In Summary

Starlets ambayo imepangwa kundi B, itaondoka nchini, Novemba 14 kuelekea Accra Ghana, kwa ajili ya AWCON, ambapo Novemba 18, wataanza kampeni yao dhidi ya Banyana Banyana ya Afrika Kusini. Kenya wako kundi moja pamoja na mabingwa watetezi Nigeria, Zambia na Afrika Kusini.

Nairobi, Kenya. Timu ya taifa ya wanawake ya Ghana, Black Queens, imetua nchini muda mfupi uliopita kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Harambee Starlets, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AWCON).

Ghana ambao ni wenyeji wa michuano hiyo, itakayotimua vumbi kuanzia Novemba 17 hadi Desemba mosi mwaka huu, wanatarajiwa kufanya mazoezi mepesi kabla ya kuwavaa Starlets.

Black Queens ambao wametoka kuambulia kipigo cha 3-2 kutoka kwa Zambia, watakutana na kikosi cha vijana wa David Ouma ambao walitia aibu jana baada ya kuruhusu kipigo cha 3-1 kutoka kwa wadogo zao, timu ya U-15.

Mechi dhidi ya Ghana itakuwa ni mechi ya tatu ya kujipima ubavu kwa Starlets, kwani mechi ya kwanza waliifunga kikosi cha ligi kuu ya wanawake 1-0, kabla ya jana kuburuzwa 3-1 na wadogo zao (U-15). Baada ya hapo, Harambee Starlets watawavaa Uganda Crested Cranes, Novemba 7, kabla kumalizana na Zambia.

ADVERTISEMENT