In Summary

Ngoma za Mama Nipe Radhi, Nani Kama Mama, Viwavi Jeshi, Mama Mashauzi, Mapenzi Hayana Dhamana, Asiyekujua Hakuthamini, Sura Surambi, Kismet, Thamani ya Mama. Ngoma hizo zote zilikuwa kwenye mahadhi ya taarabu.

KAMA unadhani walimpa Isha Mashauzi jina la Queen of the best melodies walikosea basi utakuwa umelala na unatakiwa kuamshwa kutoka usingizi.
Umeshasikia ngoma za Mama Nipe Radhi, Nani Kama Mama, Viwavi Jeshi, Mama Mashauzi, Mapenzi Hayana Dhamana, Asiyekujua Hakuthamini, Sura Surambi, Kismet, Thamani ya Mama. Ngoma hizo zote zilikuwa kwenye mahadhi ya taarabu, ambao staili yake zilikuwa zikiwafanya mashabiki kupandwa mizuka.
Waweke pembeni kwanza akina Khadija Kopa, Nasma Hamis Kidogo ambao hakika hawana mpinzani, Mzee Yusuf na Isha Mashauzi wana mchango mkubwa sana kwenye taarabu ya kisasa ambayo ilikuwa na staili za kupiga masebene hivyo, mashabiki kupata burudani hadi kupatwa mizuka.
Lakini, baada ya kutamba kwenye taarabu na kutengeneza jina, Isha Mashauzi alitoka na kwenda kuanzisha bendi yake ya Mashauzi Classic na hapo akaangusha ngoma za Nimlaumu Nani, Nimpe Nani, Jiamini na Nibembeleze ambazo zilikuwa kwenye mahadhi ya muziki wa dansi.
Hata hivyo, kwa sasa Isha Mashauzi yuko kwenye mchakato matata wa kuvamia kwenye Bongo Flava na tayari kuna ngoma mpya ya Yeke Yeke ambayo imeshaiva lakini bado hajaichia.
Isha Mashauzi, ambaye amewahi kubeba tuzo kibao ikiwemo ile ya Kilimanjaro Music kupitia taarab, amesema kuingia kwenye Bongo Flava hakuna maana kwamba, anaachana na kuimba taarabu ama dansi, bali kuna fursa moja matata sana ameiona huko.
"Muda si mrefu nitaishusha Yeke Yeke kwa mashabiki, lakini sio kuwa nitaweka makazi jumla kwenye Bongo Flava, hapana ni suala la kutanua wigo wa biashara tu na kudhihirisha uwezo wangu kwenye muziki. Natambua kuwa niko vizuri hivyo, nataka kudhihirisha hilo," alisema na kuongeza:
"Kiukweli staili ninayotumia itabamba sana na kamwe haitawachanganya mashabiki wangu ila itakwenda kuongeza mzuka hasa kwa ambao hawapendi dansi na taarabu."

ADVERTISEMENT