In Summary
  • Madagascar ikumbukwe ndio mara yake ya kwanza kabisa kushiriki katika mashindano haya. Imewashangaza wengi mno. Kweli kujiamini kunahitaji roho kama ya Madagascar.

MASHINDANO ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kifupi Afcon yanazidi kutia fora Misri.

Kanda hii yetu ya Afrika Mashariki ikiwakilishwa na nchi nne zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda na Burundi.

Hadi kwa sasa nchi ambayo imefuzu na kuingia kwa raundi ya kumi na sita bora kutoka kanda hili ni Uganda Cranes ambao ipo katika Kundi A, kundi ambalo liko na mwenyeji Misri ambao pia wameshaafuzu.

Timu nyingine za kundi hilo, DR Congo na Zimbabwe ambayo imeshaondolewa katika mashindano hayo.

Uganda ilipoteza mechi dhidi ya Misri kwa mabao mawili kwa bila.

Hata hivyo alama nne ilizokuwa nazo ziliwawezesha kufuzu kutoka katika kundi hilo. DR Congo iliilaza Zimbabwe mabao 4-0 katika mechi ya mwisho ya kundi hilo.

Wakati hayo yakitendeka, Nigeria ambayo nilikuwa nimeipigia upatu wa kufuzu kama ya kwanza kutoka katika Kundi la B ilipoteza mechi yake dhidi ya Madagascar, kwa kichapo cha mabao 2-0.

Madagascar ikumbukwe ndio mara yake ya kwanza kabisa kushiriki katika mashindano haya. Imewashangaza wengi mno. Kweli kujiamini kunahitaji roho kama ya Madagascar.

Kumbuka katika kundi hilo kulikuwa na Guinea na Burundi. Kwa Madagascar kufuzu kutoka kundi ambalo lilikuwa na Guinea inafaa kuvuliwa kofia. Hongera sana kwao.

Wakati nikiingia mitamboni vijana wetu wa kanda hii, Kenya na Tanzania ambao wako katika Kundi C walikuwa wanajitayarisha kuingia uwanjani. Kundi C linajumuisha Algeria, Senegal, Tanzania na Kenya.

Nikiingia mitamboni Algeria ilikuwa inaongoza kundi hilo ikiwa na alama sita, Senegal alama tatu, Kenya alama tatu na Tanzania haikuwa na chochote. Mechi bab’kubwa dhidi ya Kenya na Senegal.

Yoyote itakayopata ushindi hapo basi haina budi kujiunga na Algeria. Tanzania nayo kwa sababu ya heshima ni lazima angalau ingepata alama hata moja tu kutoka kwa mechi yake ya mwisho dhidi ya Algeria.

Nikiingia mitamboni mechi hizi hazikuwa zimechezwa. Yote tisa kazi ipo kwa timu zetu kutoka kanda hili.

Mechi kati ya Kenya na Tanzania ilikuwa moto kwelikweli na natumaini hayo makali watayapeleka katika mechi za mwisho za makundi. Nasubiri kuona ni yupi hasa atajiunga na Uganda kwa raundi ya kumi na sita bora. Tayari Burundi imeyaaga mashindano hayo.

Kenya ilikuwa ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu iwapo ingelazimisha sare yoyote ile katika mechi yake dhidi ya Senegali. Kazi ilikuwapo kwa mabeki wa Harambee Stars kumsimamisha Sadio Mane, mshambuliaji wa Klabu ya Liverpool ya Ligi Kuu England ambaye anasaka bao lake la kwanza kwa mashindano hayo.

Bado Mane hadi jana alikuwa hajatikisa nyavu hadi sasa. Mwenzake, Mohamed Salah tayari ashacheka na nyavu mara mbili. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake wakati atapatana na kikosi ambacho kina motisha cha Harambee Stars. Kenya tuliwategemea Olunga na Wanyama kuibeba nchi. Kazi ilikuwapo kwelikweli.

Na lazima walitusikiza hawa Wasenegali. Hakika hakukuwa na mbuzi kuruka kamba.

Wakati huohuo natuma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa mwendazake Bob Collymore ambaye alikuwa bosi wa Safaricom nchini Kenya.

Safaricom imekuwa mojawapo ya kampuni ambazo zimekuwa zikikuza vipaji vya soka humu nchini. Alifariki jana asubuhi jijini Nairobi. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Bob Collymore alifariki dunia asubuhi ambapo taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Safaricom, Nicholas Nganga ilisema alikuwa anasumbuliwa na saratani kwa muda mrefu.

“Oktoba 2017 alienda Uingereza kwa matibabu na akarejea Julai 2018 kuendelea na majukumu yake huku akihudhuria hospitali kila ilipobidi. Mara ya mwisho alikuwa anatibiwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan hapa Nairobi kabla hali yake haijawa mbaya zaidi,” Nganga akasema katika taarifa yake.

Raia huyo wa Uingereza ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Saratani nchini Kenya, ameacha mke, Wambui Kamiru na watoto wanne.

Kifo cha Collymore (61), kimetokea mwezi mmoja kabla hajastaafu kwani alipanga kuachia wadhifa huo Agosti mwaka huu.

Katika kipindi cha uongozi wake katika kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano Afrika Mashariki, Safaricom imeweza kuisogeza mbele huduma ya M-Pesa iliyozinduliwa mwaka 2007, hivyo kuleta mageuzi katika sekta ya fedha Afrika.

Vilevile ameleta mapinduzi katika medani ya michezo kwa Safaricom kuidhamini.

Wakati Safaricom ikisifika barani Afrika na huko duniani kwa ubunifu huo, Collymore ni miongoni mwa watu muhimu katika maendeleo hayo ambayo sasa yanawanufaisha mamilioni ya wananchi huku ikirahisisha huduma za benki za biashara pia.

Tangu alipoanza kuiongoza kampuni hiyo mwaka 2010, Collymore amaeifanya Safaricom kuwa kampuni kubwa nchini Kenya inakohudumia wateja wawili katika kila watu watano wanaotumia simu za mkononi. Alikuwa anasifika kwa wanamichezo kuingilia kati kunusuru mashindano mbalimbali ya michezo.

ADVERTISEMENT