In Summary

Real Madrid wanajaribu kuishawishi Man United ili iwauzie staa huyo anayesakwa kwelikweli na Kocha Zinedine Zidane, ambaye amepanga kuijenga upya Los Blancos.

MADRID, HISPANIA.EDEN Hazard amemwambia Paul Pogba anamtaka akajiunge na Real Madrid ili wakapige mzigo wote huko Bernabeu.

Hazard ameshakamilisha dili lake la kutua Real Madrid ambalo litawagharimu wababe hao wa La Liga hadi Pauni 150 milioni, ambapo juzi Alhamisi alitambulishwa huko Bernabeu mbele ya mashabiki 50,000 na kutimiza ndoto yake ya tangu utotoni ya kwenda kuitumikia timu hiyo.

Imemchukua muda mrefu hadi Hazard kutua Real Madrid huku akiacha pengo kubwa huko Chelsea kutokana na wakali hao wa Stamford Bridge kuwa na adhabu ya kuzuiwa kusajili, hivyo itawachukua muda mrefu kupata staa wa kiwango kama chake kuziba pengo.

Sasa, Hazard anamtaka Pogba aende akajiunge naye huko Bernabeu kukifanya kikosi hicho kuwa na makali ya kutisha. Kiungo huyo wa Manchester United, Pogba naye anahusishwa na wababe hao wa Barnebau.

Real Madrid wanajaribu kuishawishi Man United ili iwauzie staa huyo anayesakwa kwelikweli na Kocha Zinedine Zidane, ambaye amepanga kuijenga upya Los Blancos.

Hazard amezungumzia pia Kylian Mbappe, ambaye pia mashabiki wanamtaka akakipige kwenye kikosi chao. “Nataka kucheza na wachezaji bora, na hao ndio wachezaji bora. Lakini, hilo si jambo langu kuzungumza kuhusu usajili.”

Huko Man United, Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka tu kuachana na Pogba, akitaka kusajili wachezaji wake, lakini jambo hilo linapingana na bosi kubwa, Ed Woodward ambaye anamtaka mchezaji huyo abaki kutokana na mambo ya kibiashara, kuvutia wadhamini.

Man United ilimsajili Pogba kwa Pauni 89 milioni, ada iliyoweka rekodi ya dunia mwaka 2016 kuutokea Juventus.

ADVERTISEMENT