In Summary
  • Mshahara huo wa Rashford utamfanya kulingana na straika moto kabisa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, anayelipwa pia kiwango kama hicho, lakini anaweza kumlipa Alexandre Lacezette mishahara yake ya wiki mbili kwa mshahara wake wa wiki moja tu.

MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER United wamejifungia chumbani na mawakala wa Marcus Rashford wakizungumza kuhusu dili jipya la kumfanya mchezaji huyo abaki Old Trafford kwa miaka mingi ijayo.

Kinachojadiliwa kikubwa ni kuhusu mshahara atakaolipwa mshambuliaji huyo ili akubali kusaini Man United na kubaki hapo Old Trafford asishawishike kwenda kwingineko anakotakiwa, hususan Hispania anakotakiwa na Real Madrid.

Man United imewaambia wasimamizi hao wa Rashford watamlipa staa huyo mkwanja wa Pauni 200,000 kwa wiki. Kwanza mshahara wake utakuwa Pauni 150,000 kwa wiki, lakini utaongezeka hadi kufika Pauni 200,000 kwa wiki.

Mkataba wa sasa wa staa huyo utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, hivyo mabosi wa Man United wanapambana mchana na usiku ili kumsainisha dili jipya asiondoke, huku wakiamini mshahara mkubwa ndio utakaomfanya abaki kwenye timu yao. Kwa kumlipa Pauni 200,000 kwa wiki jambo hilo litamfanya Rashford awe kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England.

Lakini dili hilo litamfanya Rashford mwenye umri wa miaka 21 kuwa na jeuri ya pesa, ambayo kimsingi atawatambia mastaa kibao waliopo kwenye ligi hiyo.

Kwa mshahara huo wa Rashford atakaolipwa, basi ataweza kumudu kulipa mshahara wa wiki wa mabeki wa kati wa Arsenal, Laurent Koscielny, anayelipwa Pauni 75,000 kwa wiki na Shkodran Mustafi anayelipwa Pauni 90,000 kwa wiki.

Mishahara ya mabeki hao muhimu huko Arsenal ikichanganywa kwa pamoja haifiki Pauni 200,000 kwa wiki, hivyo Rashford atakuwa na uwezo wa kuwalipa mastaa hao na chenji inabaki.

Mshahara huo wa Rashford utamfanya kulingana na straika moto kabisa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, anayelipwa pia kiwango kama hicho, lakini anaweza kumlipa Alexandre Lacezette mishahara yake ya wiki mbili kwa mshahara wake wa wiki moja tu.

Lacazette huko Arsenal kila wiki analipwa Pauni 100,000. Mshahara mpya wa Rashford utakuwa unaweza kumudu kulipa mishahara ya wengi tu kwenye Ligi ya England, wakiwamo Leroy Sane wa Manchester City anayelipwa Pauni 60,000 kwa wiki au David Silva, anayelipwa Pauni 160,000 kwa wiki na Bernardo Silva anayelipwa Pauni 120,000 kwa wiki kwenye kikosi hicho cha Etihad.

Kwenye kikosi cha Chelsea beki David Luiz mshahara wake kwa wiki ni Pauni 120,000, hivyo Rashford atamudu kumlipa na chenji inabaki, huku mastaa wengine ambao kinda huyo wa Kingereza atamudu kuwalipa kwa mshahara wake mpya na chenji zikibaki ni pamoja na Jorginho, Mateo Kovacic, Olivier Giroud, Antonio Rudiger, Pedro, ambao wote hao ni wakali wa kikosi cha kwanza huko Stamford Bridge.

Kwa umri wa Rashford na mshahara anaokwenda kulipwa hakika unamfanya kuwa mtu mwenye jeuri kubwa uwanjani na kuwafunika mastaa wengine kibao wanaocheza soka la maana kabisa kwenye Ligi Kuu England.

ADVERTISEMENT