In Summary
  • Ndege aina ya Boeing 737-Max 8 iliyopata ajali ilikuwa ni ndege mpya, iliyokabidhiwa kwa shirika la ndege la Ethiopia Julai mwaka jana.

Nairobi, Kenya. Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kenya (KFF), Hussein Swaleh ni miongoni mwa watu 157 waliofariki dunia katika ajali ya ndege ye Ethiopia iliyokuwa ikitokea Addis Ababa kwenda Nairobi, Kenya.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka KFF, Swaleh alikuwa anarejea Kenya akitokea Cairo, Misri alipokuwa amekwenda kusimamia mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu ya Ismailia na TP Mazembe ya DR Congo. Swaleh alikuwa kamishna wa mechi hiyo.

Ndege aina ya Boeing 737-Max 8 iliyopata ajali ilikuwa ni ndege mpya, iliyokabidhiwa kwa shirika la ndege la Ethiopia Julai mwaka jana.

Wakati ikipata ajali ndege hiyo iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi wanane. Ilikuwa ikitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole Addis Ababa. Chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana mpaka sasa.

Kwa sasa wafanyakazi wa msalama mwekundu wamekuwa wakifanya kazi bila kupumzika kuhakikisha wanakusanya miili hiyo ya watu waliopoteza maisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la ndege la Ethiopia, ndege hiyo iliruka saa 2:38 asubuhi kwa saa za Ethiopia kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole na watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wanatoka katika nchi 33.

 

ADVERTISEMENT