In Summary

Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitafunguliwa rasmi Juni 21 kwa mechi baina ya Misri na Zimbabwe na ile ya Uganda na DR Congo ingawa Stars itacheza Juni 23 dhidi ya Senegal.

Dar es Salaam. Serikali imezindua rasmi Harambee ya kuichangia timu ya Taifa 'Taifa Stars' kwa ajili ya kufanikisha ushiriki wake katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoanza Ijumaa huko Misri.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa harambee hiyo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema fedha zitapelekwa moja kwa moja kwa wachezaji ili ziwape hamasa.

"Tunasikia taarifa jinsi nchi nyingine zinavyojipanga kuhakikisha vijana wao wanafanya vizuri katika mashindano hayo kwa kuwapa kiasi kikubwa cha fedha.

“Sisi tumeona ni vyema kuwapa hamasa vijana wetu. Vijana wetu ni wazalendo sana. Hicho kinachofanywa na nchi nyingine ni vita ya kisaikolojia hivyo tumeona ni vyema tufanye kitu ili kuwapa morali wachezaji wetu wafanye vizuri," alisema Waziri Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa Watanzania walio tayari kuchangia wanapaswa kutuma fedha kupitia akaunti ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) namba 0111010009781 kwenye Benki ya NBC au akaunti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) namba 01J1019956700 au kupitia mtandao wa simu za mkononi wa Vodacom kwa kupiga *150*00# kisha kubofya.

Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Taifa Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema huu ni wakati wa Watanzania kuonyesha umoja kwa kuichangia timu hiyo.

"Imani yangu kwamba kupitia hili, Watanzania wataungana na Serikali ya awamu ya tano kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na morali. Tunawaomba tuonyeshe kuwa nchi hii ina umoja kwa kuisapoti Taifa Stars," alisema Makonda

ADVERTISEMENT