In Summary

Yanga ina pointi 50, Azma wao wamekusanya pointi 40 mbapo Simba wana pointi 33 lakini lengo lao ni kutetea ubingwa huo, kazi kubwa ipo kwenye umaliziaji wa mechi za mzunguko wa lala salama ambao utaanza hivi karibuni.

Baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara zimebaki mechi moja pekee kumaliza mzunguko wa kwanza.
Kuna timu tatu ambazo zinashika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi ikiongozwa na Yanga, Azam na mabingwa watetezi Simba.
Simba ndiyo timu pekee ambayo haijacheza mechi nyingi kutokana na majukumu waliyonayo kwani inashiriki michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa wameingia hatua ya makundi.
Yanga ina pointi 50, Azma wao wamekusanya pointi 40 mbapo Simba wana pointi 33 lakini lengo lao ni kutetea ubingwa huo, kazi kubwa ipo kwenye umaliziaji wa mechi za mzunguko wa lala salama ambao utaanza hivi karibuni.
Pointi walizoachana ni pointi nyingi kwa kuzihesabu lakini kwa kucheza ni pointi chache maana itategemea jinsi timu hivyo itakavyokuwa zinapata matokeo uwanjani.
Misimu yote mzunguko wa lala salama unakuwa kama vita kubwa, haki huwa haitendeki ipasavyo kwa baadhi ya timu kwani hutokea malalamiko mengi sana upande wa baadhi ya timu kuonewa na waamuzi.
Huwa inaelezwa kwamba lala salama hata waamuzi hupoteza umakini wao kwa kuzibeba baadhi ya timu ili mradi tu zipate matokeo mazuri.
Ni hatua ambayo ni mbaya kwa timu zisizokuwa na uwezo, hatua mbaya kwa wachezaji kutuhumiwa kuhujumu timu zao endapo tu matokeo yanakuwa mabaya kwao.
Kitu pekee ambacho kitasaidia kuepusha malalamiko kama hayo ni wachezaji, viongozi wa timu na waamuzi kuwa makini na kufuata sheria za soka.
Wachezaji wanapaswa kujituma uwanjani ili kuzipambania timu zao,  waamuzi wanatakiwa kufuata sheria 17 za soka huku viongozi wao wanapaswa kuwajibika katika majukumu yao ya kiongozi.
Kuepusha lawama na malalamiko ama kufungiwa kwa baadhi ya waamuzi kutokana na maamuzi yao ya hovyo yanayoonekana wazi kushindwa kuhimili mchezo husika kufuata sheria tu na si vinginevyo.
Mara nyingi timu zenye uwezo kupesa ndizo hutuhumiwa kuhujumu timu zenye uchumi mdogo kwa madai ya kuwarubuni wachezaji wao kucheza chini ya kiwango, jambo ambalo ni hatari kwa mchezaji na timu yenyewe.
Lala salama inapaswa kuwa karibu sana na Takukuru ili kuzuia mianya yote ya ukandamizaji na matumizi mabaya ya sheria za soka ikiwemo mpenyezo wa rushwa kwa wachezaji, waamuzi na kila mmoja anayehusika na soka.
Takukuru wakiwa karibu na soka kwenye hatua hii ni wazi bingwa atakayepatikana atakuwa ni bingwa wa kweli na si kubebwa kwa namna yoyote ile.
Ligi hivi sasa haina mdhamini, hivyo kupelekea kukosekana kwa mdhamini isiwe sababu ya kuwatumia kwenye mchezo mchafu wale ambao kipato chao ni cha chini ili kujinufaisha iwe kwa kutwaa ubingwa ama kushika nafasi bora za juu.
Ukata wa udhamini wa ligi utumike kama changamoto za timu kujituma na kuonyesha viwango vyao bila kubebwa na mtu kuliko kuonyesha wazi kwamba Simba, Yanga au Azam ni lazima wapate pointi tatu kutoka timu fulani kwasababu tu zina ukata.
Lala salama ichezwe kwa umakini na ushindani wa viwango vya uwanjani na sio ushindani wa nje ya uwanja.

ADVERTISEMENT