In Summary
  • Nahodha huyo wa Taifa Stars, amefunga mabao hayo 20 kwenye michezo 28 ya Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ na kwenye idadi hiyo ya michezo pia ametoa ‘asisti’ zilizozaa mabao matatu.

STRAIKA na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ ndiye mshambuliaji wa Kiafrika anayekimbiza zaidi barani Ulaya akiwaburuza Mohamed Salah wa Liverpool na Nicolas Pepe wa Lille.

Samagoal ambaye jana Jumapili alikuwa akiiongoza klabu yake ya KRC Genk mbele ya Club Brugge kwenye mchezo wa mchujo, Ligi Kuu Ubelgiji, anaongoza orodha ya mastaa kibao wa Kiafrika waliofunga mabao mengi kwenye ligi zao barani humo.

Kabla ya mchezo wa jana usiku, Samatta ambaye ni kinara wa mabao kwenye Ligi ya Ubelgiji akiwa na mabao 20, alimuacha kwa mabao mawili Mmisri, Mo Salah (18) ambaye anacheza soka la kulipwa nchini England.

Nahodha huyo wa Taifa Stars, amefunga mabao hayo 20 kwenye michezo 28 ya Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ na kwenye idadi hiyo ya michezo pia ametoa ‘asisti’ zilizozaa mabao matatu.

Salah ambaye amekuwa akitegemewa kwenye kikosi cha Liverpool kilichopo chini ya kocha wao, Jurgen Klopp, ametumia mechi 33 kufunga mabao 18 huku akitoa ‘asisti’ tisa.

Msenegal Pepe wa Lille kabla ya Jumapili usiku naye alikuwa mzigoni kuipigania klabu yake mbele ya PSG kwenye mchezo wa Ligi, alikuwa ameachwa na Samatta kwa mabao mawili sawa na Salah ambaye naye chama lake lilikuwa na kibarua dhidi ya matajiri wa London, Chelsea.

Pepe ametumia michezo 31 ya Ligi Kuu Ufaransa kufunga mabao 18 huku akiwazidi Salah na Samatta kwenye kutengeneza mabao. Msenegal huyo ametengeneza mabao 11.

Nyota wengine wa Kiafrika waliochwa mbali kwa mabao kwenye ligi mbalimbali barani Ulaya ni Msenegal, Sadio Mane wa Liverpool na Mgabon, Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal wote wenye mabao 17.

Wengine ni Mualgeria Ishak Belfodil wa Hoffenheim (13), Mtunisia Wahbi Khazri wa AS Saint-Etienne (12), Muivory Coast Gervais Yao Kouassi ‘Gervinho’ wa Parma, Max-Alain Gradel wa Toulouse, Mguine Francois Komano wa Bordeaux na Muafrika Kusini Lebo Mothiba wenye mabao 10 kila mmoja.

VITA JUU YA VITA

Samatta mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kukutana na baadhi ya mastaa wa Kiafrika ambao amewapoteza kwa ufungaji barani Ulaya kwenye fainali za Mataifa ya Afrika akiwa na Taifa Stars nchini Misri Juni mwaka huu.

Mastaa hao ni Mane na Belfodil ambao mataifa yao ya Senegal na Algeria yamepangwa na Tanzania kwenye Kundi C pamoja na Kenya yenye nyota kama Victor Wanyama.

ADVERTISEMENT