In Summary
  • Kwenye fainali za mwaka huu, baadhi ya rekodi hizo zinaweza kuvunjwa, kuboreshwa au kuwa ngumu kuvunjwa au kufikiwa. Mwanaspoti inakuletea dondoo juu ya rekodi hizo.

BADO siku nne tu kabla ya kipyenga kupulizwa kuashiria kuanza kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) huko Misri ambazo kwa mara ya kwanza zitashirikisha jumla ya nchi 24 zilizopangwa katika makundi sita.

Fainali za mwaka huu ni za 32 tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mnamo mwaka 1957 na Misri ndiyo bingwa wa kihistoria wa mashindano hayo ikiwa imetwaa taji mara saba ikifuatiwa na Cameroon ambayo imeibuka bingwa mara tano.

Katika awamu 31 zilizopita za mashindano hayo kumekuwa na rekodi mbalimbali ziizowekwa ama na nchi, wachezaji au makocha kwa nyakati tofauti.

Kwenye fainali za mwaka huu, baadhi ya rekodi hizo zinaweza kuvunjwa, kuboreshwa au kuwa ngumu kuvunjwa au kufikiwa. Mwanaspoti inakuletea dondoo juu ya rekodi hizo.

Umri mkubwa

Naby Yattara wa Guinea, Carlos Kameni (Cameroon), Jeremy Morel (Madagascar) na Aggrey Morris (Tanzania) ndiyo wachezaji wenye umri mkubwa zaidi katika fainali za AFCON mwaka huu wakiwa na miaka 35 kila mmoja.

Hiyo inamaanisha kuwa rekodi iliyowekwa kwenye fainali za mwaka 2017 na aliyekuwa kipa wa Misri, Essam El Hadary, itashindwa kuvunjika kwani yeye aliandika rekodi hiyo baada ya kucheza akiwa na umri wa miaka 44 na siku 21.

Umri mdogo

Kama ambavyo ilivyo ngumu kuvunja rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza AFCON ambayo iliwekwa na Hadary ndivyo ilivyo vigumu kwa mashindano ya AFCON mwaka huu kuvunja rekodi ya Shiva N’Zigou wa Gabon ambaye yeye ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushiriki mashindano hayo.

N’Zigou aliweka rekodi hiyo mwaka 2000 akiwa na umri wa miaka 16 na siku 93 kwenye fainali za mwaka 2000 zilizofanyika Afrika Kusini.

Wachezaji ambao wameweka rekodi ya kuwa na umri mdogo katika fainali za AFCON mwaka huu ni Marc Lamti (Tunisia), Edmar Ca (Benin), Mohammed Amissi (Burundi) na Rodrigo Kossi (Guinea-Bissau) ndiyo wachezaji wenye umri mdogo zaidi kwenye fainali hizi wakiwa na umri wa miaka 18

Ufungaji Bora

Kama kuna rekodi ambayo inaweza kuwa ngumu kuvunjwa kwenye Fainali za AFCON mwaka huu basi ni ile ya mfungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo kwani kundi kubwa la washambuliaji ambao majina yao yameorodheshwa kushirki fainali hizo mwaka huu wameachwa mbali na wale walio juu kwenye chati ya wachezaji waliopachika idadi kubwa ya mabao kwenye mashindano hayo.

Rekodi ya mchezaji aliyepachika idadi kubwa ya mabao kwenye mashindano hayo hadi sasa inashikiliwa na Samuel Eto’o ambaye amefunga jumla ya mabao 18 kwenye mashindano hayo akifuatiwa na Laurent Pokou wa Ivory Coast ambaye yeye amepachika mabao 14 na nafasi ya tatu inashikiliwa na Rashidi Yekini wa Nigeria aliyefumania nyavu mara 13.

Wachezaji ambao wana nafasi ya kuifikia rekodi hiyo ama kuivunja kwa sasa ni nyota wawili wa Ghana, Asamoah Gyan na Andre Ayew ambao kila mmoja amefunga mabao nane (8) na hivyo kila mmoja ili aifikie rekodi hiyo anapaswa kupachika mabao 10 na ili waifikie, jambo ambalo linaweza kuwa gumu kwao.

Renard ataula mkia?

Baada ya kumla ng’ombe mzima kwa kutwaa ubingwa wa AFCON akiwa na nchi mbili tofauti, kocha wa Morocco, Herve Renard amebakiza mkia ambao ni kufikia rekodi iliyowekwa na makocha Charles Gyamfi wa Ghana na Hassan Shehata wa Misri ambao ndiyo wanaoongoza kuwa makocha waliotwaa mara nyingi taji la AFCON ambapo kila mmoja amelichukua mara tatu.

Renard alibeba taji kwa mara ya kwanza mwaka 2012 akiwa na kikosi cha Zambia na miaka mitatu baadaye yaani 2015 aliiongoza Ivory Coast kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Renard pia anashikilia rekodi ya kocha pekee aliyetwaa taji la AFCON akiwa na mataifa mawili tofauti.

Ushiriki kwa wachezaji

Aliyewahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Misri, Ahmed Hassan na aliyekuwa nahodha wa Cameroon, Rigobert Song, ndiyo wachezaji wanaoshikilia rekodi za kushiriki idadi kubwa ya mashindano ya AFCON ambapo kila mmoja ameshiriki mara nane.

Wawili hao wameshiriki fainali za mwaka 1996, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008 na 2010.

Song na Hassan wanafuatiwa na Essam El-Hadary na Hossam Hassan (Misri), Siaka Tiene, Kolo Toure na Boubacar Barry (Ivory Coast), Geremi Njitap (Cameroon) na Seidou Keita wa Mali ambao kila mmoja ameshiriki fainali saba (7) za AFCON.

Asamoah awatisha Eto’o na Bwalya

Kama atafanikiwa kufunga bao kwenye fainali za mwaka huu, Asamoah Gyan atavunja rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga bao katika fainali nyingi za AFCON na kuwapiku Samuel Eto’o wa Cameroon na Kalusha Bwalya wa Zambia.

Gyan, Bwalya na Eto’o wamefunga bao katika fainali sita za AFCON hivyo kama Asamoah atafunga kwenye fainali za mwaka huu, atafanya hivyo kwa mara ya saba.

Nani kumpiku Mulamba?

Kadri miaka inavyozidi kusonga mbele, namba ya mabao inayofungwa na mfungaji bora wa mashindano hayo imekuwa ikipungua siku hadi siku. Inawezekana kuna sababu nyuma ya hilo lakini bado haitoshi kuwa utetezi.

Hata hivyo, rekodi ya upachikaji mabao kwenye fainali moja ya AFCON inashikiliwa na Ndaye Mulamba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambaye kwenye fainali za Mwaka 1974 alifunga jumla ya mabao tisa.

ADVERTISEMENT