In Summary
  • Simba imetolewa ikiendeleza rekodi yao ya kushindwa kupata ushindi ugenini tangu walipotinga raundi ya kwanza kwani imepoteza kwa Nkana ya Zambia, AS Vita ya DR Congo, Al Ahly ya Misri na sasa Mazembe pia ya DR Congo, huku mechi pekee waliyoshinda ugenini ni ile ya raundi ya awali dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini.

KIKOSI cha Simba kilirejea usiku wa juzi mara baada ya pambano lao la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo na asubuhi hii wanaianza safari kuelekea jijini Tanga kuwahi mechi yao na Coastal Union, huku nyuma straika Meddie Kagere na beki Juuko Murshid wakiwa gumzo kubwa.

Simba iliifuata Mazembe kwao katika mechi ya marudiano kuwania kutinga nusu fainali na kufungwa mabao 4-1, huku baadahi ya wadau wa soka wakifunguka kuhusu nyota hao wawili wa Msimbazi.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ya kuwaanzisha benchi, Kagere na Clatous Chama, kisha kumtoa beki kisiki Juuko Murshid kumetajwa kama sababu ya Simba kung’olewa na Mazembe, licha ya kuwatangulia kuwafunga bao la mapema mjini Lubumbashi.

Kocha Aussems alifanya mabadiliko hayo dakika ya 46 kwa kumtoa kiungo mshambuliaji, Mzamiru Yassin na beki Juuko na kuwaingiza Chama na Kagere, jambo lililoibua mjadala mkubwa kwa wadau wa soka wakiamini ndicho kilichoiponza timu hiyo ikung’utwe mabao 4-1 na kuaga mashindano.

Inaelezwa kuwa, Mbelgiji huyo ni kama alichemka kwa kumuanzisha benchi Kagere anayeongoza kwa mabao kwenye kikosi hicho katika michuano ya CAF na hata Ligi Kuu.

Kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyeidakia Simba na Pilsner, Idd Pazi ‘Father’ alisema kilichofanywa na Aussems cha kumtoa Juuko ili kumuingiza Kagere wakati timu ipo nyuma kwa mabao 2-1 kilikuwa kama kuiunguza timu na ndicho alichokivuna Aussems.

“Juuko ndiye alikuwa amebaki pale nyuma baada ya Wawa (Pascal) kuumia, halafu unamtoa unamuingiza fowadi ili akakabe au alimaanisha nini?” Alihoji kocha huyo wa zamani wa makipa wa Simba.

Pazi alisema kocha alicheza pata potea katika sabu yake huku akidai hata mabao 4-1 waliyofungwa yalikuwa madogo kama Mazembe wangetulia kwani, kosa kosa zilikuwa nyingi langoni kwa Simba kulinganisha na mabao waliyofungwa.

“Tulipaswa kutulia baada ya Mazembe kusawazisha, hata walipoongeza bao la pili, ilikuwa ni sisi tujipange tu na kutafuta mbinu ya kusawazisha ili iwe 2-2, lakini tulishindwa na baada ya mabadiliko mabao ndiyo yakaongezeka,” alisema.

Hata hivyo, Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla na mchambuzi wa soka, Ally Mayay walitofautiana na Pazi, kwani kiungo wa zamani wa Yanga na Stars, Mayay alisema kwa kocha kujaribu na kukosea au kupatia kwenye sabu ni kawaida, ingawa katika mechi hiyo, Mazembe walikuwa na kila sababu ya kushinda.

“Hakuna sababu ya kumlaumu kocha, angalieni na ubora wa Mazembe imemiliki mipira kwa asilimia 70, isitoshe Simba ilikuwa imeshafungwa, kocha alikuwa anajaribu ili kuona kama wachezaji anaowaingiza watapindua meza, lakini ikashindikana,” alisema Mayay.

Aliongeza hatua waliyofikia Simba ni kubwa na kama msimu ujao watapata nafasi nyingine ya kushiriki mashindano hayo watafika mbali zaidi.

Naye Dk Msolla alimkingia kifua Aussems kumuanzishia Kagere benchi akisisitiza kuwa hata yeye amekuwa akitumia mbinu hiyo.

“Mashabiki wasimlaumu kocha kwa kumuanzisha Kagere benchi, inawezekana mchezaji mkubwa kuanzia benchi ili kuusoma mchezo na akiingia anakwenda kubadili matokeo. Lakini kwa mechi ya jana, tayari Simba ilishazidiwa hivyo hata anayeingia angehangaika tu na ndicho kilitokea,” alisema.

Akizungumzia udhaifu wa Simba, Dk Msolla ambaye ni Mgombea Uenyekiti katika Uchaguzi wa Yanga, alisema bado wana tatizo katika matumizi ya viungo na mabeki wao kufanya makosa yanayojirudia.

“Viungo wa Simba hawashambulii, hawatanui uwanja ili kuwatawanya mabeki, hawatoa pasi sahihi na kwa wakati hicho ndicho kinawagharimu, lakini pia mabeki wanafanya makosa yale yale, lakini pia timu haijawa na maarifa ya kucheza ugenini,” alisema.

KASHASHA AFUNGUKA

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha yeye alisema wazo la kocha kwenye sabu lilikuwa ni sawa na kubeti.

“Matokeo yangebaki 2-1 maana yake Simba wametoka, hivyo kocha alipaswa kushambulia, lakini aangalie pia asifungwe, huwezi kufunga halafu usizuie usifungwe, hiyo ni sawa na kubeti,” alisema.

Mchambuzi huyo maarufu alisema ni kweli Kagere ana mabao mengi, lakini wakati mwingine mwalimu huangalia aina ya mchezo na jinsi ya kuwatumia vijana wake, hivyo kwake siyo ishu japo anafahamu kukaa benchi kwa straika huyo mwenye mabao 14 katika Ligi na sita ya CAF kuliwashtua wengi.

Simba imetolewa ikiendeleza rekodi yao ya kushindwa kupata ushindi ugenini tangu walipotinga raundi ya kwanza kwani imepoteza kwa Nkana ya Zambia, AS Vita ya DR Congo, Al Ahly ya Misri na sasa Mazembe pia ya DR Congo, huku mechi pekee waliyoshinda ugenini ni ile ya raundi ya awali dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini.

WAGOSI WAJIPANGE

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri leo Jumatatu kwenda Tanga kwa ajili ya mechi yao ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, huku rekodi zikionyesha katika mechi 10 zilizopita Simba haijapoteza hata moja katika ligi hiyo, hivyo Wagosi lazima wajipange kwelikweli.

Mechi ya Simba na Coastal ambayo awali ilipangwa kuchezwa leo itafanyika keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Mkwakwani, siku ambayo Yanga itakuwa mjini Morogoro kuvaana na Mtibwa Sugar na kuzidi kuongeza presha ya ubingwa kwani jana Azam walikuwa ugenini dhidi ya Mbeya City.

Yanga ndio wanaoongoza msimamo kwa alama 74.

ADVERTISEMENT