In Summary
  • Gipco inajitupa uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo uliopita ikiwa ugenini bao 1-0 dhidi ya Milambo,huku Kasulu Red Star wakipoteza nyumbani mbele ya Kumuyange mabao 2-0.

Kasulu Red Star imeiangalia kwa umakini Gipco FC mwenendo wake kwenye Ligi Daraja la Pili na kutamka mchezo wao wa Jumamosi wapinzani hao wajipange kwa kichapo cha nguvu.

Gipco imekuwa na matokeo mazuri na wanaongoza kundi lao B kwa pointi saba wiki hii itakuwa ugenini kucheza na Kasulu Red Star mchezo utakaopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Meneja wa klabu hiyo, Mfungo Bitta alisema wapinzani wao wana ushindani mkali ambao unawapa matokeo mazuri lakini wamejipanga kushinda mchezo huo na kuwapunguza kasi.

Alisema kwa sasa wanaendelea kujiweka fiti ili kuhakikisha wanawakalisha vinara hao wa kundi, kwani malengo yao ni kumaliza katika nafasi nzuri.

“Tunaamini mchezo utakuwa mgumu kutokana na kasi ya wapinzani wetu waliyoanza nayo lakini tumejipanga kuwatuliza kwa mara ya kwanza kuhakikisha tunashinda na kujiweka nafasi nzuri,” alisema Bitta.

Meneja huyo aliongeza vijana wao wote wana ari na morali nzuri na kutamba makosa waliyoyafanya mechi iliyopita dhidi ya Kumuyange watayafanyia kazi ili wasipoteze tena.

“Ni kweli tulipoteza tukiwa nyumbani lakini ni makosa madogo ambayo tuliyafanya kwa hiyo tunaenda kuwakabili wapinzani kwa umakini ili tusipoteze tena,” alisema.

ADVERTISEMENT