In Summary
  • Baobab wanashika nafasi ya 11 ikifunga bao moja na kufungwa 12, huku Tanzanite wakiwa juu yao ikiwa imefunga mabao mawili na kufungwa 10 na kumpa kazi Kocha aliyepandisha daraja, Abdallah Juma kuwa na kazi ya ziada kuizoea ligi hiyo.

ACHANA na matokeo ya mechi yao ya jana Jumatano dhidi ya Baobab ya Dodoma, watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL), JKT Queens wameonyesha dhamira ya kutetea taji hilo baada ya kushinda mechi zao tatu za awali ikiwa timu pekee iliyofanya hivyo.

Kadhalika nyota wake Fatuma Mustafa na Asha Rashid ‘Mwalala’ wakiongoza orodha ya wafungaji kileleni, wakiwaburuza wenzake.

Fatuma amefunga mabao 14 akifuatiwa na Asha mwenye 11 na kufanya wawili theluthi mbili ya mabao ya timu yao ambayo ni 31 huku ukuta wao ukiwa haujaruhusu bao lolote kama ilivyo kwa Mlandizi Queens na Sisterz ya Kigoma.

JKT waliobeba taji hilo msimu uliopita, imeshinda mechi zao zote kwa asilimia 100, ikifikisha alama 9 na mabao 31 na kama jana imepata ushindi basi huenda ikazidi kuwaacha mbali wapinzani wao 11 wanaochuana nao kwenye msimu huu wakiwamo wageni Yanga Princess na Tanzanite FC ya Arusha.

Waliokuwa mabingwa wa awali wa michuano hiyo ilipoanzishwa miaka mitatu iliyopita Mlandizi Queens na Sistars na Simba Queens kabla ya mechi zao za jana walikuwa wakiwafukuzia watetezi hao kwa kuwa na alama 7 kila mmoja.

Eneo la mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo inayochezwa kwa msimu wa tatu mfululizo tangu ilipoasisiwa enzi za utawala wa TFF ya Jamal Malinzi, wapo Mapinduzi Queens ambayo ndio timu pekee ambayo haijafunga bao hata moja, huku yenyewe ikiruhusu mabao 29 kutokana na michezo mitatu ambayo yote imepoteza.

Sio Mapinduzi tu isikuwa na pointi, bali haya Baobab Queens ya Dodoma na wageni wa ligi hiyo, Tanzanite ya Arusha nazo hazijaonja ushindi wala sare, lakini zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na waburuza mkia.

Baobab wanashika nafasi ya 11 ikifunga bao moja na kufungwa 12, huku Tanzanite wakiwa juu yao ikiwa imefunga mabao mawili na kufungwa 10 na kumpa kazi Kocha aliyepandisha daraja, Abdallah Juma kuwa na kazi ya ziada kuizoea ligi hiyo.

Tanzanite ilipanda msimu huu baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi Daraja la Kwanza kwa kufungwa katika fainali ya ligi hiyo na Yanga Princess iliyoshiriki pia Ligi ya Daraja la Kwanza kwa mara ya kwanza na kupanda ikiishangaza wazoefu hao.

Kwenye orodha ya wafungaji mpaka sasa, nyota wa JKT Queens wanawaburuza wengine, jambo linaloonyesha wababe hao wamepania kufanya kweli msimu huu kwa mara nyingine.

ADVERTISEMENT