In Summary
  • Mazingira ya nyumba anayoishi ni utulivu, huku wachezaji wengi wa Azam wakiwa wamepanga wote maeneo hayo, hivyo kimekuwa kama ni kijiji chao cha kukaa karibu ili waweze kuwahi mazoezini.

MASHABIKI wa Simba ni ngumu kulisahau jina la Idd Kipagwile ‘Mtoto Idd’ baada ya kuwatoa katika mashindano ya Mapinduzi Cup kupitia bao lake na kuzua balaa katika kikosi hiko.

Baada ya bao hilo na kiwango ambacho alichokionyesha katika mashindano hayo, wengi walitarajia kuona mchezaji huyo akienda katika moja ya klabu mbili zilizopo mitaa ya Kariakoo, lakini aliendelea kusalia Azam.

Msimu huu Kipagwile amegeuka kuwa mchezaji wa kawaida kiasi ambacho Mwanaspoti liliamua kumpigia kambi mpaka nyumbani kwake mitaa ya Chamazi na kupiga naye stori.

Mazingira ya nyumba anayoishi ni utulivu, huku wachezaji wengi wa Azam wakiwa wamepanga wote maeneo hayo, hivyo kimekuwa kama ni kijiji chao cha kukaa karibu ili waweze kuwahi mazoezini.

MKE AMWEKA SAWA

Ni ngumu kuamini kama Kipagwile ameamua kuishi na mtu ndani, kwani baada ya Mwanaspoti kutia timu nyumbani kwake tulikuta nyumba ipo katika mazingira ya usafi na ndipo alifunguka kuna mrembo, Nayma Yusuph ambaye anaweka mambo sawa. Jamaa anafunguka baada ya kumuoa mdada huyo ni kama amemwongezea maarifa kichwani kwake kwani anatambua kabisa hivi sasa anapambania maisha yake na wengine.

“Ukiwa na mtoto wa mtu ndani unatakiwa upambane, pia amenitanua akili zaidi kwa sababu tunakaa pamoja na kutengeneza mipango ya mbele zaidi, pia ananifanya kuwa wa tofauti.”

SIMBA YAMPIGIA HESABU MUDA MREFU

Ishu imefichuka kumbe sio baada ya kuifunga tu Simba ndio akawekwa katika mipango ya kusajiliwa na timu hiyo, Kipagwile alisema baada ya kutoka Majimaji alikuwa anahitajika na Simba lakini mtu wake wa karibu alimshauri kwenda Azam kutokana na kuahidiwa kupata kila kitu kwa wakati.

“Nilikuwa nahitaji kucheza timu kubwa na ofa zilikuja kipindi kile lakini kaka yangu ambaye ananishauri mambo mengi aliniambia niende Azam, kweli nilivyofika mpaka hivi sasa napata kila kitu kwa wakati,”.

Aliongeza baada ya kuitoa Simba katika michuano ya Mapinduzi mwaka juzi, alikuwa akihusishwa kwenda tena Simba, hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote ambaye alifika kuzungumza nae.

“Hakuna kiongozi yeyote wa Simba ambaye amenifuata, tetesi tu zilikuwa zinaenea na kuzisikia kama watu wengine walivyokuwa wanazisikia, lakini inawezekana hawakuja kwa sababu nilikuwa na mkataba wa muda mrefu,” alisema mchezaji huyo aliyewahi kuichezea timu ya vijana ya Simba kabla ya kutimkia Majimaji.

AZAM YAMPA MJENGO

Ndoto za wachezaji wengi hivi sasa ni kuhakikisha wanatimiza baadhi ya vitu ambavyo walikuwa wamevipanga, kwa Kipagwile napo ni hivyo hivyo kwani Azam imempa maisha baada ya kuweza kujenga mjengo wake nyumbani kwao Songea.

“Hapana hapa sio kwangu nimepanga tu, mimi nilivyopata pesa yangu ya usajili Azam niliamua kujenga nyumbani Songea, kitu kikubwa hiki kwa sababu hujui kesho yako na ndiyo maana nimeamua kuanza naamini mambo mazuri mengine yatakuja,” alisema.

SIRI YA KUTOSIKIKA

Kwenye msimu huu ambao ndio wa mwisho kwa Kipagwile amekuwa na wakati mgumu katika kikosi cha Azam, baada ya kushindwa kabisa kuingia katika kikosi cha Kwanza.

Hata hivyo, yeye mwenyewe alikiri ugumu upo kwa upande wake lakini bado hajavunjika moyo wa kuzidi kupambana kuhakikisha anarejea katika kikosi cha kwanza.

“Huwezi kusikika kama ukiwa huchezi na hilo nalijua kabisa mimi sio yule wa msimu uliopita, lakini sio kwamba kiwango kimeshuka hapana, kwa sababu nikipata nafasi nacheza na nikijipima najiona uwezo wangu,” alisema.

Aliongeza katika michezo iliyosalia atahakikisha analishawishi benchi la ufundi ili aweze kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.

UBINGWA WA TPL

Tangu ameingia Azam, timu hiyo imeweza kuchukua vikombe tofauti kama Kagame na Mapinduzi mara mbili mfululizo, lakini Kipagwile bado ameweka akili yake katika kombe la Ligi Kuu.

Huku akishusha pumzi na kuonyesha tabasamu usoni mwake, anasema jambo kubwa ambalo analihitaji kwa muda huu ni kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu.

“Vikombe vingine tayari nimeshavaa medali zake, natamani sana nivae medali ya ubingwa wa Ligi Kuu, kama nikivaa nikiwa na Azam ni sawa au nikiwa sehemu nyingine ndoto yangu ni kuvaa medali hiyo.”

KUVUKA MIPAKA

Kipangwile pia ana ndoto ya kutoboa na kwenda kujaribu bahati yake nje ya nchi.

“Mipango ipo na lolote linaweza likatokea hivi karibuni kwa sababu kuna mtu ananisimamia kuhakikisha nasogea mbele, muda ukifika mtaona na kusikia.”

ADVERTISEMENT