In Summary
  • Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya mchango na ufanisi wa kila mchezaji wa Taifa Stars katika Afcon ambayo inapimwa kwa alama au pointi chini ya 10.

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinaendelea Misri na leo hatua ya 16 bora itafikia tamati kabla ya kuanza mechi za robo fainali.

Wakati hatua ya 16 bora ikimalizika, Taifa Stars imeaga baada ya kuwa timu ya kwanza kuondolewa kwenye fainali hizo, ikifungwa mechi zote tatu ilizocheza dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria, ikipachika mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Katika kundi la wachezaji 23 ambao walikuwemo katika kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki Afcon, wapo ambao walifanya vizuri zaidi, wapo waliotoa mchango wa wastani, kuna wale ambao walionyesha kiwango cha chini na pia wengine walishindwa kucheza mechi hata moja.

Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya mchango na ufanisi wa kila mchezaji wa Taifa Stars katika Afcon ambayo inapimwa kwa alama au pointi chini ya 10.

Aishi Manula-7

Amemaliza hatua ya makundi ya Afcon akishika nafasi ya pili katika chati ya makipa waliookoa idadi kubwa ya mashambulizi katika hatua hiyo akifanya hivyo mara 14 huku kinara akiwa ni Lloyd Kazapua wa Namibia aliyeokoa michomo 15.

Alifanya kazi nzuri katika mechi dhidi ya Senegal lakini kwenye mechi ya pili dhidi ya Kenya alifanya makosa kadhaa ambayo likiwemo la kuokoa vibaya mipira ya kona, faulo na krosi.

Metacha Mnata-4

Hakucheza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Senegal na Kenya lakini akaja kupangwa katika mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria ambao Taifa Stars ililala mabao 3-0.

Pamoja na uchanga wake, alijitahidi kwa kiasi chake kulinda lango akipanga vizuri mabeki na kuwasiliana nao mara kwa mara ingawa alifanya makosa kadhaa ambayo kama angekuwa na uzoefu pengine yasingejitokeza. Pamoja na hilo, aliokoa michomo miwili ambayo ingeweza kuwapa Algeria mabao.

Hassan Kessy-4

Hakuonyesha kiwango kizuri katika mechi ya kwanza dhidi ya Senegal ambayo alicheza rafu za mara kwa mara ambazo zilichangia aonyeshwe kadi ya njano lakini pia alishindwa kukaba na kufanya wapinzani watumie zaidi upande wake.

Alicheza vyema dhidi ya Kenya lakini katika mechi dhidi ya Algeria ya mwisho alikuwa na kiwango cha wastani.

Kelvin Yondani-7

Alijitahidi kufuta makosa mengi ya mabeki wenzake na kukabiliana na washambuliaji wasumbufu lakini bado juhudi zake zilikwamishwa na udhaifu wa wenzake ingawa hakucheza mechi ya mwisho dhidi ya Algeria baada ya kuumia.

Alicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na alifanya faulo tatu tu katika mechi zote jambo lililomfanya asionyeshwe kadi katika mashindano hayo.

David Mwantika-5

Alicheza kwa juhudi katika michezo yote akitumia vyema umbo lake kuwakabili washambuliaji wa timu pinzani akiondosha hatari 10 zilizoelekezwa langoni mwa Taifa Stars. Hata hivyo nidhamu yake ilikuwa chini na alifanya faulo nne ambazo zilimfanya amalize akiwa na kadi moja ya njano.

Gadiel Michael-7

Miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri kwenye kikosi cha Taifa Stars katika mechi mbili alizocheza. Alitengeneza nafasi mbili, alipiga krosi tano ambazo hazikuzaa matunda, alipiga shuti moja lililolenga lango na kiwango chake bora kilisababisha awe miongoni mwa wachezaji waliofanyiwa faulo nyingi ambapo alichezewa rafu mara tatu.

Erasto Nyoni-6

Alikosa mechi ya kwanza kutokana na majeruhi na akarudi uywanjani katika mechi ya pili na tatu dhidi ya Kenya na Algeria ambazo alicheza dakika 170.

Alinasa mipira saba aliyogombea na wachezaji wa timu pinzani na alipiga jumla ya pasi 85 kwenye mechi mbili.

John Bocco-3

Alicheza mechi zote tatu kwa dakika 115. Alipiga pasi 27 tu zilizofika kwa walengwa. Hakupiga shuti hata moja lililolenga lango ingawa alipiga mawili ambayo hayakulenga.

Feisal Salum-3

Alipiga pasi 33 katika mechi mbili alizocheza, alipora mipira kwa wapinzani mara tatu. Hakutengeneza nafasi hata moja wala kupiga pasi ya mwisho na alimaliza akiwa na kadi moja ya njano.

Mbwana Samatta-9

Alikuwa mfano bora ndani ya uwanja kama nahodha. Alifunga bao moja na kuchangia kupatikana kwa linguine dhidi ya Kenya. Ndiye mchezaji aliyekuwa akitazamwa zaidi na wachezaji wa timu pinzani.

Saimon Msuva-7

Alicheza mechi zote tatu kwa dakika 246. Alifunga goli moja, akipiga shuti moja lililolenga lango na pia amemaliza akiwa na mashuti matatu ambayo hayakulenga lango. Alitengeneza nafasi tatu na kupiga krosi moja iliyofikia mlengwa.

Farid Musa-8

Alitengeneza nafasi nne kwenye mashindano hayo na miongoni mwa wachezaji waliopiga idadi kubwa ya pasi kwenye mashindano ambazo ni 64. Kasi yake ilionekana kuwapa nafasi wapinzani kumdhibiti.

Mudathir Yahya-7

Ni mchezaji aliyefanya kazi kubwa kwenye safu ya kiungo, kutokana na uwezo wake wa kutengeneza balansi ya timu kwa kusaidia safu ya ulinzi na kuchezesha timu. Alitengeneza nafasi moja ya bao, alipiga mashuti mawili ambayo hayakulenga lango, alipiga pasi 82 ingawa alimaliza na kadi ya njano.

Frank Domayo-2

Alicheza mechi mbili tu kwa dakika 16. Hakutoa mchango mkubwa kwani alipiga pasi tisa tu.

Ally Mtoni-5

Alicheza mechi ya mwisho tu dhidi ya Algeria lakini alijitahidi kuonyesha kiwango kizuri, akipiga pasi 35, kuondosha hatari nne pasipo kufanya faulo yoyote huku yeye akichezewa rafu mara moja.

Himid Mao-4

Hakuonyesha kiwango kizuri kwenye mechi zote tatu ambazo Stars ilicheza. Alifanya faulo za mara kwa mara ambazo ziliiweka Taifa Stars hatarini. Alipiga pasi 65 zilizofikia walengwa na alimaliza akiwa na kadi moja ya njano.

Mohammed Hussein-3

Alicheza mechi moja tu ambayo ilikuwa ya mwisho dhidi ya Algeria. Mechi ambayo alipata wakati mgumu mbele ya Adam Ounas ambaye alikuwa mwiba kwake na idadi kubwa ya mashambulizi ambayo Algeria ilipeleka langoni mwa Taifa Stars yalitokea upande wake. Hakupiga krosi hata moja wala kutengeneza nafasi ingawa alipiga jumla ya pasi 40 zilizofikia walengwa.

Adi Yussuf-2

Alicheza kwa dakika 45 tu kwenye mashindano hayo tena akiingia kutokea benchi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Algeria akichukua nafasi ya Farid Musa. Alifanya faulo nne zilizopelekea aonyeshwe kadi ya njano. Alikuwa mzito na alipiga mashuti mawili ambayo moja lililenga lango huku jingine likitoka nje ingawa alionyesha uwezo mzuri wa kujipanga kwenye nafasi.

Thomas Ulimwengu-4

Nguvu zake zilisaidia katika kupambana na kuwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani na kupelekea afanyiwe faulo tatu lakini hakupiga shuti hata moja langoni mwa timu pinzani na alipiga pasi 18 tu katika dakika 94 alizocheza kwenye mechi mbili.

Waliokosa nafasi

Wachezaji Aaron Kalambo, Vicent Phillipo, Rashid Mandawa,na Yahya Zayd hawakupata bafasi ya kucheza mechi hata moja.

ADVERTISEMENT