In Summary
  • Macho ya mashabiki na wadau wa soka yanawatazama mastaa hiyo kuona kama watazisaidia timu hizo kucheza Ligi Kuu.

MWANZA. LIGI Daraja la Kwanza inaendelea kushika kasi, huku ushindani ukiwa mkali kwa timu zote kutafuta tiketi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao ili kuungana na Simba na Yanga.

Hadi sasa timu hizo tayari zimeshacheza mechi 16 katika makundi yote mawili katika Kundi A Namungo ikiongoza ikiwa na pointi 34 ikifuatiwa Mbeya Kwanza yenye alama 28. Katika kundi hilo, Dar City yenye alama tisa iko mkiani.

Katika Kundi B, vigogo Geita Gold FC chini ya Kocha Hassan Banyai ndio vinara wakiwa na alama 33 huku Polisi Tanzania chini ya Mbwana Makata ikiwa na pointi 29 na Mgambo Shooting ikiburuza kwa alama tisa.

Pamoja na vita ya kuwania kupanda Ligi Kuu kwa timu hizo, kazi kubwa ipo kwa wakongwe ambao kila moja inasaka heshima kuiwezesha klabu yake kufikia ndoto na kukwepa lawama mwisho wa ligi.

Ligi hiyo imeonekana kuwa na wachezaji wengi wakongwe waliozichezea Simba na Yanga kwa vipindi vya nyuma.

Macho ya mashabiki na wadau wa soka yanawatazama mastaa hiyo kuona kama watazisaidia timu hizo kucheza Ligi Kuu.

Salum Machaku – Rhino Rangers

Winga huyu ambaye aliwahi kutamba na ‘Wekundu wa Msimbazi’ ndiye anayeongoza safu ya ushambuliaji kwenye kikosi cha Rhino Rangers ya mkoani Tabora.

Machaku hadi sasa ameshafunga mabao mawili na kuifanya klabu hiyo kuwa na pointi 21 katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo na nyota huyo amekuwa katika wakati mgumu kuonyesha uzoefu wake wa kuipandisha daraja timu hiyo.

Moja ya mkakati wa timu hiyo yenye maskani yake Tabora kumshusha klabuni hapo mkongwe huyo ni kuwahamasisha nyota chipukizi kupambana kuipandisha Ligi Kuu.

Zahoro Pazi –Arusha United

Mmoja kati ya usajili uliotikisa medani za soka nchini ulikuwa ni ule uliofanywa na Arusha United kumpa kandarasi kiungo huyu kuitumikia kwa nia ya kuipandisha Ligi Kuu.

Pazi ambaye aliwahi kuichezea Simba na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa sasa ndiye mchezaji mkongwe kwenye kikosi hicho cha jijini Arusha akipambana na wenzake kuipandisha Ligi Kuu.

Hadi sasa kiungo huyo mtoto wa kipa mkongwe wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi ameshaifungia timu yake mabao matatu na kuiweka kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28.

Hata hivyo, bado presha ya kupanda Ligi Kuu inaendelea kuwa juu kutokana na mashabiki wa Arachuga kusubiri kuona kama makeke ya nyota huyo yataisaidia.

Mbali na Pazi, wakongwe wengine waliomo kwenye kikosi hicho ni Abdulhalim Humoud na Gaudence Mwaikimba ambao wana uzoefu mkubwa kwenye soka na waliwahi kucheza timu kubwa.

Humoud aliyetimuliwa na Klabu ya Ligi Kuu ya KMC kwa madai ya utovu wa nidhamu, aliwahi pia kuzitumikia Simba, Coastal Union na Mtibwa Sugar na sasa anatesa na Arusha United.

Naye anaingia kwenye mtego wa kukubali kusifiwa au kukebehiwa mwishoni mwa msimu huu.

Kwa upande wake Mwaikimba ambaye aliwahi kukipiga Yanga Azam FC na Taifa Stars hatakuwa na la kujitetea pale Arusha United itakaposhindwa kuzipeleka Simba na Yanga mkoani Arusha msimu ujao.

Kudra Omary – Dar City

Nyota huyu wa zamani wa Yanga ana wakati mgumu katika kuhakikisha anainusuru timu yake kutoshuka daraja baada ya mipango ya kupanda Ligi Kuu kwenda mrama.

Omary ambaye aliitumikia Yanga mwaka 2001-06 bado hajafunga bao lolote na klabu yake na ndiyo inayoburuza mkia kwenye Kundi B ikiwa na pointi tisa na inapambana kukwepa rungu la kucheza Ligi Daraja la Pili.

Ni wazi benchi la ufundi na mashabiki wa Dar City wanamuangalia zaidi mkongwe huyo kuona kama atatumia uzoefu wake kwenye soka kuibakiza.

Hata hivyo, katika mazungumzo maalumu na Mwanaspoti, Omary alisema kwa sasa hali si shwari klabuni kwao na wanapambana kukwepa janga la kushuka daraja.

“Ni kweli matokeo si mazuri lakini binafsi nitawahamasisha wenzangu kupambana na kutokata tamaa kuhakikisha tunabaki Ligi Daraja la Kwanza,”alisema Omary.

Shija Mkina – Pamba FC

Pengine aliocheza nao miaka hiyo kwenye kikosi cha Simba huenda wakisikia sauti ya straika huyu watashika midomo kwani bado anatesa kwenye soka na sasa hivi ndiye anayeiongoza Pamba FC ‘TP Lindanda’ ya Mwanza.

Mkina ambaye tayari ameshafunga mabao mawili kwenye kikosi hicho na kuisaidia kuwa nafasi ya nne kwa pointi 26 anaendelea kuipigania timu hiyo kupanda Ligi Kuu.

Mkina ambaye aliwahi kuliambia Mwanaspoti anafurahia maisha ndani ya Pamba, amekuwa na msaada mkubwa kwani licha ya kutofunga mabao, ameweza kusaidia upatikanaji wake ‘assist’.

Pia, mkongwe huyu amekuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi cha TP Lindanda na ndiye kivutio kwenye kikosi hicho kinapokuwa uwanjani wengi humtazama yeye. Hata mabeki wa timu pinzani hujitahidi kumlinda ili asilete madhara.

Ni dhahiri Pamba ikipanda Ligi Kuu msimu ujao au ikikwama, Mkina atakuwa miongoni mwa wachezaji watakanyooshewa vidole kutokana na matokeo hayo.

Nassor Masoud ‘Chollo’ – Dodoma FC

Beki huyu ambaye aliwahi kuitumikia Simba miaka minne iliyopita, kwa sasa bado anatesa na Dodoma FC sambamba na wakongwe wengine katika kuipandisha timu hiyo ya Makao makuu ya nchi.

Chollo na wenzake watakuwa na maelezo iwapo watashindwa kuipeleka Ligi Kuu msimu ujao baada ya kusota kwa msimu wa pili mfululizo na tayari uongozi umeshaachana na aliyekuwa kocha wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

ADVERTISEMENT