza kujiamini na kusonga mbele.

“Ni angalizo kwao. Lakini bado wapo katika michuano, sawa, wana mechi mbili ngumu zinakuja lakini inabidi waamini kwamba wanaweza kupita. Ilikuwa rahisi kwao (kufuzu Ligi ya mabingwa msimu uliopita). Angalia mabao mangapi walifunga katika michuano msimu uliopita, walikuwa wanafunga kwa kujisikia. Walianza hivi hivi katika hatua ya mwanzo, kwa hiyo wanajiamini watapita.” Alisema Sherwood.

“Bado wanajiamini, wana kile kitu cha kujisikia miongoni mwao kwamba wanaweza kwenda katika hatua inayofuata na kushinda michuano hii, wana haki hiyo kwa sababu walifika fainali katika msimu uliopita.”

Kiungo wa Liverpool, James Milner alikiri kwamba kipigo hiko kimeiacha timu yao ikiwa katika nafasi ngumu ya kufuzu lakini akawa na uhakika kutokana na uwezo walionao bado wana uwezo wa kushinda mechi mbili zilizobaki.

“Inabidi twende na kushinda mechi zetu zilizobaki. Kama habari ni hiyo tu na hilo lipo katika nguvu zetu basi inabidi tuonyeshe ukubwa wetu na kufanya hivyo. Tunajua tunaweza kuzifunga timu zote mbili. Wote wawili ni wazuri lakini kwa sasa ni juu yetu kuonyesha tuna timu nzuri na ni wazi tutacheza vizuri kuliko tulivyofanya dhidi ya Belgrade.” Alisema Milner

Kipigo cha Liverpool juzi kilikuwa cha tatu mfululizo ugenini katika michuano ya Ligi ya mabingwa Ulaya ukiwa ni mwanzo mbovu zaidi kwao katika michuano ya Ulaya tangu mwaka 1979.

Katika pambano hilo kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alijaribu kubadilisha kikosi chake kutoka katika kile ambacho kilicheza na Arsenal kwa kujaribu kuwaanzisha Joel Matip, Adam Lallana na Daniel Sturridge lakini hata hivyo mambo yalikuwa magumu kwa Liverpool ambayo iliruhusu mabao mawili ndani ya dakika 25 za mwanzo za pambano hilo na kuwaweka kwenye hali ngumu kwenye mchezo ambao ilipaswa kushinda.

ADVERTISEMENT