In Summary

Katika ufunguzi wa fainali hizo, mashabiki wachache walijitokeza uwanjani na kufanya sherehe zisinoge kama ilivyotarajiwa na huenda hiyo imechangia waziri huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza ofa hiyo kwa mashabiki ambao sasa ni wao tu.

UKISIKIA ganda la ndizi ndilo hili buana, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza neema kwa mashabiki wa soka kuwa kuanzia leo, ni wao tu na miguu yao kwani hakutakuwa na kiingilio chochote kuzishuhudia fainali hizo za Afrika kwa Vijana U17.

Waziri Majaliwa, alitangaza jana wakati wa ufunguzi wa fainali hizo zinazofanyika Tanzania kwa mara ya kwanza na kusema kuanzia leo mashabiki wataingia bure kwenye mechi za fainali hizo.

“Sisi kama Serikali tunasema kuanzia kesho (leo) Jumatatu Watanzania wote wataingia bure uwanjani, Tanzania Oyee,” alimalizia kwa kusema hivyo.

Katika ufunguzi wa fainali hizo, mashabiki wachache walijitokeza uwanjani na kufanya sherehe zisinoge kama ilivyotarajiwa na huenda hiyo imechangia waziri huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza ofa hiyo kwa mashabiki ambao sasa ni wao tu.

Awali mechi za michuano hiyo ilipangwa kuanza saa 8 mchana na ile ya pili kupigwa saa 10 jioni lakini ikasogezwa kwa mechi ya kwanza kuanza saa 10 jioni na ile ya pili saa 1 usiku kwa madai ya kutoa nafasi mashabiki wengi kuhudhuria, lakini hali ilikuwa tofauti na matarajio ya wengi.

ADVERTISEMENT