In Summary

Minziro amewahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga amezinoa timu kadhaa za Ligi daraja la kwanza nchini.

Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza ni kwanini kocha Fred Minziro anapoipandisha timu, uongozi unampa mkono wa kwaheri na kutafuta kocha mwingine? Minziro anasema tatizo ni viongozi kumgeuka.

Minziro nyota wa zamani wa Yanga, amewahi kuzipandisha timu za Singida United na KMC zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, pia kuwa kocha msaidizi wa Yanga amezinoa timu kadhaa za Ligi daraja la kwanza nchini.

"Nimekuwa nikifanya kazi kwa moyo wangu wote pale ninapotafuta mafanikio ya kuipandisha timu na viongozi wananipa ahadi kem kem, lakini tunapofanikiwa wananigeuka na kuniona sifai," alisema kocha huyo.

Alisema hivi sasa sina timu, lakini mipango yake ni kufundisha Ligi Kuu, kama itashindikana ndipo atageukia timu za daraja la kwanza ikiwamo Stand United ambayo imeshuka daraja.

"Stand wamefanya mazungumzo na mimi na wanahitaji huduma yangu, lakini ndio hivyo, naweza kujito hadi tukapanda daraja nao wakaniacha, ndiyo sababu nimelazimika kuangalia kwanza timu za Ligi Kuu," alisema.

"Siyo kazi nyepesi kupandisha timu hadi iweze kucheza Ligi Kuu, ni kazi ngumu kweli kweli, sema baadhi ya viongozi uwa wanachukulia poa," alisema Minziro.

 

ADVERTISEMENT