In Summary
  • Mwandishi mmoja wa habari maarufu huko Ulaya, alisema Mourinho anajiona kabisa anarudi kuinoa Real Madrid na huenda akabamba dili hilo kabla ya msimu huu kumalizika.

MADRID,HISPANIA .WANASEMA kufa kufaana. Na watoto wa uswahilini wana msemo wao, adui yako mwombee njaa. Basi sawa, sema unavyotaka kusema, lakini pengine hayo yote yatakuwa yanafanywa na Jose Mourinho kwa sasa.

Hakuna ubishi, Mourinho kuna mtu atakuwa anamwombea njaa kwa sasa. Hapana, hawezi kuwa Ole Gunnar Solskjaer kwa sababu huko ameshaharibu na hawezi kurudi tena kwa sasa.

Mourinho alifutwa kazi mwezi uliopita tu huko Manchester United na sasa yupo kijiweni hana kazi. Lakini huko na huko anasikia jina lake linatajwa likihusishwa na kazi mpya huko, Santiago Bernabeu kwenye kuinoa Real Madrid kwa mara nyingine.

Lakini ajira hiyo inategemea na kile atakachofanya kocha wa sasa, Santiago Solari. Wachambuzi wa mambo wanadai Mourinho kwa sasa sala zake ni kuona Solari akifanya hovyo Bernabeu, ili akachukue kazi.

Kulenga kupata ajira hiyo ndio maana hata Mourinho ameripotiwa kukataa ajira ya kuinoa Benfica, akidai anataka kazi kwenye klabu kubwa.

Mwandishi mmoja wa habari maarufu huko Ulaya, alisema Mourinho anajiona kabisa anarudi kuinoa Real Madrid na huenda akabamba dili hilo kabla ya msimu huu kumalizika.

Mwandishi, Daniel Storey alisema hamwoni Solari kama atadumu kwenye kikosi hicho kutokana na timu kuendelea kupata matokeo mabovu uwanjani, ambayo kimsingi ndiyo yaliyomfukuzisha kazi mtangulizi wake.

Solari amekuwa kwenye presha kubwa akishindwa kubadili matokeo ya kwenye kikosi hicho, Madrid ikipoteza tu na kushuka zaidi kwenye msimamo wa ligi tangu alipochukua mikoba kutoka kwa Kocha Julen Lopetegui. Mourinho hana kazi na amedaiwa kuwa na uhusiano mzuri na Rais wa Real Madrid, Flortentino Perez, hivyo Storey anaamini Mreno huyo hawezi kusota kwa muda mrefu kijiweni kabla ya kukamatia kazi hiyo ya nguvu kabisa.

“Inaonekana wazi kabisa Jose Mourinho inaweza kuwa bahati yake hii,” alisema Storey.

“Mashabiki walionyesha wazi kabisa wakimweleza Rais Florentino Perez hawafurahii kinachoendelea. Kwa hilo nadhani siku za Santiago Solari zimeshafika mwisho, nadhani kuna mwisho wa Mourinho kuja kwenye timu hiyo.”

Real Madrid kwa sasa ipo nje ya nafasi itakayoifanya ikamatie tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo hali ikiendelea kuwa mbaya haiwezi kuvumilia na kuliacha hilo likiendelea, bila ya shaka Solari ataonyeshwa mlango wa kutokea.

Real Madrid inafahamu wazi nahodha wake, Sergio Ramos huenda akaachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu, hivyo haioni shida kumrudisha Kocha Mourinho kwenye kikosi chake. Mourinho aliinoa Real Madrid kwa miaka mitatu, kuanzia 2010 na kufutwa kazi 2013.

Kwa sasa kikosi hicho kinashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa La Liga, kikiwa pointi 10 nyuma ya vinara ambao ni mahasimu wao wakubwa kwenye mbio za ubingwa, Barcelona. Hali yao ni mbaya na imekuwa ikifungwa hadi na timu zisizotarajiwa.

ADVERTISEMENT