In Summary

Jokate ampongeza Dulla Mbabe kumchapa Francis Cheka ampatia eneo la kufanyia mazoezi na kuwafundisha vijana wengine.

Dar es Salaam. Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amempa eneo la kufanyia mazoezi bondia Abdallaha Pazi ‘Dulla Mbabe’ ili aweze kuwafundisha vijana wa wilaya hiyo mchezo wa masumbwi.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Dulla Mbabe kushinda pambano lake dhidi ya Bondia wa Morogoro, Francis Cheka na kuitangaza Kisarawe kwenye ramani ya michezo.
Jokate amesema, wilaya hiyo ina vijana wengi wenye vipaji hivyo uongozi umeona umpatie Dulla eneo la mazoezi ili aanze kuwapa mafunzo wanaotaka kujifunza mchezo huo.
“Tunataka kila kitu tufanye vizuri Kisarawe nina imani vipaji vipo vingi lazima tuvikuze na kuvitangaza. Alichokifanya Dulla kimetupa heshima sasa tunataka vijana kama hawa wawe wengi, uwezo huo tunao na hilo litafanikiwa,”alisema Jokate.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu amemkaribisha Dulla Mbabe bungeni kwa ajili ya kupeleka mkanda alioupata katika pambano hilo.
“Umetuletea heshima kubwa na kuonyesha kwamba Kisarawe kuna vipaji tunataka kuandika historia tunakukaribisha bungeni,”amesema Vullu.

ADVERTISEMENT